Anga la washenzi na Joana anaona kitu usiku

Anga la washenzi na Joana anaona kitu usiku

*ANGA LA WASHENZI -- 31*

*Simulizi za series*

ILIPOISHIA

Lakini mwanaume huyo akampatia mawazo Nade. Atakuwa ni mtu mwerevu, ama mwenye uzoefu na mambo haya. Anajihusisha na nini?

Akatoka nje ya hoteli akiendelea kutazamatazama na kuwaza kichwani. Akafungua gari na kuzama ndani. Lakini kabla hajawasha chombo, akahisi kitu cha baridi shingoni, na amri:

“Tulia hivyo hivyo!"

ENDELEA

Sauti hiyo ya kiume ilikuwa ngeni kwa Nade. Hakujua ni nani huyo, akapapaswa na woga. Alikuwa amezidiwa ujanja, akawa mpole kama maji mtungini.

"Haya washa gari na twende ntakapokuelekeza," sauti ikaamuru. Nade akawasha gari na kutoka eneo la hotelini akipewa maelekezo na mwanaume aliyekuwa amemteka.

Sura ya mwanaume huyu ilikuwa mpya! Alikuwa ni mbaba mweusi mwenye nywele fupi zilizochanjwa 'ways' nne. Macho yake yalikuwa mekundu na madogo.

Mikono yake ilikuwa imepitiwa pitiwa na michirizi ya mishipa lukuki. Alikuwa amevalia shati 'beach boy' na suruali ya jeans iliyokoza.

Mwanaume huyu anajulikana kwa jina la Nyokaa! 'Chalii' wa Arusha maarufu kwa pesa za madini. Kazi ambayo aliianza tokea akiwa mtoto mdogo, 'nyokaa' lakini mpaka leo hii amekuwa mtu mzima, jibaba, bado anajulikana kwa jina hilo hilo maarufu.

Alimwongoza Nade mpaka nje ya jiji akiwa amenyamaza asiseme lolote. Akamwamuru asimamishe gari na kuanza kumuuliza maswali.

Akataka kujua Miriam yupo wapi na yupo na nani. Yeye ni nani na ametumwa kuja kufanya nini? Nade akalaghai Miriam yupo polisi, na yeye ni polisi pia.

Nyokaa akajua janja hiyo. Akamtishia Nade kuwa atamnyofoa uhai wake kama akiendelea na michezo yake ya kitoto!

"Sina muda wa kupoteza we malaya! Sawa? Najua Miriam atakuwa kwa Eliakimu. Na wewe utakuwa kibaraka wake. Usinifanye mimi mtoto mdogo, najua kila kinachoendelea!"

"Sasa kwanini unaniuliza kama unajua kila kitu?" Nade akauliza. Nyokaa akamzaba kofi zito lililomchana Nade lips. Akavuja damu.

"Unifahamu vizuri, mwanamke! Ngoja utanijua vema muda si mwingi na utanipa kila ninachokitaka."

Baada ya Nyokaa kusema hivyo akamziraisha Nade kwa kumpiga na kitako cha bunduki kisogoni. Kisha akampigia simu mtu aliyemtunza kwa jina la Ninjaa.

Akamwelekeza mahali alipo na kumtaka afike hapo muda si mrefu kuna kazi wanatakiwa kuifanya. Lakini pia akamtaka ajiweke sawa kwa kuwapasha habari wengineo ya kwamba vita inaweza kuzuka muda wowote.

Basi haikuchukua muda mrefu, gari moja kubwa Hammer nyekundu ikasogea eneo la tukio. Wakashuka njemba tatu, mmoja wao akiwa ndiyo yule Ninjaa.

Watu hawa walikuwa wanafanana kwa rangi, weusi, na wenye sura angama za kazi. Miili yao ilikuwa mirefu na iliyojaa.

Wakateta na Nyokaa kwa muda kidogo, wakamchukua Nade na kumtia kwenye Hammer kisha wakalipua gari ya Nade na kuhepa!

Kitu ambacho hawakuwa wanajua ni kwamba kuna mtu upande mwingine aliyekuwa anasikiliza kila jambo. Mtu huyu aliona wakati Nade akitekwa na hakufanya jambo lolote.

Mtu huyu aliachwa kule hotelini, ila bado alikuwa anawafuatilia kwa ukaribu akitumia kifaa cha simu cha Miriam ambacho Nade alikuwa nacho mfukoni.

Mtu huyu ndiye pekee aliyekuwa anajua kama Nade ametekwa na wapi anapelekwa. Hakuwa mwingine bali Jona!

Mambo yalikuwa yanazidi kupamba moto, na hakutaka kujishughulisha kuuzima moto huu upesi mpaka aone haswa kina cha maji haya ambayo hayatakiwi kupimwa kwa mguu!

Baada ya muda mfupi Nade kuziraishwa, Jona akatimka toka mazingirani mwa hoteli kichwani mwake akiwaza mambo kadhaa ambayo hakika hakuwa na majibu nayo.

Akawaza kama kuna namna zaidi ambayo anaweza akatumia kupata zaidi mambo toka kwenye ile application ambayo ameipakua na kuitunza kwenye simu ya Nade.

Hapo akapata wazo la kumshirikisha Panky. Huenda mwanaume huyo akawa na mawazo zaidi. Ila kwanza akapitia kazini kwake kuhakikisha kila jambo lipo sawa kabla ya kunyookea nyumbani.

Huko ambapo alikuwa amemfungia Panky.


***


"Sasa?" Nigaa akauliza baada ya kuchomoa sigara yake mdomoni. Macho yake yalikuwa yanamtazama Lee ambaye alikuwa ameshika tama. Walikuwa ndani ya makazi yao, Nigaa amekunja nne, pakti mbili za sigara zikiwa zimekaa pembeni.

Lee alikuwa anatazama televisheni ila macho yake yakizama fikirani.

"Inabidi leo twende. For once and for all, nijue moja!" Akasema Lee.

"Kazi ndogo sana hiyo Lee. Siyo ya kuumiza kichwa kabisa. Si unajua huyo manzi anapoishi?"

"Ndio."

"Na huyo famba?"

"Ndio."

"Sasa kuna nini hapo? Tukiwapata tunawanyonya macho! Hawaweza wakatuletea pigo za kifala fala!" Akasema Nigaa alafu akapiga pafu nne za sigara na kuchafua chumba kwa moshi.

"Kwanini tusiende sasa hivi? Naona kama tunakawia," Nigaa alisema akitabasamu. Lee akatikisa kichwa na kumwambia wavute vute kidogo. Wakiwahi sana wataenda kukawia huko.

Ulikuwa ni muda wa majira ya saa tatu na nusu hivi, Lee alitaka wavute mpaka majira ya saa nne nne, angalau viwanja vinakuwa vimefunguliwa ama kujaa jaa watu.

Lee alimtaka Nigaa wanywe na kuvuta kwani hakutarajia kama angalikuwepo hai kwa muda huo. Hakutegemea kama angelitoka salama toka chumba cha mkuu.

"Sikuamini alipopiga risasi zile pembeni. Niliposikia mlio wa silaha nikajua nimeshakwesha. Niliposikia kauli ya kupewa nafasi ya mwisho ndipo nikajua bado nipo duniani, na ninahema."

"Una bahati sana, Lee," akasema Nigaa. "Mkuu anajua fika akikumaliza basi naye hatapata karatasi hiyo. Wewe ndiyo njia pekee na kuu ya kupata hiyo karatasi."

"Sidhani," Lee akasema akitikisa kichwa. "Ni mara ngapi anamaliza watu wakiwa kwenye misheni kubwa na nzito kisha anawaweka wengine? Nadhani siku yangu haikuwa imewadia."

"Unajua ni mara chache sana Mkuu anampatia mtu nafasi ya pili?" Akasema Nigaa. Lee akakubaliana na kauli hiyo. Kwake ilikuwa kama ngekewa!

Basi muda ule ambao walikuwa wanaungojea, ukawadia. Muda wa kwenda kufanya tukio. Wakajikusanya na kwenda kwenye gari mpaka kwa yule mwanamke, Glady. Ila hawakumkuta!

Walikuta mashoga zake wawili ambao walisema Glady ametoka muda si mrefu. Kwahiyo ikabidi Lee aongoze mpaka kule klabu alipomkuta mwanamke huyo.

Huko napo hawakumkuta. Lee asife moyo akanyooshea usukani kuelekea viwanja vile ambavyo Glady alimpeleka kumtazama yule mwanaume wakianzia na Maisha.

Bahati huko wakamwona mlengwa wao. Alikuwa na mwanaume fulani hivi mrefu katika mazingira ya kimahaba wakiketi kochini. Lee akasonga na kumnyaka bega mwanamke huyo, akamtaka atimize kazi yake.

Alah! Kumbe yule mwanaume aliyekuwepo naye ndiye yule yule wanayemtafuta. Lee akajikuta anatabasamu na kuangua kicheko kabla hajamwambia Nigaa kwamba siku hiyo imekuwa nzuri maana wamewakuta walengwa wao wote kwa mkupuo.

Mwanaume yule kutaka kuonyesha umwamba, akanyanyua chupa ambamizd nayo Lee kichwani. Haki hakuamini kilichotokea! Mkono wake ulidakwa upesi na mguu wa Lee, alafu ukakunjwa na kuvunjwa. Chupa ikadondokea chini!

Mwanaume yule akapiga sana kelele za maumivu. Na kumbe wenzake hawakuwa mbali. Haraka wakasogea karibu. Wanaume wawili warefu, wakijiandaa kwa kubebelea chupa mikononi.

Kwa namba ambavyo wanaume hawa walivyokuwa wanaogopeka, hata mabaunsa hawakuthubutu kuwazuia zaidi ya kuwaomba waachane na huyo mchina na mwenzake kabla hawajaaribu mambo.

Ila hawakusikia. Walitaka kuonyesha ubavu wao. Hawakutaka kudharaulika! Kila mmoja akajigawa kumfuata wake, mmoja akienda kwa Lee na mwingine Nigaa.

Watu wakapisha uwanja hapo klabu na kubakia wakitazama pambano. Ikiwemo hata na mabaunsa wenyewe wanaohusika na ulinzi.

Bwana we! Wale wanaume wakaonjeshwa joto ya jiwe! Hawakufurukuta wala kufanya kitu, teke na ngumi zao zilikuwa kama mvua za vuli zikapita! Chupa walizokuja nazo zikawakata wenyewe na kuwaacha wakivujilia damu lukuki!

Lee akamfuata yule mwanaume kochini na kumuuliza juu ya karatasi yake. Mwanaume yule akiwa bado ameshikilia mkono wake uliokunja nne, akasema ipo nyumbani!

Lee na Nigaa wakambeba na kwenda naye nyumbani. Wakapata nyaraka yao.

"Kuna yeyote uliyempatia hii karatasi?" Lee akauliza.

Mwanaume akatikisa kichwa upesi.

"Hapana hapana ... hakuna!"

Lee na Nigaa wakaondoka zao. Lee asipoteze muda akanyookea kwa mkuu na kumkabidhi karatasi ile. Mkuu akaikagua na kuridhika. Ila naye akaguswa na swala la usiri wa nyaraka ile.

Akaulizia. Lee akamwambia bado ni ya siri. Ila bado mkuu akataka akahakikishe jambo hilo kwa ufasaha zaidi. Lee akakubali na kisha akaenda.


***


"Umependeza sana," alisema Mke wa Boka akimtazama Miranda kwa matamanio.

"Ahsante sana!" Miranda akapokea sifa kwa tabasamu pana huku akijitazama tazama.

Akakaribishwa kwenye sebule kubwa kama ukumbi. Hapo kulikuwa kuna viti virefu vikiambaa ambaa na sebule. Viti hivi vilikuwa vina rangi ya kupendeza viking'arisha sebule.

Sebule ilikuwa inametameta kwa samani za bei ya juu! Palikuwa panavutia kuvunja shingo ya mgeni kuangaza angaza.

Miranda asidhulumu macho yake akatazama na kupekua.

Kinywaji kikaja na hata chakula cha usiku. Wakiwa wanakula wakaendelea na kuteta mambo yao kuhusu urembo na ulimwende. Wakajadili kwa muda wa kama lisaa limoja.

Wakakubaliana Miranda kuwa balozi wa kampuni ya urembo ya mama huyo. Atakuwa ndiye msemaji mkuu na atahusika na kuwakilisha kampuni hiyo maeneo mbalimbali.

"Kesho ama keshokutwa tunaweza tukawa na utambulisho mbele ya vyombo vya habari. Utakuwa na muda na utayari?" Akauliza Mama Boka.

Kabla Miranda hajajibu, akasita kwanza. Alihofia endapo akijianika kwenye mtandao na kwenye televisheni inaweza ikamletea tatizo. Maadui zake watajua na itakuwa kana kwamba amewachokoza.

Hapa palihitaji hekima. Na hekima kwasababu ya asili ya kazi zake.


***
 
*ANGA LA WASHENZI -- 32*

*Simulizi za series*


ILIPOISHIA...

"Kesho ama keshokutwa tunaweza tukawa na utambulisho mbele ya vyombo vya habari. Utakuwa na muda na utayari?" Akauliza Mama Boka.

Kabla Miranda hajajibu, akasita kwanza. Alihofia endapo akijianika kwenye mtandao na kwenye televisheni inaweza ikamletea tatizo. Maadui zake watajua na itakuwa kana kwamba amewachokoza.

Hapa palihitaji hekima. Na hekima kwasababu ya asili ya kazi zake.

ENDELEA

Akamwambia mama Boka ampatie muda kidogo. Ila kumbuka interview ilitakiwa kuwa kesho ama keshokutwa. Basi ikalazimika isogezwe mbele kukidhi haja ya Miranda.

"Kwahiyo itakuwa lini?" Akauliza mama Boka. Miranda napo akakosa jibu la kusema. Bado akarejea kule kule. Nitakwambia.

Mama Boka akampatia mwanya ila akamtaka awahishe maana hamna muda zaidi. Miranda akaafiki kichwani akipanga kwenda kumwambia BC hilo jambo aone atasemaje.

Basi wakahitimisha hilo jambo na kwendelea kuongea zaidi na zaidi. Usiku ulikuwa unakua, na kwa Miranda hakuwa na presha kwani nje usafiri ulikuwa unangoja.

Kwenye majira ya saa tano, waziri akarejea nyumbani. Akastaajabu kumkuta Miranda hapo mpaka muda huo, akamsalimu na kumkonyeza.

Akatamani sana aupate muda binafsi na mwanamke huyo ila haikuwezekana maana mkewe alikuwa hapo kila sekunde akitazama kila jambo. Ikabidi Waziri awe anamtumia ujumbe binti huyo wakati wakiendelea kuongea.

Chating zao:

"Umependeza love."

"Kweli? Asante..."

"Karibu. Mpaka nikasisimka."

"Lol acha uongo bana.."

"Kweli nakuambia, sasa vipi lile jibu langu mrembo?"

"Mmmm umeanza nawee..."

"Niambie bas na mie nile vitamu. Mwenzako nangoja na hutaki kunijibu."

"Ntakujib usjali."

"Lini sasa?"

Kimya kidogo.

"Kesho tunaweza tukakutana?" Ujumbe wa Boka ukauliza. Ila mara hii Miranda hakutaka kujibu, akajifanya amaeupotezea. Akaaga aende.

Boka na mkewe wakamsindikiza akajipaki garini na kwenda. Akiwa anatembea barabarani akawa anasoma jumbe za Boka ambazo bado hazikukoma kuingia.

Akatabasamu na kuzipuuza. Si kwamba hakuwa anaziona, la hasha, bali alikuwa anatengeneza mazingira ya kuonekana si mtu wa 'bei chee'.

Mpaka anafika kulikuwa kuna jumbe kama nane za Boka. Ujumbe wa mwisho ukiwa ni wa kuingiziwa pesa, Boka akiwa ametuma shilingi elfu hamsini!

"Nakutumia nauli ya kesho basi tukutane mida ile ile kule kule sawa?"

Ulisema ujumbe wa pili tokea mwishoni.

Miranda akajikuta akitabasamu. Napo hakujibu ujumbe huo.


***

Saa saba kasoro, usiku...


Sauti ya vibofyeo vya tarakilishi inagonga gonga na kuacha. Kutokana na ukimya uliokuwepo ndani ya chumba na majira haya ya usiku, sauti hiyo inasikika vema.

Mbele ya tarakilishi alikuwapo Jona na Panky.

Panky alikuwa mbele akikodolea kioo cha tarakilishi kana kwamba anatafuta jambo. Jona yeye alikuwa amesimama kwa nyuma mkononi akiwa amebebelea kikombe cheupe cha chai.

Hii kazi wameanza tangu muda. Jona alikuwa amechoka, akipiga piga mihayo, ila Panky yeye alikuwa fiti. Uzoefu wake kukaa kwenye viti muda mrefu, mbele ya tarakilishi, ulikuwa unamsaidia.

Mara Panky akatabasamu na kusema:

"Tayari! Kila kitu kipo sawa sasa!"

Akamweleza Jona kwamba kuanzia muda ule wanaweza wakai - trace ile simu ya Miriam na kujua wapi ilipo. Kama haitoshi hata mawimbi ya sauti yatakuwa bora zaidi.

Na punde ataweza hata kuiwajibisha kuchukua picha ama video!

Jona akafurahi sana na kumpongeza. Na kuhakikisha hilo akaanza kusoma ramani ya wapi Nade alipo. Akapaona! Akaweka earphone masikioni, mawimbi yalikuwa yametulia kiasi kwamba akawa anasikia kitu kilichokuwa kinafanyika kwa mbali!

"Itakuwa wana party," alisema Jona.

"Yah! Kwa nje ya nyumba huko," Panky akajazia taarifa. Mbali na muziki huo uliokuwa unasikika kwa mbali hakukuwa na sauti nyingine mbadala.

Mazingira yalikuwa yametulia mno.

"Usijali, hauna haja ya kusikiliza muda wote. Pindi kutakapokuwa na sauti yoyote karibu, itataarifu simu yako kwa njia ya vibration, kwahiyo utasikiliza."

Utaalamu huo ukamsisimua sana Jona. Alivutiwa nao na akataka kujua historia ya Panky. Ametokea wapi na ilikuaje akajiunga na Sheng'.

Panky akamjibu kifupi, tamaa ya pesa. Alikuwa ametoka mafunzoni na hakuwa na fedha ya kulelea familia yake maskini. Sheng' akamuahidi mshahara mnono, lakini pia masomo zaidi.

"Ila hapo mwanzoni sikujua kama Sheng' anajihusisha na biashara haramu. Hata serikali haifahamu. Ni mtu mkubwa na mfanyabiashara wa mambo mengi, mambo ambayo anayatumia kama mwamvuli kukingia biashara zake zimwingiazo pesa zaidi ...

Hata pale nilipokuja kugundua, nilikuwa tayari nimeshachelewa. Sikuweza kutoka tena."

Jona akamuuliza kama angelipendelea kupata fursa ya kutoka, Panky akatabasamu na kujibu, haijalishi namna gani anataka kutoka huko, hilo jambo haliwezekani.

Kwa sasa anamfanyia kazi Sheng' kwasababu ya uhai wake na wa familia yake tu. Isingelikuwa hivyo angeshalifanya mambo mengine ya maana.

"Hakuna jambo lisilo na kikomo," Jona akamwambia. "Na pengine haukujaribu vya kutosha kuupata mlango. Mimi naamini inawezekana wewe kutoka."

Panky akataka kujua ni kwa namna gani hilo linawezekana. Akatega masikio na macho. Jona akamwambia wao ndiyo watu wa kufanikisha hilo na si wengine.

Lakini Panky alikuwa anahofia. Alichokuwa anahofia si yeye, bali mke na mwanaye Nasra.

"Ndiyo kwanza anatimiza miaka minne. Nisingependa afe kwasababu yangu."

Jona akamhakikishia hakuna atakayekufa. Lakini inatakiwa wawe werevu mno kufanikisha hilo. Jambo kubwa ni kwamba inawezekana kama wakitia nia.

"Mimi nina mpango," Jona akasema. "Ili kumdhibiti na kummaliza Sheng' inabidi mtu fulani awepo ndani ya system yake. Mtu huyu ajue yanayoendelea huko. Kila kinachofanyika. Alafu awepo na mtu wa nje, ambaye atakuwa anachanga karata kutengua mipango."

"Ni hatari," akasema Panky. Alihofia sana lakini Jona akamwambia hiyo ndiyo njia pekee la sivyo atakuwa mtumwa milele, na misha yake na ya familia yake yakiwa rehani.

"Umetumwa kunimaliza. Wakijua mimi sijafa, watakumaliza wewe. Inabidi uende kwa Sheng' na umwambie umenimaliza. Nami nitapotea kwa muda fulani. Wakati huo wewe ukiendelea kufanya kazi."

Jona alimwambia Panky kwamba hiyo ndiyo njia pekee ya yeye kuishi na kuwa salama tangu hajamaliza kazi aliyoagizwa. Lakini pia ndiyo fursa ya wao kufanya jambo kwa urahisi kwasababu mosi, Panky atakuwa amerudi ndani ya system, pili, Sheng' hatahangaika na Jona kwa kujua amemmaliza.

"Ngoja tuone," Akasema Panky.

"Kumbuka muda unaenda, inatakiwa urejeshe ripoti kwa Sheng'," Jona akakumbusha.

Panky akashusha pumzi ndefu.

***

Saa kumi na moja asubuhi ...

Kinoo anarejelea ujumbe alioundika na kuutunza kwenye simu jana yake wakati anaongea na Sarah.

'Nyumba moja kubwa nyeupe yenye geti jekundu. Ukuta wake una sinyenge kwa juu zilizosokotwa sokotwa.'

Aliposoma ujumbe huo akatazama nyumba iliyo mbele yake. Akaona vigezo vilivyomo ndani ya ujumbe vinafanana.

Mwanaume huyu alikuwa juu ya pikipiki yake kubwa. Kichwani amevalia kofia ngumu, mwilini kibodi cheusi na suruali ya jeans na raba - All star.

Jana yake usiku, pasipo Sarah kutambua, Kinoo akamchunguza juu ya makazi ya Brokoli. Mwanamke huyo akabwabwaja na kumjaza Kinoo taarifa. Kinoo akarekodi kwenye ujumbe kana kwamba alikuwa anachat na mtu.

Sasa alikuwa mbele ya nyumba ambayo alihisi wazi ni ya Brokoli kwa mujibu wa maelezo. Akazima pikipiki na kuijongea.

Kwanini wanapenda majira haya ya asubuhi?

Majira haya yana uhakika zaidi kumkuta mtu nyumbani. Muda wa kurudi usiku huwa hautabiriki, na muda wa mchana ni ngekewa!

Lakini asubuhi ya mapema, kwa wafanya kazi huwa ndiyo wanaamka kwenda makazini, wengi wao. Na bado hakujawa zogo.

Mara kaap! Kinoo akatua ndani ya uzio wa nyumba ya Brokoli. Alikuwa hapo kutekeleza jambo moja tu, mauaji! Akuanzaye mmalize.

Kabla hajafanya kingine chochote akasoma kwanza mazingira. Akagundua kuna mbwa wawili wakubwa karibia na chumba cha mlinzi!

Mbwa hao wakampatia ishara ya kwamba pale hapakuwa pa kukaa muda mrefu kwani harufu yake yaweza kusababisha zogo

Basi mfukoni akatoa mfuko mmoja soseji. Akauchanja na meno na kuuweka chini, alafu haraka akaizunguka nyumba.

Punde mbwa wakasikia harufu hiyo. Ikawapuuzisha wasisikie ya Kinoo. Wakafakamia soseji zile. Mlinzi akagutuka na kusonga karibu na mbwa apate kuona nini hicho wanatafuna.

Akaona soseji!

Kutazama vema akaona alama za viatu juu ya sakafu! Akajua wameshavamiwa. Ila haikusaidia kitu, kwani kabla hajafanya lolote, akajikuta amedakwa shingo na kuvunjwa!

Chini akadondoka akifuatiwa na mbwa wake. Kinoo sasa akaachiwa mwanya wa kufanya mambo yake taratibu pasipo papara. Akatega kumwona Brokoli akitoka nje.

Dakika kama kumi mwanaume huyo akatoka nje akiwa amevalia taulo na mswaki upo mdomoni. Kuna kitu alikuwa anaenda kuchukua kwenye gari lake, VX la grey.

Lakini wasaa huo ukawa wa mwisho kwake! Akajikuta amekabwa na mkono mzito. Pua na mdomo vikabanwa na kitambaa kizito chenye malighafi kama taulo.

Kuvuta kwake hewa kukawa kosa. Alivuta mara moja tu na mara mapigo yake ya moyo yakasimama! Habari yake ikaishia hapo hapo!

Kinoo akayoyoma zake akifunga mahesabu...


***
 
textgram_1511183830.png



Anga la wenyewe. Anga la mabaazazi. Anga la mashababi. Anga la wababe.


ANGA LA WASHENZI!



Leo saa tatu usiku. Unaanzaje kukosa?
 
Back
Top Bottom