*ANGA LA WASHENZI --- 40*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Kulikuwa kuna milango miwili maeneo hayo, milango yote hii ikiwa ni ya kioo. Ukutani kulikuwa kumechorwa picha kadhaa za wanawake, maua na silaha.
Muziki ukiwa unaendelea kukonga nyoyo za watu, kama si vichwa, mlango mmoja ukafunguliwa na mwanaume fulani aliyekuwa amejaza mwili. Mwanaume huyu alitembea kwa kasi kuelekea meza fulani ukutani. Hapo akamnong’oneza mwenziwe sikioni.
Ghafla huyo aliyenong’onezwa akanyanyuka. Akaangaza kule kaunta akatoa ishara ya mkono, mara muziki ukakata! Akapaza sauti kusema wamevamiwa!
ENDELEA
Haraka wanaume wote wakatoka nje, na hapo ndiyo ikaonekana kumbe mwanaume yule aliyepewa taarifa alikuwa ni Nyokaa, na hayo yalikuwa ni makazi yake. Haraka walielekea kwenye chumba walichokuwa wamemfungia Nade, hawakukuta mtu zaidi ya kiti kitupu na kamba zilizokatwa!
Nyokaa akatukana na kusaga meno. Akapiga ngumi kiganja chake na kuwatazama wenzake kwa macho mekundu.
“Mtafuteni huyo hayawani aliyediriki kumchezea simba sharubu! Upesi!”
Basi isijulikane na hata wanaume wengine walitokea wapi, jumla wakawa ishirini! Wengi wao walikuwa wamebebelea bunduki, na wachache, watatu kwa idadi wakiwa hawana silaha yoyote ile. Msako ukaanza!
Wakasambaa huku na huko. Wakibeba tochi na wengine wakiyakodoa macho yao kana kwamba matonge ya ugali ili wapate kuona wanachokitafuta. Hawakujua mvamizi ameelekea upande gani, ilikuwa ni kubashiri tu wakiwa wanaamini hatakuwa yupo mbali.
Uzuri kwao, eneo hili lilikuwa ni kubwa, kwa mtu kuvamia na kutoka, haikuwa rahisi. Ingemchukua muda mrefu, na akili pia kwani eneo lilikuwa limezingirwa na msitu mkubwa na njia fupi fupi zilizokomea mitini!
Lazima Nade apatikane. Na si hivyo tu, na huyo mvamizi pia apatikane kwa ajili ya adhabu na kueleza ametumwa na nani.
“Ananitania, hanijui vizuri!” alisema Nyokaa. Pembeni yake alikuwa amesimama Roba. Mkononi mwa Nyokaa kulikuwa kuna chupa kubwa ya kinywaji cha Ciroć, kikihudumia kinywa chake mara kwa mara.
“Ameuchokoza moto uliokuwa umezima, sasa ataona cha mtemakuni!” aliendelea kunena Nyokaa, alafu akajipooza na kinywaji chake.
“Tulifanya makosa sana kumwamini yule mshenzi,” alisema Roba. “Hatukuwa na haja ya kufanya naye mazungumzo yoyote yale, bali vitendo.”
“Nilimpatia nafasi ya kuyamaliza kwa amani,” akasema Nyokaa akitikisa kichwa. “Lakini kaniona fala. Sasa kichwa cha huyu malaya wake, pamoja na huyo mbwa aliyemtuma vitakuwa ni salamu zake tosha. Na kama hatamleta Miriam hapa, tutamfuata mwenyewe huko alipo!”
Wakati maongezi haya yanaendelea, Jona alikuwa anatazama. Alikuwa amejificha kwa kujibanza kando ya jengo akiusoma mchezo mzima. Kumbe wakati wanaume wametapakaa huku na huko kwenda kumtafuta, yeye alikuwepo pale walipopaacha.
Mtihani wake ulikuwa ni kutoka ndani ya eneo hilo akikwepa watu waliozagaa huko. Hili halikuwa gumu kwake kabisa kama angelikuwa mwenyewe, ila shida ni kwamba mgongoni mwake alikuwa amembebelea Nade aliyekuwa hoi.
Macho ya mwanamke huyo yalikuwa yanarembua kwa kuchoka. Mwili wake ulikuwa unanuka damu ukijawa na majeraha. Kama Jona angelimwacha pale, asingeliweza kwenda popote pale kwa maana hakuwa na nguvu hizo.
Jona akapiga mahesabu, kushoto ama kulia, kaskazini ama kusini. Kwa kuhofia kupotea ndani ya eneo hilo alikuwa ameikariri ramani ya eneo zima kichwani kabla hajafanya kazi yake hiyo. Alikuwa anajua wazi wapi kuna njia na wapi kuna kupotelea msituni.
Na basi kwa akili zake timamu akaamua kuenenda upande anaoujua hamna njia. Akifanya hivyo kwasababu za kiusalama zaidi akiamini ya kwamba wanaume wale waliotapakaa huko, watakuwa wamejijaza mahala penye njia wakidhani amezitumia.
Akihema taratibu na akikanyaga hatua fupi fupi za haraka, akasonga. Ndani ya ‘mamiti’ hali ya hewa ilikuwa ni ya ubaridi. Udongo ulikuwa ni wa kutitia ukilowanishwa na unyevunyevu. Kulikuwa ni giza, taa za makazi ndizo zikisaidia kwa mbali.
Wakati Jona akisonga, Roba akasikia sauti ya kukatika kwa kipande cha mti kaskazini mwake upande wa kushoto. Upesi akatazama eneo hilo. Alilitilia mashaka, ila akapuuzia. Hili likawa kosa lake kubwa mno!
Baada ya sekunde chache, roho yake ikiwa haijaridhika, akamwomba Nyokaa kurunzi na kumulika kule alipokuwa amepatilia shaka. Kurunzi ilikuwa kubwa yenye mwanga mkali mweupe. Aliipeleka mbele na nyuma akiangaza, lakini hakuona kitu!
Jona alikuwapo wapi?
Bada ya kurunzi hiyo kuzima na kiza kurudi ndani ya miti, sauti ya Jona inanong’oneza ndani ya msitu:
“Amka, twende!”
Kumbe alikuwa amelala chini, yeye pamoja na Nade. Anamnyanyua Nade na kisha anamuweka tena mgongoni. Wakaendelea na safari.
Lakini Roba hakukaa na amani tangu pale aliposikia mlio ule wa mti. Hakuchukua muda mrefu sana, akamuaga Nyokaa anataka kwenda kutazama hali kule alipomulikia kurunzi.
“Twende wote!” Nyokaa akaropoka akisimama kwa shida.
“Hapana,” akasema Roba. “We kaa hapa, nakuja muda si mrefu.”
Nyokaa akaleta ubishi kidogo, alikuwa chakari kwa kulewa. Hata kusimama likuwa tabu, Roba akamsaidia kwa kumshikilia. Akamtuliza kitako na kisha haraka akapandisha kwenda kutazama.
Ndani ya dakika mbili, Roba akaona alama za viatu kwenye udongo. Akachuchumaa na kuzitazama alama hizo vema, kwa kuusoma ulaini wa udongo akagundua adui alipita hapo ndani ya muda mfupi. Na kwa kusoma kina cha alama hizo, akajua adui alikuwa amembembelea mateka wao.
Basi akatabasamu maana aliona kazi imeshakwisha. Endapo adui huyo amembebelea mateka, basi hatakuwa na kasi ya kutembea wala kukimbia. Na alama zake za miguu zitaonekana kwa urahisi udongoni.
Akaona hamna haja ya kuita watu wengine, kazi ataimaliza kwa mkono wake mwenyewe. Haraka akaanza kusonga kwenda mbele. Alitumia macho yake kama kurunzi na alijitahidi kwa kadiri ya uwezo wake kutembea kimya kimya japo kwa upesi ili asimgutue adui mapema.
Macho yake yalitazama chini, na akitumia alama za miguu kama ramani. Akafikia mahali ambapo alama hizo zilikata. Akasimama na kumulika na kurunzi aone.
Mahali hapo ndiyo palikuwa sehemu ambapo Jona alilala punde baada ya kuona mwanga wa kurunzi kwahiyo Roba alipomulika kwa mbele kidogo, akafanikiwa kuona alama za viatu vya Jona vikiendelea, naye akaendelea kuvifuatilia.
Lakini pasipo kufahamu, akawa ametenda kosa lingine la pili ndani ya usiku huu. Kitendo cha kumulika kurunzi msituni kwa mara nyingine, kikamshtua Jona na kumtaarifu kuwa anafuatwa kwa ukaribu. Anapaswa kuchukua hatua!
Dakika tano mbele, Roba akafika tena mahali ambapo hakuona alama za miguu. Akasimama na kuangaza. Pembeni yake akaona mwili wa binaadamu. Haraka akawasha kurunzi kumulika. Akamwona Nade amejilaza!
Kwa tahadhari akasogea. Akamulika kushoto, kulia, mbele na nyuma. Hakukuwa na mtu wala alama za viatu. Alipotaka kumulika juu ya mti, mara vuuup! Jona akashuka kama radi akamparamia na kumwagusha chini!
Kurunzi ikarukia kando.
Jona akang’ang’ania shingo ya Roba wakishindana nguvu. Roba akamtupia mwanaume huyo mbali kwa kutumia miguu yake, alafu haraka akasimama. Naye Jona upesi akasimama kwa kujifyatua kama mtego wa panya.
“Huu ndiyo mwisho wako!” Roba akasema kwa msisitizo kisha akafikicha pua yake kama mtu mwenye mafua. Akamjongea Jona akijiandaa kwa pambano.
Ngumi na mateke yakarushwa kwa fujo! Kila mtu alikuwa stadi kwenye kukwepa mashambulizi ya mwenzake. Ngumi na mateke ya Roba yalikuwa mazito zaidi, lakini hazikufanikiwa. Jona alikuwa mwepesi mno kukwepa kana kwamba anacheza gemu la nyoka.
Kwa sekunde chache akausoma mchezo wa Roba, na sasa akaanza kucheza faulo za kuleta ushindi. Kila Roba aliporusha ngumi yake nzito, Jona akawa anaipisha na kuisukumia mbali kuharibu balansi ya adui.
Akafanya hivyo mara tano. Roba akajaribu kurusha teke, Jona akalikwepa na kugusa kidogo mguu ulioleta shambulizi , Roba akaenda kombo. Kuja kukaa sawa akamkuta Jona yupo hewani. Kabla hajavuta pumzi, akala teke la kibabe, likamnyanyua na kumtupia chini! Hoi!
Mdomo ulimwaga damu. Macho hayakuona vema, kichwa kikaita kwa miale ya maumivu makali. Lakini hakutaka kushindwa, akajikokota kunyanyuka. Akakunja ngumi apambane tena.
Lakini kwa mara hii haikumuwia vigumu Jona. Alijua adui yake hakuwa sawa, na basi akamruhusu arushe shambulizi lake yeye awe wa mwisho. Roba akaingia mkenge. Aliruhusu hasira zikamtawala. Akairusha ngumi yake kwa pupa, Jona akaiyeya kama amefungiwa ‘springi’, Roba akakatiza hatua mbili mbele, Jona akamrusiha nyuma kwa teke la kukunjuka lililomkita kifuani. Roba akalala tuli asionekane mwenye dalili ya kuamka!
Jona akamuweka Nade mgongoni, wakaendelea na safari. Wakatembea kwa hatua kumi na tano, mara wakamulikwa na kurunzi!
Watatoboa?