*ANGA LA WASHENZI –24*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Wakangoja na masaa yakazidi kwenda mpaka saa saba usiku, mwanamke yule hakuonekana. Saa nane … saa tisa, kimya.
“Imekula kwetu,” Nigaa akasema.
“Sasa nafanyaje?” Lee akauliza.
“Inaonekana hili zoezi litatuchukua zaidi ya leo hii.”
ENDELEA
Walikaa hapo mpaka kwenye mishale ya kukaribia asubuhi pasipo kumwona mtu wanayemngoja. Waliamua kutia moto chombo na kwenda zao. Lee akiwa na mawazo na majuto.
Akitafakari na kudadavua kichwani. Akitanabahi ni njia gani ya kuenenda pasipo kupata majibu yoyote yale. Aliwaza endapo mkuu wake akipata habari hizi, nini kitatokea.
Hakuna kingine zaidi ya kifo.
“Nigaa, naomba ushike usukani,” alisema Lee akiegesha gari pembeni. “Sijisikii vema.”
“Usiwaze sana, Lee. Huyo malaya tutampata tu,” Nigaa alimpa Lee moyo.
“Shida si kumpata, Nigaa. Bali yale yaliyomo mule kwenye pochi kama yatakuwepo salama. Sijawahi kufanya uzembe wa aina hii.”
Nigaa alichukua usukani wakaendelea na safari mpaka kwenye makazi yao ambapo waliamua kupumzika kwanza kabla ya baadae kuendelea na kazi zingine. Haswa ya kwenda kuonana na mkuu wao awaeleze kumhusu mtu yule ambaye Bigo alitumwa akammalize.
Kwenye majira ya saa nane mchana wakawa tayari wameshaamka na kujumuika na mwenzao aitwaye Mombo wakaenda kuonana na mkuu wao.
Wakamweleza haja ya mioyo yao. Mkuu akawataka watulie kwani tayari hilo jambo ashalichukulia hatua.
“Wŏ yĭjīng fāle lìng yīgè rén,” (Tayari nimeshamtuma mtu mwingine,) alisema mkuu akikuna kidevu chake chongofu. “Ràng wŏmen kàn kàn hui fāshēng shènme.” (Acha tuone nini kitatokea.)
Kwahiyo hapo wakawa hawana tena kauli mpaka pale yule aliyetumwa arejeshe taarifa ama naye atokomee ndipo mkuu achukue hatua nzito.
Kwasababu Jona ni mchoraji tu, hamna haja ya kuhofia sana mpaka kutuma kikosi kamili.
Mwanaume aliyetumwa alijulikana kwa jina la Panky. Mwanaume fulani mwembamba urefu saizi ya kati. Kichwani mwake alikuwa ana nywele zilizochongwa kama mtaro zikiwa zimesimama kama moja.
Kwa shingo upande Lee na wenzake wakaridhia. Ila kabla hawajaondoka, mkuu akauliza:
“Lee, nĭ hái hăo ma?” (Lee, upo sawa?) Akimtazama Lee machoni. upesi Lee akatazama chini na kutikisa kichwa chake kuridhia ya kwamba alikuwa sawa. Wakatoka nje.
***
Saa nane mchana …
“Vipi upo poa now?”
“Ndiyo, nadhani nina muda sasa. Tunaweza tukaenda.”
“Saa hii?”
“Ndio. Au wewe ulikuwa unataka twenda muda gani?”
“Usiku. Bila shaka ndiyo muda atakaokuwa nyumbani.”
“Unajua usiku nina miadi na Boka. Siwezi kwenda, kama unavyojua kuna ishu nataka nichonge naye.”
“Lakini sidhani kama muda huu atakuwepo nyumbani. Mchana huu.”
“Basi fanya hivi, si upo town, pitia pale ofisini kwake umcheki.”
“Nipe kama robo saa.”
“Iwe kweli.
Baada ya robo saa …
“Hayupo!”
“Pamefungwa?”
“Hapana. Yupo yupo mshkaji mwingine.”
“Muulize basi.”
Punde, Kinoo anashuka kwenye gari na kufuata ofisi ya Jona. Alimkuta Jumanne pekee ambaye alimsalimu na kumuulizia Jona.
“Atakuwa yupo kwake, jana na leo hajafika job. Ila naweza nikakusaidia.”
“Usijali,” akajibu Kinoo. “Nilikuwa namhitaji yeye mwenyewe.”
Akarudi kwenye gari na kumtumia Miranda ujumbe:
“Tuelekee nyumbani.”
“Poa, nipitie nipo tayari,” ujumbe ukajibu.
____
Saa nane na dakika hamsini na tano …
Jona alikuwa amevalia bukta na kaushi nyeupe. Kuna baadhi ya michoro alikuwa anaiweka sawa kwenye ubao wake wa karatasi, michoro ambayo kwa kuitazama upesi huwezi jua alikuwa anachora nini hasa.
Alisikia hodi getini, akaacha shughuli yake na kuangaza dirishani. Akaona Range Rover sport nyeupe. Akashtuka kidogo. Alijua usafiri huo ni wakina nani. Basi akaenda chumbani na kukwapua bunduki yake aliyofichia nyuma ya kiuno akiijaladia na shati jeusi.
Kwa kujiamini akalifuata geti na kuwaruhusu wageni waingie ndani.
“Hatujaja kwa shari, bali maongezi,” alisema Miranda. Mwanamke ndani ya sketi fupi nyeusi na topu ya pinki. Akiongozana na Kinoo mwenye nguo zijulikanazo kila uchwao.
Jona akawakaribisha sebuleni akiketi kwenye kiti cha kando kilichoruhusu kila mmoja kumtazama mwenzake.
“Karibuni japo ujio wenu haukuwa na taarifa. Natumai mlikuwa mnajua kama nipo nyumbani.”
“Ndio, tulipitia kazini kwako.”
Pasipo kupoteza muda Miranda akaeleza kilichowaleta. Ya kwamba ni picha na baadhi ya taarifa ambazo wanataka kumfikishia Jona.
Wakamwambia kuhusu msako ule wa picha, haswa wakiuhusisha na kundi la kihalifu la kichina ambalo lipo nyuma yake. Ya kwamba picha ile ni mali yao, wanaitafuta na kwa gharama yoyote ile wataipata.
“Uhai wako upo hatarini. Watu hawa hawatakoma kutuma watu wao mpaka pale watakapohakikisha wameitia hiyo picha mkononi. Japokuwa hatujawahi kuiona hiyo picha, tunaamini itakuwa na nyaraka muhimu sana kwao. Na ndiyo maana nasi twaisaka.”
Huu ukawa muda muafaka kwa Jona kuuganisha tarifa zake kichwani na kupata mantiki. Ina maana wageni wake hawa wanawafahamu hawa wachina ambao alikuwa anahangaika kufumbua fumbo?
Hawa wachina ambao wamefanya mauaji ya watu kadhaa!
Kabla hajaongelea picha, akawauliza wakina Miranda kama wanafahamu lolote juu ya kifo cha bwana Fakiri na Jigeleka. Wakasema hawafahamu. Jona akawaambia ni kwa namna gani amepata taarifa za hao marehemu.
“Nilikuta picha zao kwenye hifadhi ya mtumishi wao.”
“Bila shaka walikuwa kwenye pumzi zao za mwisho,” akasema Miranda. Jona akakumbuka neno hilo ‘pumzi ya mwisho’. Ni neno la kichina lililoandikwa kwenye picha za watu wale aliowaona kwenye paspot.
“Unajua lolote kuhusu pumzi ya mwisho?” Akauliza.
“Ndio, najua. Ni kikosi cha mauaji kinachohusika na mauaji ya wale wote wanaoleta kizingiti mbele ya kazi yao. Kikosi hichi kinaundwa na watu stadi wa kazi. Wenye uwezo wa kuua pasipo kubakiza ushahidi wala kielelezo.”
“Na unajua kilichomuua bwana Jigeleka?”
“Hapana, sijajua. Wanaua watu wengi, siwezi nikajua haswa kwanini kila mmoja huuawa.”
Baada ya Jona kuuliza maswali ya kutosha, akataka kujua kwa undani juu ya wakina Miranda, wao ni wa kina nani haswa na wanajishughulisha na nini. Miranda akajibu kwa ufupi kwamba wao ni wafanyabiashara, wakihusika na biashara za kuingiza madawa nchini, madawa ya afya wakiwa na ubia na MSD.
“Makajuanaje na hawa wachina?” Jona akauliza.
“Kwasababu walikuwa ndiyo wapinzani wetu kibiasara. Siku zote rafiki huwa karibu, ila adui karibu zaidi.”
“Sasa picha itawasaidia nini?”
“Kama tulivyosema ni adui zetu. Tunataka kujua kila nyendo yao.”
“Basi?”
“Basi. Hicho pekee ndicho kinatuhusu.”
Jona akakereketwa rohoni. Kwanini watu hawa wanafanya uhalifu nab ado wanadunda mtaani? Kwanini wanaua watu nab ado hawachukuliwi hatua? Alijaribu kuwauliza wakina Miranda, akajibiwa kwa ufupi.
“Mikono na miguu yao ina mafunzo. Akili zao zina ujuzi. Mifuko yao ina pesa.”
Wakateta kwa ufupi kabla Jona hajaenda kuwaletea picha ambayo aliwakabidhi na kuwaambia:
“Mnaweza mkanishrikisha kama kuna jambo mtaling’amua kwenye picha hiyo. samahani sitawapa mwende nayo.”
Miranda na Kinoo wakaridhia.
Wakaitazama picha kwa umakini sana wakila dakika kama kumi na tano. Lakini wakatoka patupu!
“Una uhakika picha yenyewe ni hii?” akauliza Kinoo.
“Ndiyo yenyewe. Sina zaidi.”
Mbona ni picha ya kawaida tu? visiwa na ndege! Wakatahamaki. Hawakujua nini haswa dhamira ya picha ile. Waliona ni kama urembo.
Ila kama isingelikuwa na maana kwanini itafutwe? Kwanini Jona alengwe kuuawa?
“Hamna chochote ulichokipata pichani?” Miranda akamuuliza Jona. Jona akatikisa kichwa.
“Hapana. Nikadhani pengine nyie mwajua.”
Wote walitota. Hakuna aliyeona cha maana. Ila Jona akasisitizia lazima picha hiyo itakuwa na maana, hawana budi kufuatilia.
“Nakumbuka wakati Bite ananiambia nimchoree hii picha alinipa maelezo very simple, ila alitaka niyafuate na kuyazingatia haswa. Nilirudia kuchora picha hii mara tatu, tena kwasababu ndogo ndogo sana, mara ndege wamekaa mbali, niwasogeze, ama visiwa ni virefu sana na kadhalika. Bila shaka alikuwa na maana yake.”
Mwishowe Jona akawakabidhi wakina Miranda picha nyingine, kopi ya ile orijino ambayo aliichora kwa penseli na karatasi, wakakubaliana yeye abakie na ile orijino.
“Jona,” Miranda akaita. “Wewe ni nani?” Akauliza. Jona akatabasamu kwanza kabla ya kujibu kwa kuuliza:
“Kwanini wauliza?”
“Kwasababu wewe si mchoraji pekee. Wewe ni nani?”
Jona hakutaka kusema mambo mengi, akawaambia hayo mengine yatakuja kadiri na muda.
“Kuwa makini sana,” Miranda akamsisitizia Jona.
“Usijali,” Jona akamjibu. “Naweza kujitazama vema.”
_____
Robo saa mbele...
"Mkuu, kuna jambo lipo katikati ya Jona na na wakina Miranda,"Nade akatoa taarifa. Wakati huo alikuwa amejiweka kando kidogo ya nyumba ya Jona macho yake ndani ya miwani yakiwa yanaangaza kutazama gari, Range Rover sport nyeupe, ikiishilia.
"Ndio, nimewaona wakiingia ndani ya nyumba ya Jona," akasema Nade sasa akianza kuchukua hatua kusonga mbali na nyumba ya Joana.
"Wametoka muda si mrefu. Wamedumu kwa muda wa kasoro lisaa."
Akasikilizia kidogo, kisha akasema:
"Sawa, mkuu. Ila inakuwa ngumu kujua wanachokiongelea. Nahofu isije ikawa ni kuhusu Miriam."
Kimya kidogo akisikilizia. Kisha akasema:
"Sawa, mkuu. Jicho halitafunga."
Akakata simu. Ila mara akasikia mkono wa mtu begani. Haraka akageuka.
Kutazama alikuwa ni Jona!
.
.
.
***