*ANGA LA WASHENZI -- 32*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA...
"Kesho ama keshokutwa tunaweza tukawa na utambulisho mbele ya vyombo vya habari. Utakuwa na muda na utayari?" Akauliza Mama Boka.
Kabla Miranda hajajibu, akasita kwanza. Alihofia endapo akijianika kwenye mtandao na kwenye televisheni inaweza ikamletea tatizo. Maadui zake watajua na itakuwa kana kwamba amewachokoza.
Hapa palihitaji hekima. Na hekima kwasababu ya asili ya kazi zake.
ENDELEA
Akamwambia mama Boka ampatie muda kidogo. Ila kumbuka interview ilitakiwa kuwa kesho ama keshokutwa. Basi ikalazimika isogezwe mbele kukidhi haja ya Miranda.
"Kwahiyo itakuwa lini?" Akauliza mama Boka. Miranda napo akakosa jibu la kusema. Bado akarejea kule kule. Nitakwambia.
Mama Boka akampatia mwanya ila akamtaka awahishe maana hamna muda zaidi. Miranda akaafiki kichwani akipanga kwenda kumwambia BC hilo jambo aone atasemaje.
Basi wakahitimisha hilo jambo na kwendelea kuongea zaidi na zaidi. Usiku ulikuwa unakua, na kwa Miranda hakuwa na presha kwani nje usafiri ulikuwa unangoja.
Kwenye majira ya saa tano, waziri akarejea nyumbani. Akastaajabu kumkuta Miranda hapo mpaka muda huo, akamsalimu na kumkonyeza.
Akatamani sana aupate muda binafsi na mwanamke huyo ila haikuwezekana maana mkewe alikuwa hapo kila sekunde akitazama kila jambo. Ikabidi Waziri awe anamtumia ujumbe binti huyo wakati wakiendelea kuongea.
Chating zao:
"Umependeza love."
"Kweli? Asante..."
"Karibu. Mpaka nikasisimka."
"Lol acha uongo bana.."
"Kweli nakuambia, sasa vipi lile jibu langu mrembo?"
"Mmmm umeanza nawee..."
"Niambie bas na mie nile vitamu. Mwenzako nangoja na hutaki kunijibu."
"Ntakujib usjali."
"Lini sasa?"
Kimya kidogo.
"Kesho tunaweza tukakutana?" Ujumbe wa Boka ukauliza. Ila mara hii Miranda hakutaka kujibu, akajifanya amaeupotezea. Akaaga aende.
Boka na mkewe wakamsindikiza akajipaki garini na kwenda. Akiwa anatembea barabarani akawa anasoma jumbe za Boka ambazo bado hazikukoma kuingia.
Akatabasamu na kuzipuuza. Si kwamba hakuwa anaziona, la hasha, bali alikuwa anatengeneza mazingira ya kuonekana si mtu wa 'bei chee'.
Mpaka anafika kulikuwa kuna jumbe kama nane za Boka. Ujumbe wa mwisho ukiwa ni wa kuingiziwa pesa, Boka akiwa ametuma shilingi elfu hamsini!
"Nakutumia nauli ya kesho basi tukutane mida ile ile kule kule sawa?"
Ulisema ujumbe wa pili tokea mwishoni.
Miranda akajikuta akitabasamu. Napo hakujibu ujumbe huo.
***
Saa saba kasoro, usiku...
Sauti ya vibofyeo vya tarakilishi inagonga gonga na kuacha. Kutokana na ukimya uliokuwepo ndani ya chumba na majira haya ya usiku, sauti hiyo inasikika vema.
Mbele ya tarakilishi alikuwapo Jona na Panky.
Panky alikuwa mbele akikodolea kioo cha tarakilishi kana kwamba anatafuta jambo. Jona yeye alikuwa amesimama kwa nyuma mkononi akiwa amebebelea kikombe cheupe cha chai.
Hii kazi wameanza tangu muda. Jona alikuwa amechoka, akipiga piga mihayo, ila Panky yeye alikuwa fiti. Uzoefu wake kukaa kwenye viti muda mrefu, mbele ya tarakilishi, ulikuwa unamsaidia.
Mara Panky akatabasamu na kusema:
"Tayari! Kila kitu kipo sawa sasa!"
Akamweleza Jona kwamba kuanzia muda ule wanaweza wakai - trace ile simu ya Miriam na kujua wapi ilipo. Kama haitoshi hata mawimbi ya sauti yatakuwa bora zaidi.
Na punde ataweza hata kuiwajibisha kuchukua picha ama video!
Jona akafurahi sana na kumpongeza. Na kuhakikisha hilo akaanza kusoma ramani ya wapi Nade alipo. Akapaona! Akaweka earphone masikioni, mawimbi yalikuwa yametulia kiasi kwamba akawa anasikia kitu kilichokuwa kinafanyika kwa mbali!
"Itakuwa wana party," alisema Jona.
"Yah! Kwa nje ya nyumba huko," Panky akajazia taarifa. Mbali na muziki huo uliokuwa unasikika kwa mbali hakukuwa na sauti nyingine mbadala.
Mazingira yalikuwa yametulia mno.
"Usijali, hauna haja ya kusikiliza muda wote. Pindi kutakapokuwa na sauti yoyote karibu, itataarifu simu yako kwa njia ya vibration, kwahiyo utasikiliza."
Utaalamu huo ukamsisimua sana Jona. Alivutiwa nao na akataka kujua historia ya Panky. Ametokea wapi na ilikuaje akajiunga na Sheng'.
Panky akamjibu kifupi, tamaa ya pesa. Alikuwa ametoka mafunzoni na hakuwa na fedha ya kulelea familia yake maskini. Sheng' akamuahidi mshahara mnono, lakini pia masomo zaidi.
"Ila hapo mwanzoni sikujua kama Sheng' anajihusisha na biashara haramu. Hata serikali haifahamu. Ni mtu mkubwa na mfanyabiashara wa mambo mengi, mambo ambayo anayatumia kama mwamvuli kukingia biashara zake zimwingiazo pesa zaidi ...
Hata pale nilipokuja kugundua, nilikuwa tayari nimeshachelewa. Sikuweza kutoka tena."
Jona akamuuliza kama angelipendelea kupata fursa ya kutoka, Panky akatabasamu na kujibu, haijalishi namna gani anataka kutoka huko, hilo jambo haliwezekani.
Kwa sasa anamfanyia kazi Sheng' kwasababu ya uhai wake na wa familia yake tu. Isingelikuwa hivyo angeshalifanya mambo mengine ya maana.
"Hakuna jambo lisilo na kikomo," Jona akamwambia. "Na pengine haukujaribu vya kutosha kuupata mlango. Mimi naamini inawezekana wewe kutoka."
Panky akataka kujua ni kwa namna gani hilo linawezekana. Akatega masikio na macho. Jona akamwambia wao ndiyo watu wa kufanikisha hilo na si wengine.
Lakini Panky alikuwa anahofia. Alichokuwa anahofia si yeye, bali mke na mwanaye Nasra.
"Ndiyo kwanza anatimiza miaka minne. Nisingependa afe kwasababu yangu."
Jona akamhakikishia hakuna atakayekufa. Lakini inatakiwa wawe werevu mno kufanikisha hilo. Jambo kubwa ni kwamba inawezekana kama wakitia nia.
"Mimi nina mpango," Jona akasema. "Ili kumdhibiti na kummaliza Sheng' inabidi mtu fulani awepo ndani ya system yake. Mtu huyu ajue yanayoendelea huko. Kila kinachofanyika. Alafu awepo na mtu wa nje, ambaye atakuwa anachanga karata kutengua mipango."
"Ni hatari," akasema Panky. Alihofia sana lakini Jona akamwambia hiyo ndiyo njia pekee la sivyo atakuwa mtumwa milele, na misha yake na ya familia yake yakiwa rehani.
"Umetumwa kunimaliza. Wakijua mimi sijafa, watakumaliza wewe. Inabidi uende kwa Sheng' na umwambie umenimaliza. Nami nitapotea kwa muda fulani. Wakati huo wewe ukiendelea kufanya kazi."
Jona alimwambia Panky kwamba hiyo ndiyo njia pekee ya yeye kuishi na kuwa salama tangu hajamaliza kazi aliyoagizwa. Lakini pia ndiyo fursa ya wao kufanya jambo kwa urahisi kwasababu mosi, Panky atakuwa amerudi ndani ya system, pili, Sheng' hatahangaika na Jona kwa kujua amemmaliza.
"Ngoja tuone," Akasema Panky.
"Kumbuka muda unaenda, inatakiwa urejeshe ripoti kwa Sheng'," Jona akakumbusha.
Panky akashusha pumzi ndefu.
***
Saa kumi na moja asubuhi ...
Kinoo anarejelea ujumbe alioundika na kuutunza kwenye simu jana yake wakati anaongea na Sarah.
'Nyumba moja kubwa nyeupe yenye geti jekundu. Ukuta wake una sinyenge kwa juu zilizosokotwa sokotwa.'
Aliposoma ujumbe huo akatazama nyumba iliyo mbele yake. Akaona vigezo vilivyomo ndani ya ujumbe vinafanana.
Mwanaume huyu alikuwa juu ya pikipiki yake kubwa. Kichwani amevalia kofia ngumu, mwilini kibodi cheusi na suruali ya jeans na raba - All star.
Jana yake usiku, pasipo Sarah kutambua, Kinoo akamchunguza juu ya makazi ya Brokoli. Mwanamke huyo akabwabwaja na kumjaza Kinoo taarifa. Kinoo akarekodi kwenye ujumbe kana kwamba alikuwa anachat na mtu.
Sasa alikuwa mbele ya nyumba ambayo alihisi wazi ni ya Brokoli kwa mujibu wa maelezo. Akazima pikipiki na kuijongea.
Kwanini wanapenda majira haya ya asubuhi?
Majira haya yana uhakika zaidi kumkuta mtu nyumbani. Muda wa kurudi usiku huwa hautabiriki, na muda wa mchana ni ngekewa!
Lakini asubuhi ya mapema, kwa wafanya kazi huwa ndiyo wanaamka kwenda makazini, wengi wao. Na bado hakujawa zogo.
Mara kaap! Kinoo akatua ndani ya uzio wa nyumba ya Brokoli. Alikuwa hapo kutekeleza jambo moja tu, mauaji! Akuanzaye mmalize.
Kabla hajafanya kingine chochote akasoma kwanza mazingira. Akagundua kuna mbwa wawili wakubwa karibia na chumba cha mlinzi!
Mbwa hao wakampatia ishara ya kwamba pale hapakuwa pa kukaa muda mrefu kwani harufu yake yaweza kusababisha zogo
Basi mfukoni akatoa mfuko mmoja soseji. Akauchanja na meno na kuuweka chini, alafu haraka akaizunguka nyumba.
Punde mbwa wakasikia harufu hiyo. Ikawapuuzisha wasisikie ya Kinoo. Wakafakamia soseji zile. Mlinzi akagutuka na kusonga karibu na mbwa apate kuona nini hicho wanatafuna.
Akaona soseji!
Kutazama vema akaona alama za viatu juu ya sakafu! Akajua wameshavamiwa. Ila haikusaidia kitu, kwani kabla hajafanya lolote, akajikuta amedakwa shingo na kuvunjwa!
Chini akadondoka akifuatiwa na mbwa wake. Kinoo sasa akaachiwa mwanya wa kufanya mambo yake taratibu pasipo papara. Akatega kumwona Brokoli akitoka nje.
Dakika kama kumi mwanaume huyo akatoka nje akiwa amevalia taulo na mswaki upo mdomoni. Kuna kitu alikuwa anaenda kuchukua kwenye gari lake, VX la grey.
Lakini wasaa huo ukawa wa mwisho kwake! Akajikuta amekabwa na mkono mzito. Pua na mdomo vikabanwa na kitambaa kizito chenye malighafi kama taulo.
Kuvuta kwake hewa kukawa kosa. Alivuta mara moja tu na mara mapigo yake ya moyo yakasimama! Habari yake ikaishia hapo hapo!
Kinoo akayoyoma zake akifunga mahesabu...
***