Anga la washenzi na Joana anaona kitu usiku

Anga la washenzi na Joana anaona kitu usiku

*ANGA LA WASHENZI – 29*

*Simulizi za series*


ILIPOISHIA

“Yule mfanyakazi wa marehemu Bite!” Sarah akamkubusha. Sasa Kinoo akamkumbuka. Alikuwa ni mmoja wa wale mapacha wawili aliwaona kwenye kikao cha siku ile.

Amepata wapi namba yake na alikuwa anataka kumwambia nini? Akajiuliza upesi akijtengenezea kitako. Sarah akamwambia juu ya mauaji ya Mudy. Kinoo akashtuka sana! Sarah akamwambia na mpaka kuzikwa alishazikwa. Kilichomfanya akampigia ni kutomuona msibani.

Kisha simu ikakata!

ENDELEA

Kinoo akafanya mpango wa kuongeza salio alafu akamtafuta tena Sarah na kumuuliza juu ya makazi yake. Sarah akamwelekeza na Kinoo akamuahidi kwenda kumtembelea muda si mrefu. Haitazidi lisaa.

Kinoo akajiandaa, kwa kutinga kibodi chake cheusi na suruali ya jeans, akabebelea bunduki ndogo na kisha kujipaki kwenye pikipiki yake kubwa na safari ikaanza. Huko barabarani kulikuwa kuna magari machache, muda wa foleni ulikuwa umeshapita.

Hakuchukua muda mrefu sana mpaka kuwasili alipoelekezwa na Sarah, maeneo ya Sinza Palestina. Akakuta gari, VX ya grey, nje ya makazi hayo.

Gari hili halikuwa jipya machoni. Akatafakari kwa muda mfupi na jibu akalipata, aliliona siku ile ya kikao! La nani?

Lilikuwa ni gari la Brokoli! Akili yake ikalipuka. Haraka akaficha pikipiki yake ubavni mwa nyumba na kulifuata gari lile karibu. Akatambua limekuja hapo muda si mrefu. Lilikuwa na joto kubwa.

Basi akasogelea dirishani ambapo angeweza kusikia chochote kitu toka ndani. Alikuwa na hamu ya kujua nini kimemleta Brokoli hapo. Walikuwa na ajenda gani wanayojadili?

Kwa akili ya Kinoo akafahamu fika kuwa ujio ule wa Brokoli ulikuwa ni wa ghafla. Laiti kama Sarah angelikuwa anaufahamu, basi angelimtaarifu.

Akatazama ndani asione kitu, ila akasikia sauti ya Brokoli ikinguruma. Maneno mengi hayakuwa anayasikia vizuri. Ila kwa sauti na namna yalivyokuwa yanatamkwa, yalikuwa ni maagizo ama matisho. Akili ya Kinoo ikasema vivyo.

Kwa dakika kama tano mbele, akasikia sauti ya vishindo vya miguu inasogea. Haraka akajificha na kuchngulia. Akamwona Brokoli aliyekuwa amevalia Kaunda suti ya kahawia akiingia kwenye gari na kuhepa.

Akatoka mafichoni na kwenda kukutana na Sarah. Alikuwa ameketi sebuleni akilia. Macho yake yalikuwa mekundu na nywele zake hazikuwa mpangilioni. Sasha hakuwepo, yeye alisafiri.

Kinoo akamuuliza kwanza juu ya ujio wa Brokoli hapo, haswa muda huo na kwanini analia. Sarah akamwambia ya kwamba ameacha kazi, na hataki tena! Akiwa anapaliwa na kilio hakuwa anaongea vema.

Kinoo akawa ana kibarua cha kumbembeleza.

“Amesema hataki kuona yeyote yule anasumbuka wala kusema chochote kuhusu kifo cha Mudy. Amefuatilia polisi na amewaachia kesi huko. Nimemwambia naacha kazi, akaniambia niache na kila kitu. Asije akasikia nimesema chochote kinachohusu ofisi. Nikithubutu, nitakiona cha mtema kuni!”

Kinoo akastaajabu. Na pamoja na Sarah wakamshuku Brokoli kuhusika na kifo cha Mudy. Na hata vile vile mkono wake utakuwemo kwenye kifo cha Bite.

“Vifo vyao vinafanana. Nahofia nisije nikawa anayefuata,” alisema Sarah akilowanisha macho yake kwa machozi.

Akamwonya na Kinoo kuwa hayupo salama, inabidi awe mwangalifu sana.

“Kuna taarifa amesema Mudy alizichukua kule ofisini na kumkabidhi mtu mwingine, jina hakumtaja. Na taarifa hizo ni nyeti. Bila shaka mtu huyo atakuwa ni wewe.”

Kinoo akakiri. Na akamwambia wamefuatilia nyaraka hizo na kugundua zina mahusiano na shirika fulani, tawi la kampuni kubwa ya kichina. Hapo Sarah akagutuka na jambo.

“Wachina?” Akauliza.

“Ndio, wachina. Unawajua?” Kinoo akatia swali.

Sarah akasema hawajui ila alikuwa anawaona mara kadhaa pale ofisini wakija kuteta na Bite. Na hata kwenye baadhi ya vikao walikuwa wanahudhuria. Ila hawakuwahi kujua wanahusika na nini.

“Hatujawahi kupewa mrejesho wa vikao vyao. Walikuwa wakivifanya kwa siri,” alisema Sarah. “Kikao cha mwisho wachina hao walikaa pamoja na Bite na Brokoli, ndipo likapita juma moja na Bite akauawa.”

Kinoo akamuuliza Sarah kama kuna chochote anachokijua baina ya pande hizi mbili, wachina na Bite. Walikuwa wana mahusiano gani na nini kiliwaunganisha. Sarah akasema hajui lolote zaidi ya wachina hao kuwa ‘partners’ wa mbali.

Kwa usalama, Kinoo akamshauri aondoe makazi yake hapo maana hawezi jua nini Brokoli amelenga kumfanyia. Sarah akasema hana pa kuelekea. Hana makazi mengine mbali na hayo na ndiyo hivyo kazi ameshaikataa.

Kinoo akapendekeza akakae kwake kama hatojali. Sarah akakubali baada ya mafikirio kidogo. Akabeba nguo zake chache alafu wakaondoka na Kinoo.


***


Baada ya Jona kutoka mezani kwake, alikwapua ndoo moja ya bati iliyojaa maji, akaongozana nayo mpaka stoo iliyopo nje. Akafungua mlango na kuwasha taa, kukawa na mwanga!

Ndani ya stoo hiyo iliyokuwa na vitu vichache, alikuwa amelala Panky humo akiwa amefungwa miguu na mikono. Kichwani mwake alikuwa na majeraha yaliyoacha kutoa damu.

Jona akammwagia maji kumwamsha. Panky akakurupuka na kutoa macho kumtazama Jona.

“Muda wa kulala umeisha,” Jona akasema akichuchumaa na kumtazama Panky kwa ukaribu. Mwanaume huyo alikuwa amevimba upande wake wa kushoto wa uso.

Jona pasipo kupoteza muda akamuliza ni nini alikuwa anataka kwake na nani amemtuma. Aliyauliza hayo kwa kujua mtu huyo hatasema, na hata mwishowe anaweza akafanya jaribio la kujimaliza kwa kuunyofoa ulimi.

Kama ilivyotarajiwa, Panky akaleta ubishi. Hakuwa radhi kusema chochote kile na yuko radhi kufa. Jona akaendea kidumu cha maji cha lita tano, alafu akachomoa leso ya kufutia jasho mfukoni na kuifungia usoni mwa Panky.

Taratibu akaanza kumwagia maji juu ya leso hiyo, akihakikisha maeneo ya pua na mdomo yanapata maji ya kutosha. Panky akahangaika kuhema. Kila alipovuta pumzi akawa anavuta maji puani na mdomoni.

Akapaliwa na kupata shida mno!

Jona akabandua leso usoni mwa Panky na kumuliza kama yupo tayari kuongea ama lah. Kabla Panky hajajibu akakohoa sana na kuhaha kutafuta pumzi. Lakini akasema hayupo tayari kusema kitu!

Jona asiongee sana, akarudia zoezi lake mara tatu. Panky akashindwa kuvumilia na mara akaanza kuhororoja. Akasema ametumwa na mkuu wake kuja kummaliza.

“Kwasababu gani minimalize?”

Panky akasema hakuambiwa kwa sabab gani amalizwe, ila agizo tu ya kwamba amalizwe. Zaidi ya hapo hakuna anachojua. Yeye ni mtu wa kuagizwa tu na kwenda kutenda.

Jona akamuuliza juu ya makao ya mkuu wake na anajishughulisha na nini. Panky akamtaja mkuu wake kwa jina moja la Sheng’ akisema ni mfanyabiashara wa vipuri vya magari.

Jona akakumbuka jina hilo la Sheng’. Alikuwa ndiye yule mshirika ambaye mke wa Fakiri alimweleza. Akamuuliza Panky juu ya mauaji hayo, Panky akasema hayafahamu.
Hapa Jona akapata maswali, Sheng’ anajihusisha na biashara ngapi? Na imekuaje Panky akasema mambo hayo kwa wepesi hivyo tofauti na Bigo ambaye aliamua kujiua?

Mfukoni akatoa kitambulisho cha kura cha Panky, leseni na makaratasi kadhaa. Akayatazama kwa muda kidogo, kabla hajamuuliza Panky kama anajua lolote kuhusu ‘Pumzi ya mwisho’.

Panky akasema hajui kitu. Jona akahisi anamdanganya. Akamwambia juu ya Bigo na kumgusia juu ya kikundi hicho kuhusika na mauaji. Panky akakiri, lakini akasema yeye afahamu kitengo hicho japokuwa inawezekana kikawa kipo.

“Kuna vikundi vingi ndani yetu, na kila kikundi kina majukmu yake ya kuyatimiza,” alisema Panky ndani ya kamba.

“Na wewe upo kikundi gani kati ya hivyo?” Jona akauliza. Panky akamwambia yupo kwenye kikundi cha ‘Space button’. Kikundi kinachohusika na mambo ya teknolojia, haswa udukuzi.

“Sasa ikawaje ukatumwa kummaliza mtu na ingali si kazi yako?” Jona akauliza.

“Hii ni adhabu nimepewa kwasababu ya kufeli kufanya vema kazi yangu iliyopita. Punde unapokosea, huwa unauawa. Nimetumwa kukumaliza kama namna ya kusahihisha makosa yangu. Ikishindikana basi nifie huko huko kama adhabu yangu inavyosema.”

Jona akafahamu kwanini mateka hyo ameongea kwa urahisi tofauti na Bigo. Hakuwa mtu anayehusika na mauaji bali wa kukaa mbele ya kioo cha tarakilishi. Hata mafunzo ya kujilinda hakuwa nayo na ndiyo maana hakumpatia changamoto pindi anamtia nguvuni.

Lakini Jona akataka kujua ni kosa gani ambalo Panky amelifanya kupelekea kupewa adhabu kama hiyo. Panky akamweleza ni upotevu wa faili moja muhimu sana kwenye mtindo data wao. Faili ambalo hajajua limepoteaje mpaka muda huo.

“Kwanini unaniambia yote haya?” Jona akauliza. Panky akashusha kwanza pumzi yake, na kusema kwa huzuni.

“Najua naenda kufa tu. Angalau nimpe mtu mwanga ama mahali pa kuanzia kuukata mbuyu huu … kama si na wewe, basi nitamalizwa na mkuu wangu. Sina haja ya kufa na taarifa hizi.”

Jona akamwambia hana tatizo naye, atakapopata anachokihitaji, yupo radhi kumwachia. Panky akatabasamu na kutikisa kichwa chake.

“Hata kama ukiniacha hai, sitadumu. Hamna namna ya kumkimbia Sheng’. Hata uwe wapi atakutia tu mikononi na kukumaliza.”

Panky akaongezea ya kwamba pindi unapoingia ndani ya mfumo wa Sheng’, familia yako yote anakuwa anaijua. Watu wako wa karibu na marafiki zako. Ni labda ajue umekufa, na si hai akakukosa!

“Watu kadhaa walishawahi kutoroka, wengine wakitaka kuacha kazi kwa hiyari. Hakuna aliyebakiziwa uhai hata mmoja! Kwa Sheng’ kuna kuingia tu, mlango wa kutokea haupo. Na utakapoulazimisha kuujenga ukutani, basi utalipia gharama zake.”
.
.
.
****
 
*ANGA LA WASHENZI – 30*

*Simulizi za series*

ILIPOISHIA

Panky akaongezea ya kwamba pindi unapoingia ndani ya mfumo wa Sheng’, familia yako yote anakuwa anaijua. Watu wako wa karibu na marafiki zako. Ni labda ajue umekufa, na si hai akakukosa!

“Watu kadhaa walishawahi kutoroka, wengine wakitaka kuacha kazi kwa hiyari. Hakuna aliyebakiziwa uhai hata mmoja! Kwa Sheng’ kuna kuingia tu, mlango wa kutokea haupo. Na utakapoulazimisha kuujenga ukutani, basi utalipia gharama zake.”

ENDELEA

Jona hakuona haja ya kuendelea kumweka Panky mule stoo kwa ushirikiano wake alioutoa. Akamfungua kamba na kwenda naye ndani alipomkabidhia nguo kavu na nadhifu. Wakaendelea kuongea kwa muda kidogo Jona akipeleleza baadhi ya taarifa.

Panky pasipo kumficha akampatia Jona zile azijuazo. Namna gani alikuwa anatenda na kumsaidia Sheng’ kukamata Tanzania nzima, Afriika Mashariki, na hatimaye Afrika nzima. Namna gani wanavyokusanya data toka sehemu nyeti mbali mbali na kumkabidhi Sheng’ kwa ajili ya kazi zake binafsi atakazogawia vitengo vingine.

Kwa maelezo hayo, Jona akapata uelewa namna gani Panky alivyokuwa na uwezo wa kucheza na tarakilishi kwenye kila kona. Namna gani ujuzi wake ulivyokuwa mkubwa kwenye kunyambulisha taarifa, kutengeneza na kuzipoteza.

“Kama kuna taarifa ama data hatari kwa Sheng’, na taarifa hiyo ipo kwenye mashine ama tarakilishi ya mtu yeyote yule, basi ni jukumu letu kuipoteza. Tunatengeneza virusi na kuvituma kwa mtandao kama mashine ipo mbali. Virusi hao watakula mafaili yote watakayokuta humo na kiacha mashine tupu!”

Kitengo hicho hicho cha Space Button ndicho kinahusika na ukusanyaji wa taarifa popote pale ilipo kwa njia za kisasa aidha mwenye taarifa anataka ama hataki. Kama kuna mkataba ambao Sheng’ anautaka, na upo mtandaoni ama kwenye tarakilishi ya mhusika yeyote ule. Wakimtambua wataupata!

“Sheng’ ana mikataba yote ya ujenzi, madini, ardhi na kila kitu. Ana taarifa za mawaziri, na wabunge. Ana taarifa za taasisi kubwa kubwa, yote hayo yakiwezekana kwa kupitia kitengo hichi cha Space Button.”

Pia kwa kupitia mkono wa kitengo hicho, huwa wanabambikizia watu kesi kwa kuwawekea vitu ndani ya tarakilishi zao ama kwenye tovuti zao. Kutengeneza ‘application’ mbalimbali kwa ajili ya kufanyia kazi za Sheng’.

Jona akamuuliza kama kuna uwezekano wowote wa kupata data na taarifa zilizopo kwenye ‘vault’ ya Sheng’. Panky akamwambia kitu hicho hakiwezekani na hakiwezi kufanywa na mhsika yeyote yule wa Space Button kwasababu imewekwa katika usala sana.

“Kufungua Vault ya Sheng’ utahitaji alama za vidole gumba vya wahusika wote wa Space Button, na utahitaji code nne ambazo ni Sheng’ peke yake anazifahamu.”

Maelezo hayo yakamvutia sana Jona. Kichwani kwake haraka akapata wazo la kumtumia Panky katika kazi zake. Alitafakari ni kwa namna gani ujuzi wa mwanaume huyo utakavyoweza kukamilisha kazi zake kwa ufanisi zaidi.

Lakini akahofia, bado Panky hakuwa mtu wa kumwamini kiasi hicho. Bado alihitaji kumpekua na kumsoma zaidi. Na pia kama ataridhia kufanya naye kazi, maana ni jambo la hiari, si lazima.

“Unaona picha hii?” Jona alimwonyeshea Panky picha ile aliyochora kwa ajili ya Bite. Akamwambia hiyo ndiyo sababu anatafutwa na uhai wake unawindwa. Je ana ufahamu nayo?

Panky akaiteka picha hiyo kwa mikono yake na kuitazama kwa makini. Kuna jambo alikuwa analifikiria, wapi aliona picha ile. Kumbukumbu ikamjia, alishawahi iona siku moja kule ofisini kwao, mwenzake akiwa anaishughulikia.

“Sijui ina maanisha nini lakini nakumbuka siku moja niliwahi kuiona picha hii ofisini, na ndiyo ilikuwa inatengenezwa. Sikuwahi kuifuatilia wala kuiona tena.”

Jona akamuuliza kama anamfaham mtu huyo aliyekuwa anaitengeneza, Panky akasema anamfahamu mpaka na makazi yake. Jona akapanga waende kumtafuta mtu huyo ambaye alitambulishwa kwa jina la Marwa.

Lakini kabla ya kwenda huko inabidi akakutane kwanza na yule mwanaume ambaye Nade anataka kwenda kumdhibiti kwa kuhusiana na Miriam – mke wa mheshimiwa. Kazi hiyo ilikuwa ni ya kufanywa kesho yake kwenye majira ya mchana mpevu.


***


Saa tatu asubuhi…


“Huwezi amini yule mzee ameshammaliza yule jamaa!” Alisema Kinoo aliyekuwa amebebelea kikombe cheupe cha chai. Akiwa amekaa na Miranda ambaye mkononi alikuwa ameshikilia simu yake kubwa akiperuzi.

Ni ndani ya nyumba ya Miranda, Kinoo akiwa amewasili hapo muda si mwingi. Miranda alikuwa amevalia dera, nywele zake zikifungashwa na kiremba cheusi.

Kinoo alikwa hapo kumhabarisha juu ya kifo cha Mudy, mwanaume ambaye amewapatia nyaraka zile za kampuni ya umeme wa jua.

Miranda akashangazwa na taarifa hizo. Kifo cha Mudy kilikuwa ni ishara kwamba na wao, ambao wanamiliki nyaraka hizo, wanaweza wakawa ndiyo ‘tageti’ inayofuatia.

“Ni kweli,” Kinoo akamwambia. “Inabidi tuwe makini, la sivyo tutaenda na maji.”

Miranda akasonya na kubinua mdomo. Akamtazama Kinoo kwa macho ya bumbuwazi na kumwambia hawana haja ya kuishi kama digidigi sababu ya Brokoli. Kama ameanzisha vita, basi hawana budi kupambana kabla haijatoka nje ya mikono yao.

“Tuchunge ngamia huyu asije akawa mkubwa kuliko banda. Endapo tukimwacha Brokoli akaendeleza saga hili, linaweza kuwaamsha majabali yaliyolala. Akuanzae mmalize.”

Kinoo akasita kiaina. Lakini Miranda hakuona haja yay eye kufanya hivyo kwani aliamini hayo maamuzi ya yeye kumuua Mudy yametoka mikononi mwake. Na kama amemuua Mudy, sababu ya nyaraka, hatakomea hapo.

Je wapo radhi kuuawa?

“Lakini sifahamu makazi yake,” akasema Kinoo. Miranda akamuuliza:

“Umetafuta ukakosa? Mbona unakuwa kama mgeni kazini.”

Kinoo akakumbuka numbani anaishi na Sarah, pengine atakuwa anafahamu. Akaacha kuulizwa maswali ya ‘kijinga’ kama asemavyo Miranda.

“Kwahiyo kwa muda gani utakuwa umemaliza hiyo kazi?” Miranda akauliza akimtazama Kinoo na macho yake aliyoyatoa kwenye kioo cha simu.

“Nahitaji siku moja tu,” akajibu Kinoo na mjadala huo ukaisha. Miranda akamwambia Kinoo kwamba baadae jioni ana miadi ya kwenda kukutana na mke wa Boka nyumbani kwake Upanga kwa ajili ya majadiliano.

Hivyo atamtaka ampeleke huko kama atakuwa na muda. Ajabu Kinoo akakataa, akimwambia ya kwamba ana kazi ya kufanya usiku. Miranda akataka kjua kazi hiyo.

“Tangu lini ukawa na kazi usiku nisijue?”

Kinoo akatabasamu kwanza kabla hajamtaarifu Miranda ya kwamba anaishi na Sarah – aliyekuwa mfanyakazi wa Bite kwasababu za usalama. Miranda akastaajabu. Alihofia juu ya usalama wao.

“Vipi kama huyo binti akakuchota taarifa?”

Kinoo akamtoa hofu. Anajua mwanamke huyo hatakuwa na lolote kmdhuru. Miranda akamtaka awe makini na macho muda wote.

“Najua umewahi kumpa hifadhi kwasababu ni mwanamke. Huna lolote!”

Kinoo akatabasamu na kukanusha pasipo kumaanisha.


***


Saa nane mchana…


Gari aina ya Harrier rangi ya fedha inapaki kwenye uwanja wa hoteli, na baada ya punde Nade anashuka. Amevalia miwani meupe ya urembo. Koti dogo jeusi linalobana mwili wake. Suruali ya jeans na raba nyeupe.

Mkono wake wa kulia umebebelea simu ya Miriam. Na kama ukimtazama vizuri nyuma ya koti lake, utaona amefichama bunduki ndogo. Ila mpaka utazame kwa makini! Kitu ambacho ni kigmu kidogo kutokana na mwanamke huyo anavyovutia, utatazama vingine.

Akatazama kushoto na kulia. Akaridhia kila kitu kipo sawa. Akanyookea mapokezi, ambapo aliteta kidogo kabla ya kuelekezwa kwenda chumba namba fulani ambacho ndipo mtu anayemhitaji yupo.

Akabisha hodi.

Hakukuwa na majibu. Akabisha tena na tena, pasipo majibu. Akatazama simu kwa malengo ya kupiga kumtaarifu ‘mwenyeji’ kuwa ameshafika, yupo nje. Inabidi amfungulie.

Kwenye simu akakuta ujumbe. Kwasababu simu ilikuwa ‘silent’ hakujua ujumbe umeingia saa ngapi. Ilikuwa ni kama dakika kumi na tano zilizopita. Ina maana akiwa njiani kuja.

Na ujumbe huu ulikuwa umetokea kwa ‘My Heart Pale’, yaani yule mwanaume mtuhumiwa wa mahusiano na Miriam.

‘Jipangeni upya. Sipatikani kwa wepesi kiasi hicho. Mnapolala ndipo mimi naamkia.’

Shabash! Amejuaje? Nade akajiuliza. Akatazama kushoto na kulia kana kwamba labda mtu huyo anamtazama. Hakuona mtu. Akatoka eneo hilo na kwenda mapokezi kuulizia.

“Sijui, labda kweli kaondoka maana mie nimeingia zamu muda si mrefu,” alijibu mdada wa mapokezi. Nade akasonya. Itakuwa mwanaume huyo amegutuka na sauti yake, akawaza.

Lakini mwanaume huyo akampatia mawazo Nade. Atakuwa ni mtu mwerevu, ama mwenye uzoefu na mambo haya. Anajihusisha na nini?

Akatoka nje ya hoteli akiendelea kutazamatazama na kuwaza kichwani. Akafungua gari na kuzama ndani. Lakini kabla hajawasha chombo, akahisi kitu cha baridi shingoni, na amri:

“Tulia hivyo hivyo!"


Ni nani huyo?
 
Back
Top Bottom