*ANGA LA WASHENZI --- 26*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Ugomvi ukazuka.
Wakavutana nje wapate kuonyeshana. Nyama za bodyguard zikamfanya aamini kwamba anaweza kumdhibiti Lee mwenye mwili wa sisimizi.
Bahati kabla hawajaanza pambano, Lee akamshuhudia mwanamke yule aliyekuwa anamtaka. Alikuwa yupo na mwanaume fulani hivi wakifuata mlango wa kuzamia klabu. Lee akaachana na baunsa yule, akakimbilia kwa yule mwanamke.
Akamdaka mkono na kumvuta.
“Unanikumbuka?”
ENDELEA
Mwanamke akaigiza hamjui Lee. Alimtaka mwanaume huyo amwachie mkono wake kabla hajamuitia mwizi. Lee akajikuta anatabasamu. Wakati huo na yule mwanaume aliyeongozana na mwanamke huyo anataka kuchukua hatua dhidi ya Lee.
“Sitaki ukorofi wowote. Ninachotaka ni pochi yangu na vile vilivyomo ndani tu. Sina shida na pesa bali nyaraka.”
Bado mwanamke akang’ang’ania msimamo kwamba hana chochote cha Lee. Yule ‘bwana’ aliyekuwa ameambatana na mwanamke huyo akamtaka Lee aondoke na awaache waendelee na mambo yao.
“Tumekuja hapa kustarehe, si kupigana.”
Lee akashindwa kuzuia hasira zake, akamvuta kwanguvu yule mwanamke upande wake kisha akamchakaza mwanaume yule mwambatanizi kwa muda usiozidi dakika moja! Mikono na miguu yake ilikuwa mepesi kana kwamba inaendeshwa na mota.
Haraka naye baunsa akasonga kukata ngebe. Alichokumbana nacho lazima akahadithie nyumbani kwa mkewe.
Alijikuta anashikilia shingo yake kwa maumivu makali, mbavu zikiwa zimetepeta na yupo chini! Kama ungemuuliza ni kwa muda gani amepigwa hivyo, asingekuwa na jibu moja.
Lee akahepa zake kufuata gari watu wakimtazama kwa mshangao. Hakuna aliyethubutu kuhangaika naye.
Akapeleka gari mpaka nyumbani kwa huyo mwanamke akiamuru apewe pochi haraka iwezekanavyo. Hakuwa na hata tone la utani!
Mwanamke akiwa analia kwa hofu, akatafuta pochi ndani lakini hakuikuta. Akahisi anauawa. Mbona pochi ilikuwepo jana? Alijiuliza akihangaika na mikono yake inayotetemeka.
Hakuona kitu.
Macho yake yakiwa mekundu, akamwambia Lee ya kwamba hajapata kitu.
“Sitaki ujinga na tusipotezeane muda. Naomba pochi!”
Katika kuchambua fikira zake, mwanamke akakumbuka jana alimleta mgeni chumbani hapo. Pengine yeye ndiye atakuwa kaichukua.
“Twende kwake,” Lee akasema haraka. Na pasipo kupoteza muda wakaenda mpaka kwa mwanaume huyo. Uzuri mwanamke alikuwa anapafahamu. Ni mwanaume mteja wake wa enzi, mara zingine huwa anaenda kwake huduma ikiwa inahitajika.
“Naomba niende kuongea naye,” mwanamke akasema walipofika kwenye chumba cha mlengwa wao. Lee akakataa na kutaka waende pamoja kwa kuogopa kutiwa mchanga wa macho.
Akiwa yupo nyuma, akaongozana na mwanamke huyo mpaka mlangoni, akagonga na uzuri kuna mtu akawapokea, japokuwa hakuwa mlengwa wao. Alikuwa ni mwanamke mnene mweupe aliyevalia khanga.
Alitoka usingizini na ugeni ule ulimshtua. Lee akaeleza haja yake, lakini mwanamke yule akamwambia hawezi kumsaidia kwani mwenyewe hayupo.
Lee hakutaka kungoja, akazama ndani kwa mabavu. Akasaka chumba na kukuta pochi yake mezani. Akaipekua, akakuta hamna kitu! Basi asipoteze muda hapo, akachukua picha moja ya mwanaume aliyoikuta mezani, pasipoti, kisha akamrudia yule mwanamke mnene na kumuuliza:
“Atakuwa ameenda wapi?”
“Sijui!”
“Mimi najua atakapokuwa mida hii,” akadakia mwanamke aliyekuja na Lee. Basi pasipo kukawiza, wakaenda kwenye gari na safari ikaanza.
“Anapenda kwenda sana viwanja. Kama hayupo Ambiance, basi atakuwa Billicanas.”
Wakaanzia Ambiance, wakahaha klabu nzima. Hapo ndiyo yule mwanamke akajua namna gani Lee alikuwa anamaanisha kutafuta kile kilichomo ndani ya pochi. Alijiuliza ni nini hicho na thamani yake.
Mungu alikuwa upande wao, wakampata. Mwanamke alimnyooshea Lee kidole na kumnong’oneza kuwa ndiye wanayemtafuta.
“Naomba vitu vilivyokuwemo kwenye hii pochi,” Lee alienda moja kwa moja kwenye mada akiwa anamtazama mlengwa wake: mwanaume mwenye mwili kiasi, mweusi na nywele nyingi zilizo hovyo.
Mwanaume yule akaleta nyodo. Akasema vyote vilivyokuwemo amevitupa maana hakuona kama vina umuhimu. Lee akakasirika sana, lakini mwanamke yule akamvutia kando na kumsihi:
“Usianzishe ukorofi hapa. Niachie hiyo kazi n’takufanyia pasipo kutoa jasho.”
“Ndani ya muda gani?”
“Nipe siku moja tu.”
Lee pasipo kuaga, akaondoka zake baada ya kumkata jicho mwanaume yule ambaye alikuwa tayari ameshaita jamaa zake kwa ajili ya shari. Alimwacha mwanamke aliyekuja naye hapo asionekane kama aliyepotea.
Akasonya kabla hajakanyaga pedeli ya mafuta.
***
Saa mbili asubuhi …
“Nitakuchek baadae,” Jona alituma ujumbe mfupi kwenda kwenye namba aliyoitunza kwa jina la Jumanne. Akaweka simu kando na kupasulia mayai mawili kwenye frampeni.
Alikuwa amevalia bukta ya bluu akiwa kifua wazi. Akili yake ilikuwa inawaza mambo kadhaa, la kwanza juu ya usalama wake. Na pia juu ya Miriam wa mheshimiwa Eliakimu.
Alikuwa ametenga siku hiyo mahususi kwa ajili ya kupembua, kupanga na kuamua juu ya hatma ya maisha yake kutokana na yanayoendelea kwani hata kipofu angelijua ya kwamba kwa sasa yupo vitani.
Alikaanga mayai yake akayala pamoja na sharubati. Bado akiendelea kutafakari. Akatathmini maisha yake na tathmini hiyo akaenda kuirejelea kwenye makaratasi yake meupe anayotumia kuchora. Hapo akaandika na kuchora kila ambalo lilikuwa linazingira maisha yake.
Kuanzia sakata la kifo cha mke na mtoto wake, biashara yake kufa, picha, Eliakimu, Miranda na Kinoo, Bigo, na mauaji yale yote aliyopata kukumbana nayo. Je vitu hivyo vitakuwa vina mahusiano? Akajiuliza na nafsi yake.
Akachoropoa chupa kubwa ya mvinyo alafu akagida akiendelea kutafakari. Mwishowe alipomaliza chupa nzima, akapitiwa na usingizi baada ya kichwa kuwa kizito.
Alipokuja kuamka yalikuwa majira ya jioni, na simu yake ilikuwa na jumbe nne, tatu toka kwa Miriam na moja toka kwa Jumanne. Kabla ya kusoma jumbe hizo akaoga, alafu akavaa na kutoka ndani mpaka baa iliyokuwepo karibu.
Akaagiza maji makubwa tu, alafu ndipo akatoa simu na kuanza kuhangaika nayo.
“Am in Dar,” (Nipo Dar) alituma ujumbe kwenda kwa Miriam. “Where are you now? When shall we meet?” (Upo wapi saa hii? Lini tutakutana?”)
Hakutaka kungoja. Alitaka sasa kufanya mambo haraka aone matokeo yatakuwaje. Hakuona haja ya kungoja ngoja kuumiza tumbo.
Alipotuma ujumbe huo, akaufungua na ujumbe wa Jumanne.
“Mbona kimya? Kuna mtu amekuja kukuulizia hapa?”
“Nani huyo?” Jona akatuma ujumbe kuuliza.
“Hajajitambulisha,” Jumanne akajibu. “Ni jamaa fulani hivi mwembamba.”
“Alikuja na usafiri?”
“Sijajua. Sikumwona na usafir”
Jona akajiuliza juu ya mtu huyo. Inawezekana akawa ndiye yule anayetaka kummaliza? Akajikuta anatikisa kichwa. Wa kwanza alikuwa Bigo, na sasa huyu.
Suluhisho siyo kummaliza, bali kuukata mzizi kabisa. Endapo akifanikiwa kummaliza huyo anayemtafuta, bado atatumwa mwingine … na mwingine na mwingine. Basi kwakuwa Miranda na Kinoo wanafahamu kuhusu hawa watu, hana budi kuwawahisha kaburini upesi.
Akanywa maji yake. Muda si mrefu, akapokea ujumbe toka kwa Miriam. Alikuwa amefurahi sana kusikia taarifa ya ‘mtu’ wake kuwapo Dar es salaam. Wakaongea kidogo na akajieleza wapi alipo, wakapanga pia pa kukutania.
“I think tomorrow I’ll be free.” (Nadhani kesho nitakuwa huru.) aliandika Jona. Akapata uhakika wa kuonana Miriam.
Baada ya hapo akampigia simu Miranda na kumtaka waonane kesho yake jioni kwani kuna jambo la kuliongelea na kuliweka sawa.
-----
Siku iliyofuata, Lamada hotel, majira ya saa sita mchana.
Jona alikuwa tayari ameshampanga Miriam kwamba wakutane hapo. Miriam alifika hapo hotelini na gari nyeupe Nissan Murano akiwa amevalia suruali ya kitenge. Karibu na mabwawa ya kuogelea, akaketi hapo na kuanza kuteta na Jona kwa kupitia simu.
Hakufahamu kwamba Jona alikuwa tayari ameshafika eneo hilo, na alikuwa anamtazama.
Baada ya muda mchache Jona akajitokeza na kusogea papo baada ya kuhakikisha kwamba Miriam alikuwa mwenyewe, hamna kampani. Akaketi na kujitambulisha kwa jina la Roden, na kitambulisho cha polisi akatoa kotini.
“Usijali, na wala usihofu. Sina haja wala nia ya kukuumiza,” akasema Jona akimtazama Miriam ambaye uso wake ulikuwa mweusi kwa hofu. Hata mwili wake ukitetemeka.
Jona akasema ametumwa na Eliakimu na yupo pale kwa lengo moja tu, la kumtwaa na kumpeleka huko. Miriam akatikisa kichwa upesi, akamwomba Jona kumwachia huru kwani kumpeleka kwa Eliakimu ni sawa na kumpeleka kwenye domo la simba mwenye njaa.
“Nipo radhi kwa lolote ila si kunipeleka huko. Nakuomba, nipo chini ya miguu yako.”
Hii ikawa fursa adhimu sana kwa Jona kutimiza malengo yake. Akaanza kumpeleleza na kumdadavua Miriam kwa undani. Akahakikisha anapata kile ambacho Eliakimu anamficha.
Alimtaka Miriam afungue simu yake na kumkabidhi. Miriam akafanya hivyo na kinyume na matarajio yake kwamba Jona ataenda kwenye uwanja wa ujumbe, mwanaume huyo akaenda mtandaoni na kupakua kitu fulani na kukitunza kwenye simu ya Miriam. Kisha akairejesha simu na kuendelea na maongezi.
Tukio hilo lilichukua sekunde ishirini tu kisha akaendelea na maongezi.
Lakini wakiwa katikati ya maongezi hayo, Jona akasikia sauti ya kike nyuma yake ikinong’oneza kumwamuru asimame akiwa amenyoosha mikono juu! Haikujulikana ni wapi mwanamke huyo ametokea.
Kwa ustadi mwanamke huyo aliambaa na ukuta na kuhakikisha hagundulikani na yeyote yule. Nywele zake ndefu za bandia zilizozonga uso wake ukijumlisha pia na miwani ya macho, haikuwa rahisi kumng’amua.
Miriam alimwona mwanamke huyo ila alidhani ni mpita njia. Kumbe alikuwa Nade, na ndani ya koti la zambarau alilolivaa alikuwa ameweka bunduki yake ndogo ambayo kwa sasa mdomo wake ameuminyia kwenye mbavu za Jona. Bado bunduki akiwa ameifichia ndani ya koti.
Haraka akampekua Jona na kubeba bunduki yake kisha akamtaka asogee mbali na Miriam asogee upande wake haraka. Matukio hayo yakafanikiwa ndani ya muda mchache mno! Nade akatoka na Miriam ndani ya hoteli.
Wakajipaki ndani ya gari, wakayoyoma! Jona akawatazama namna wanavyoishilia. Akatabasamu na kusema:
“Kama ilivyopangwa.”
Nade pasipo kujua alikuwa ametanguliwa hatua mbili mbele.
.
.
.
***