*ANGA LA WASHENZI – 29*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
“Yule mfanyakazi wa marehemu Bite!” Sarah akamkubusha. Sasa Kinoo akamkumbuka. Alikuwa ni mmoja wa wale mapacha wawili aliwaona kwenye kikao cha siku ile.
Amepata wapi namba yake na alikuwa anataka kumwambia nini? Akajiuliza upesi akijtengenezea kitako. Sarah akamwambia juu ya mauaji ya Mudy. Kinoo akashtuka sana! Sarah akamwambia na mpaka kuzikwa alishazikwa. Kilichomfanya akampigia ni kutomuona msibani.
Kisha simu ikakata!
ENDELEA
Kinoo akafanya mpango wa kuongeza salio alafu akamtafuta tena Sarah na kumuuliza juu ya makazi yake. Sarah akamwelekeza na Kinoo akamuahidi kwenda kumtembelea muda si mrefu. Haitazidi lisaa.
Kinoo akajiandaa, kwa kutinga kibodi chake cheusi na suruali ya jeans, akabebelea bunduki ndogo na kisha kujipaki kwenye pikipiki yake kubwa na safari ikaanza. Huko barabarani kulikuwa kuna magari machache, muda wa foleni ulikuwa umeshapita.
Hakuchukua muda mrefu sana mpaka kuwasili alipoelekezwa na Sarah, maeneo ya Sinza Palestina. Akakuta gari, VX ya grey, nje ya makazi hayo.
Gari hili halikuwa jipya machoni. Akatafakari kwa muda mfupi na jibu akalipata, aliliona siku ile ya kikao! La nani?
Lilikuwa ni gari la Brokoli! Akili yake ikalipuka. Haraka akaficha pikipiki yake ubavni mwa nyumba na kulifuata gari lile karibu. Akatambua limekuja hapo muda si mrefu. Lilikuwa na joto kubwa.
Basi akasogelea dirishani ambapo angeweza kusikia chochote kitu toka ndani. Alikuwa na hamu ya kujua nini kimemleta Brokoli hapo. Walikuwa na ajenda gani wanayojadili?
Kwa akili ya Kinoo akafahamu fika kuwa ujio ule wa Brokoli ulikuwa ni wa ghafla. Laiti kama Sarah angelikuwa anaufahamu, basi angelimtaarifu.
Akatazama ndani asione kitu, ila akasikia sauti ya Brokoli ikinguruma. Maneno mengi hayakuwa anayasikia vizuri. Ila kwa sauti na namna yalivyokuwa yanatamkwa, yalikuwa ni maagizo ama matisho. Akili ya Kinoo ikasema vivyo.
Kwa dakika kama tano mbele, akasikia sauti ya vishindo vya miguu inasogea. Haraka akajificha na kuchngulia. Akamwona Brokoli aliyekuwa amevalia Kaunda suti ya kahawia akiingia kwenye gari na kuhepa.
Akatoka mafichoni na kwenda kukutana na Sarah. Alikuwa ameketi sebuleni akilia. Macho yake yalikuwa mekundu na nywele zake hazikuwa mpangilioni. Sasha hakuwepo, yeye alisafiri.
Kinoo akamuuliza kwanza juu ya ujio wa Brokoli hapo, haswa muda huo na kwanini analia. Sarah akamwambia ya kwamba ameacha kazi, na hataki tena! Akiwa anapaliwa na kilio hakuwa anaongea vema.
Kinoo akawa ana kibarua cha kumbembeleza.
“Amesema hataki kuona yeyote yule anasumbuka wala kusema chochote kuhusu kifo cha Mudy. Amefuatilia polisi na amewaachia kesi huko. Nimemwambia naacha kazi, akaniambia niache na kila kitu. Asije akasikia nimesema chochote kinachohusu ofisi. Nikithubutu, nitakiona cha mtema kuni!”
Kinoo akastaajabu. Na pamoja na Sarah wakamshuku Brokoli kuhusika na kifo cha Mudy. Na hata vile vile mkono wake utakuwemo kwenye kifo cha Bite.
“Vifo vyao vinafanana. Nahofia nisije nikawa anayefuata,” alisema Sarah akilowanisha macho yake kwa machozi.
Akamwonya na Kinoo kuwa hayupo salama, inabidi awe mwangalifu sana.
“Kuna taarifa amesema Mudy alizichukua kule ofisini na kumkabidhi mtu mwingine, jina hakumtaja. Na taarifa hizo ni nyeti. Bila shaka mtu huyo atakuwa ni wewe.”
Kinoo akakiri. Na akamwambia wamefuatilia nyaraka hizo na kugundua zina mahusiano na shirika fulani, tawi la kampuni kubwa ya kichina. Hapo Sarah akagutuka na jambo.
“Wachina?” Akauliza.
“Ndio, wachina. Unawajua?” Kinoo akatia swali.
Sarah akasema hawajui ila alikuwa anawaona mara kadhaa pale ofisini wakija kuteta na Bite. Na hata kwenye baadhi ya vikao walikuwa wanahudhuria. Ila hawakuwahi kujua wanahusika na nini.
“Hatujawahi kupewa mrejesho wa vikao vyao. Walikuwa wakivifanya kwa siri,” alisema Sarah. “Kikao cha mwisho wachina hao walikaa pamoja na Bite na Brokoli, ndipo likapita juma moja na Bite akauawa.”
Kinoo akamuuliza Sarah kama kuna chochote anachokijua baina ya pande hizi mbili, wachina na Bite. Walikuwa wana mahusiano gani na nini kiliwaunganisha. Sarah akasema hajui lolote zaidi ya wachina hao kuwa ‘partners’ wa mbali.
Kwa usalama, Kinoo akamshauri aondoe makazi yake hapo maana hawezi jua nini Brokoli amelenga kumfanyia. Sarah akasema hana pa kuelekea. Hana makazi mengine mbali na hayo na ndiyo hivyo kazi ameshaikataa.
Kinoo akapendekeza akakae kwake kama hatojali. Sarah akakubali baada ya mafikirio kidogo. Akabeba nguo zake chache alafu wakaondoka na Kinoo.
***
Baada ya Jona kutoka mezani kwake, alikwapua ndoo moja ya bati iliyojaa maji, akaongozana nayo mpaka stoo iliyopo nje. Akafungua mlango na kuwasha taa, kukawa na mwanga!
Ndani ya stoo hiyo iliyokuwa na vitu vichache, alikuwa amelala Panky humo akiwa amefungwa miguu na mikono. Kichwani mwake alikuwa na majeraha yaliyoacha kutoa damu.
Jona akammwagia maji kumwamsha. Panky akakurupuka na kutoa macho kumtazama Jona.
“Muda wa kulala umeisha,” Jona akasema akichuchumaa na kumtazama Panky kwa ukaribu. Mwanaume huyo alikuwa amevimba upande wake wa kushoto wa uso.
Jona pasipo kupoteza muda akamuliza ni nini alikuwa anataka kwake na nani amemtuma. Aliyauliza hayo kwa kujua mtu huyo hatasema, na hata mwishowe anaweza akafanya jaribio la kujimaliza kwa kuunyofoa ulimi.
Kama ilivyotarajiwa, Panky akaleta ubishi. Hakuwa radhi kusema chochote kile na yuko radhi kufa. Jona akaendea kidumu cha maji cha lita tano, alafu akachomoa leso ya kufutia jasho mfukoni na kuifungia usoni mwa Panky.
Taratibu akaanza kumwagia maji juu ya leso hiyo, akihakikisha maeneo ya pua na mdomo yanapata maji ya kutosha. Panky akahangaika kuhema. Kila alipovuta pumzi akawa anavuta maji puani na mdomoni.
Akapaliwa na kupata shida mno!
Jona akabandua leso usoni mwa Panky na kumuliza kama yupo tayari kuongea ama lah. Kabla Panky hajajibu akakohoa sana na kuhaha kutafuta pumzi. Lakini akasema hayupo tayari kusema kitu!
Jona asiongee sana, akarudia zoezi lake mara tatu. Panky akashindwa kuvumilia na mara akaanza kuhororoja. Akasema ametumwa na mkuu wake kuja kummaliza.
“Kwasababu gani minimalize?”
Panky akasema hakuambiwa kwa sabab gani amalizwe, ila agizo tu ya kwamba amalizwe. Zaidi ya hapo hakuna anachojua. Yeye ni mtu wa kuagizwa tu na kwenda kutenda.
Jona akamuuliza juu ya makao ya mkuu wake na anajishughulisha na nini. Panky akamtaja mkuu wake kwa jina moja la Sheng’ akisema ni mfanyabiashara wa vipuri vya magari.
Jona akakumbuka jina hilo la Sheng’. Alikuwa ndiye yule mshirika ambaye mke wa Fakiri alimweleza. Akamuuliza Panky juu ya mauaji hayo, Panky akasema hayafahamu.
Hapa Jona akapata maswali, Sheng’ anajihusisha na biashara ngapi? Na imekuaje Panky akasema mambo hayo kwa wepesi hivyo tofauti na Bigo ambaye aliamua kujiua?
Mfukoni akatoa kitambulisho cha kura cha Panky, leseni na makaratasi kadhaa. Akayatazama kwa muda kidogo, kabla hajamuuliza Panky kama anajua lolote kuhusu ‘Pumzi ya mwisho’.
Panky akasema hajui kitu. Jona akahisi anamdanganya. Akamwambia juu ya Bigo na kumgusia juu ya kikundi hicho kuhusika na mauaji. Panky akakiri, lakini akasema yeye afahamu kitengo hicho japokuwa inawezekana kikawa kipo.
“Kuna vikundi vingi ndani yetu, na kila kikundi kina majukmu yake ya kuyatimiza,” alisema Panky ndani ya kamba.
“Na wewe upo kikundi gani kati ya hivyo?” Jona akauliza. Panky akamwambia yupo kwenye kikundi cha ‘Space button’. Kikundi kinachohusika na mambo ya teknolojia, haswa udukuzi.
“Sasa ikawaje ukatumwa kummaliza mtu na ingali si kazi yako?” Jona akauliza.
“Hii ni adhabu nimepewa kwasababu ya kufeli kufanya vema kazi yangu iliyopita. Punde unapokosea, huwa unauawa. Nimetumwa kukumaliza kama namna ya kusahihisha makosa yangu. Ikishindikana basi nifie huko huko kama adhabu yangu inavyosema.”
Jona akafahamu kwanini mateka hyo ameongea kwa urahisi tofauti na Bigo. Hakuwa mtu anayehusika na mauaji bali wa kukaa mbele ya kioo cha tarakilishi. Hata mafunzo ya kujilinda hakuwa nayo na ndiyo maana hakumpatia changamoto pindi anamtia nguvuni.
Lakini Jona akataka kujua ni kosa gani ambalo Panky amelifanya kupelekea kupewa adhabu kama hiyo. Panky akamweleza ni upotevu wa faili moja muhimu sana kwenye mtindo data wao. Faili ambalo hajajua limepoteaje mpaka muda huo.
“Kwanini unaniambia yote haya?” Jona akauliza. Panky akashusha kwanza pumzi yake, na kusema kwa huzuni.
“Najua naenda kufa tu. Angalau nimpe mtu mwanga ama mahali pa kuanzia kuukata mbuyu huu … kama si na wewe, basi nitamalizwa na mkuu wangu. Sina haja ya kufa na taarifa hizi.”
Jona akamwambia hana tatizo naye, atakapopata anachokihitaji, yupo radhi kumwachia. Panky akatabasamu na kutikisa kichwa chake.
“Hata kama ukiniacha hai, sitadumu. Hamna namna ya kumkimbia Sheng’. Hata uwe wapi atakutia tu mikononi na kukumaliza.”
Panky akaongezea ya kwamba pindi unapoingia ndani ya mfumo wa Sheng’, familia yako yote anakuwa anaijua. Watu wako wa karibu na marafiki zako. Ni labda ajue umekufa, na si hai akakukosa!
“Watu kadhaa walishawahi kutoroka, wengine wakitaka kuacha kazi kwa hiyari. Hakuna aliyebakiziwa uhai hata mmoja! Kwa Sheng’ kuna kuingia tu, mlango wa kutokea haupo. Na utakapoulazimisha kuujenga ukutani, basi utalipia gharama zake.”
.
.
.
****