Anga la washenzi na Joana anaona kitu usiku

Anga la washenzi na Joana anaona kitu usiku

*ANGA LA WASHENZI -- 55*
*Simulizi za series*

ILIPOISHIA

Akazima taa na kisha kujimwaga kwenye kitanda kipana, maridadi kabisa, apate kulala. Kwa 'kajoto' kalichokuwepo, hakuhitaki kujifunika shuka.

Alikuwa amechoka mno kwa 'shughuli pevu' aliyopewa na Miranda. Hakudumu macho kwa muda mrefu, akapotelea usingizini akiwa anakumbuka raha alizopewa.

Raha za karne.

Lakini mkewe hakuwa amelala. Muda huo alikuwa anatiririsha machozi bujibuji. Alikuwa akisaga meno, kichwa kinamuwaka moto. Likapita lisaa limoja. Akashindwa kuvumilia.

Akanyanyuka na kutoka ndani ya chumba. Baada ya dakika tatu, akarejea akiwa ameshikilia kisu mkononi!

ENDELEA

Alikuwa amejawa na hasira kedekede. Hakuwaza tena kama ana watoto aliozaa na huyo mwanaume. Hakuwaza kama ana familia inayomtegemea, wala mambo lukuki waliyoyapanga na kuadhimia na huyo mwanaume. Hakuwaza kifungo cha maisha.

Aliwaza kuua tu kuridhisha nafsi yake kwa kuua.

Lakini anawezaje kufanya hili wakati hata kuchinja kuku hajawahi?

Akamsogelea mumewe aliyekuwa hajitambui, kazamia usingizini. Kifuani moyo wake ukimdunda haswa! Na jasho likiwa tayari limelowanisha gauni lake jepesi la usiku.

Mikono yake ilikuwa inatetemeka. Kisu kikienda huku na kule, akijitahidi kukituliza.

"Nitamkita tu tumboni ... hapana, anaweza akapona ... namkita kifuani. Si atakufa? ... Atakufa ndio!" Alikuwa anazoza mwenyewe na nafsi yake.

Lakini ghafla mwanga wa simu ukammulika usoni. Akashtuka mno! Kama isingelikuwa mbavu, moyo wake angeliukutia nje.

Ilikuwa ni simu ya mumewe. Kuna mtu alikuwa anapiga. Baada ya simu kutoa mwanga, punde sasa ikaanza kuita kwa wimbo kwanguvu. Mwanamke akachanganyikiwa. Hakujua cha kufanya kwa haraka.

Alitupia kisu chini kwa kupagawa, alafu upesi akaketi kwenye kingo ya kitanda. Akasikiliza simu ya mumewe ikiita ... ikiita ... ikiita.

Ikakata!

Ikaita tena. Lakini ikakata pasipo kupokelewa. Mara hii haikuita tena kwa muda mrefu kama hapo awali. Kwa muda wote huo Boka hakusikia chochote kile. Alikuwa akiendelea kukoroma kana kwamba hakuna kilichojiri.

Simu ilikata na kunyamaza kwa muda wa dakika kadhaa. Chumba kikarejea katika hali ya kiza, lakini mama hakukifuata tena kisu chake. Akaendelea kuketi kingoni mwa kitanda akifikiria mambo kadhaa kichwani.

Mara akanyanyuka na kwenda kutazama aliyepiga simu. Alikuwa ni mfanyakazi mwenziwe na mumewe. Akapuuza. Akaelekea kule kwenye jumbe, akainakili namba ya mtu aliyekuwa anachat na mumewe na kuihamishia kwenye simu yake.

Mara namba hiyo ikatokea na jina! Kumbe alikuwa nayo simuni.

Alikuwa ni Miranda.

"Malaya mkubwa!" Akajikuta akitusi. Amekunja ndita na ngumi kwa hasira. "Kumbe ni wewe! ... kumbe ni wewe unanizunguka?"

Akajiona mpuuzi sana. Kumbe mwanamke aliyeingia naye kwenye mahusiano ya kibiashara, alikuwa anamzonga nyuma ya mgongo!

Kichwa chake kikampitishia picha za kumbukumbu akiwa na mwanamke huyo, tangu siku ya kwanza kuonana naye. Siku wakiteta na kucheka.

Akaghafirika mno.

Akarejesha kisu jikoni kisha akajilaza kitandani akiwa sasa anapiga mahesabu ya kumpata Miranda. Hakujua atamfanya nini. Ila hakika hakitakuwa kizuri, hiko ndicho alikijua na kuwa na uhakika nacho.

Hakitakuwa kizuri.

Hakulala usiku wote huo.

***

Saa mbili na nusu asubuhi; ndani ya ofisi ya Kamanda mkuu wa polisi mkoa.

Kamanda akamtazama Alphonce kwa macho ya nje ya miwani akiwa ameshikilia gazeti la The Guardian mkononi. Kofia yake ilikuwa juu ya meza, amejilaza kuegemea kiti chake cha kunesa na kuzunguka.

Akamkagua Alphonce aliyekuwa amevalia suti kubwa rangi ya kahawia na mwenye sura ya ukakamavu, alafu akarudisha macho yake gazetini.

Kwa muda kidogo kukawa kimya kana kwamba hamna mtu ndani ya ofisi.

Kamanda akashusha pumzi ndefu puani, alafu akasonya kama mtu aliyesikitishwa na jambo. Akatoa macho yake gazetini na kumtazama Alphonce tena.

Kwa utaratibu akamuuliza:
"Tumeshindwana?"

"Hapana mkuu!" Alphonce akajibu kwa ukakamavu. Kamanda akawela gazeti lake mezani kisha akaendea kabati lake akitembea kwa uchovu. Akalifungua na kutoa faili kubwa zito jeusi alilolipekua karatasi kadhaa ndaniye.

Akaita,

"Alphonce," akiwa anaendelea kuliperuzi faili lake.

"Afande!" Alphonce akaitikia.

"Unajua nina kazi nyingi mno za kuzifuatilia. Kazi lukuki lukuki. Lakini sasa nashindwa kufanya kazi zangu hizo kwa ajili yako, uzembe wako, ubishi na ukaidi wako ..."

"Hapana, mkuu si ka --"

"Nyamaza!" Kamanda akageuka na kumtazama Alphonce kwa jicho la bundi. "Sitaki kusikia lolote toka kwako. Lolote! Unajua jana alikwenda wapi? Kufanya nini? Unachukulia haya mambo mepesi, sio?"

Kamanda akarejesha faili kabatini, akamsogelea Alphonce na kuketi juu ya meza akimtazama.

"Unajuwa wazi, tulimaliza familia yake. Tulichoma nyumba yake. Tuliharibu biashara yake. Tukaua washirika wake. Kwako ni mepesi hayo?"

"Lakini mkuu, kwanini tulimrejesha jeshini? Hukuona itakuwa salama yeye ang ---"

Twaaah! Kamanda akamzaba kofi zito Alphonce!

"Pumbavu wewe!" Akalaani. "Unadhani nilikuwa siyajui hayo? Jona alikuwa anahitajika kurudi jeshini kwa namna yotote ile. Huo ulikuwa ni msalaba wangu. Jukumu nililopewa kutimiza na IGP. Sikutia sahihi barua yake ya kujiuzulu mpaka leo hii. Jona anahitajika taifa zima. Haswa kipindi kama hiki!"

Kamanda akashusha pumzi ndefu. Akanyaka chupa yake ya maji makubwa ya Kilimanjaro yaliyokuwa mezani akagida mafundo kadhaa kujipoza.

"Ni jambo la muda mfupi tu. Nilikuambia umtazame kwa muda mfupi tu maana naamini wewe ndiye unayeweza hilo jukumu. Shida yangu ni kujua nyendo zake. Kujua kama anafuatilia nyayo zetu za damu. Basi!"

Akanywa tena mafundo kadhaa ya maji. Akamaliza chupa nzima.

"Sasa hivi, sitakuelewa tena, Alphonce ... sitakuelewa." Akarudia akimtazama mlengwa wake.

"Ni wewe tu ndiye wa kumfuatilia Jona. Kila hatua ... kila muda ... kila saa!"

Punde Alphonce akatoka ndani ya ofisi na kwenda kukaa ndani ya gari lake. Macho yake yalkuwa mekundu. Uso wake ulikuwa umevimba kwa hasira. Si kwasababu ya kuzabwa kofi, hapana. Moyo wake ulikuwa umejawa na wivu.

Wivu juu ya Jona.

Aliona Jona anathaminiwa kuliko yeye. Jona ni nani haswa? Kwani yeye ndiye jeshi lote la polisi nchini. Hili jambo lilimuuma sana. Lilikuwa linautoboa moyo wake.

Akiwa humo garini, punde akamwona Jona akizama ndani ya ofisi ya Kamanda kuripoti. Alikuwa amevalia suruali jeans na shati nyeupe aliyoichomekea.

Baada ya dakika kama tano, akatoka ndani ya ofisi na kwenda zake.

Alphonce akawasha gari.

****
 
*ANGA LA WASHENZI -- 56*

*Simulizi za series*

ILIPOISHIA

Punde Alphonce akatoka ndani ya ofisi na kwenda kukaa ndani ya gari lake. Macho yake yalkuwa mekundu. Uso wake ulikuwa umevimba kwa hasira. Si kwasababu ya kuzabwa kofi, hapana. Moyo wake ulikuwa umejawa na wivu.

Wivu juu ya Jona.

Aliona Jona anathaminiwa kuliko yeye. Jona ni nani haswa? Kwani yeye ndiye jeshi lote la polisi nchini. Hili jambo lilimuuma sana. Lilikuwa linautoboa moyo wake.

Akiwa humo garini, punde akamwona Jona akizama ndani ya ofisi ya Kamanda kuripoti. Alikuwa amevalia suruali jeans na shati nyeupe aliyoichomekea.

Baada ya dakika kama tano, akatoka ndani ya ofisi na kwenda zake.

Alphonce akawasha gari.

ENDELEA

Baada ya nusu saa ... Ocean road hospital

"Anaendelea vizuri, anaweza akaongea," alisema nesi kwa tabasamu huku akimtazama Jona.

Walikuwa wamesimama nje kidogo ya chumba alicholazwa mwanamke huyo.

"Kwahiyo naweza nikamwona?" Jona akauliza akiwa anatarajia kuruhusiwa. Mguu wake ulikuwa tayari umeshajiseti kwendaze.

"Mmmmh kwa sasa hapana," akasema Nesi. "Nimetoka kumdunga sindano ya usingizi muda si mrefu. Amekuwa halali, kuna mambo anayawaza sana bila shaka."

Jona akajitengenezea vizuri kumtazama Nesi.

"Kwahiyo usiku mzima hakulala?"

"Ndio. Alikuwa anamimina machozi tu na kuvuta makamasi. Sasa anakosa muda wa kupumzika kitu ambacho kinaweza kumpa shida. daktari akaniagiza nimpumzishe kabla sijaondoka maana shift yangu ishakwisha."

"Oooh!" Jona akatazama kushoto na kulia. "Naweza kuonana na daktari?"

"Bila shaka," Nesi akamjibu na kuanza kutembea. Jona akamfuata kwa nyuma mpaka ndani ya ofisi ya daktari, kisha Nesi akaenda zake. Jona akaendeleza maongezi na daktari.

Daktari akampatia maelezo ya kutosha juu ya hali ya maendeleo ya Nade.

"Anaonekana mwenye mawazo. Tungepata ndugu au wanafamilia wake nadhani wangetusaidia," daktari alisema akimtazama Jona kwa macho ya uhakika. Kisha akatazama tarakilishi yake ya mezani.

"Kwa ile dawa mliyompatia, atarudi kwenye fahamu zake muda gani?" Jona akauliza.

"Si muda mrefu in such kwani atahitaji kula chakula chake cha mchana," daktari akamjibu.

"Ok, then ntangoja," Jona akasema. Kisha kukawa kimya. Daktari alikuwa anatarajia Jona atatoka ndani ya ofisi yake muda si mrefu, ila haikuwa hivyo.

Akamtazama Jona. Wakakutana macho kwa macho.

"Dokta," Jona akaita. "Kuna mtu mwingine alikuja baada ya mimi kuondoka siku ile?"

Dokta akamtazama Jona kwa kukodoa. Jona akatambua swali lake hilo limemshtua mwanaume huyo muhindi. Hakukwepesha macho yake, akamtazama.

Dokta akahamishia macho yake kwa kioo cha tarakilishi.

"Watu wanakuja wengi afisa, kila saa na kila muda. Siwezi nikawakumbuka wote waliokuja baada yako," daktari akajielezea. Jona akiwa anaendelea kumtazama machoni, akamuuliza tena:
"Hakuna mwanaume uliyeonana naye muda mfupi baada ya mimi kutoka? ... Ni polisi."

"Hapana." Daktari akatikisa kichwa. "Hamna!"

"Una uhakika?" Jona akauliza.

"Ndio, hamna polisi aliyekuja hapa baada yako."

"Nikithibitisha alikuja, sitakuwa na soni nawe. Nitaenda kukulaza ndani kwa juma zima upate akili."

Daktari akawa kimya. Akamtazama Jona, akamwona ni mtu anayeongea kwa uhakika. Akahofia.

"Afande, nina kazi nyingi za kufanya muda huu. Tafadhali naomba unipatie nafasi," daktari akajitetea akijikaza kumtazama Jona.

Jona akatoa pingu ubavu wake wa kulia kisha akasimama.

"No! You dont have to do that, kaa chini tuongee," daktari akamwomba.

"Umekataa maongezi, sina tena huo muda wa kupoteza na wewe hapa," Jona akakaza.

"Si kwamba sitaki, nimeambiwa nisiseme!" Daktari akaropoka. Jona akaketi chini, akarudishia pingu yake.

"Mnaniweka kwenye wakati mgumu!" Daktari akalalama. "Huyu anakuja ananiambia hivi, mwingine naye anakuja ananiambia hivi. I am confused!"

Kwa utulivu, Jona akaanza kumdadisi. Daktari akamwambia alikuja polisi aliyemtaka aeleze kila kitu alichofanya pamoja na Jona. Baada ya kuambiwa kila kitu, akatoa kitisho kwa nesi na yeye, wasiseme kama alikuja hapo hospitali!

Jona alipopata taarifa hizo akashukuru sana, akamuaga daktari na kumwambia anaenda zake nje kupata chakula. Atakuwapo hapo mpaka pale Nade atakaporejea fahamuni wapate kuteta mambo kadhaa.

Akaenda kantini kula, akiwa hapo akawa anatazama saa yake na huku akitazama njia endapo atabahatisha kumwona Alphonce. Alijua wazi mwanaume huyo anamfuatilia.

Akawa anakula taratibu kuvuta muda.

***
Saa sita mchana ... ndani ya nyumba ya Miranda.

Dada wa kazi alimkaribisha Kinoo akiwa ameongozana na wanawake mapacha: Sara na Sasha, wanawake waliowahi kuwa wafanyakazi wa Bite kipindi yu hai.

Wanawake hawa kwa muda walikuwa wametengana ambapo Sasha alikuwa amesafiri akimwacha dada yake Sara aliyejipeleka mikononi mwa Kinoo kwasababu ya hofu. Sasa Sasha alikuwa amerejea, na jana yake tu wakawa na kikao pamoja na Kinoo juu ya mustakabali wao.

"Wewe ni mgeni hapa enh?" Kinoo akamuuliza yule dada wa kazi. Dada akatabasamu,

'"Ndio, nimekuja hapa wiki iliyopita tu."

"Oooh! Karibu sana," Kinoo akamkarimu kisha akajitambulisha kama rafiki mkubwa wa bosi wake. "Ukiniita Kinoo hutokuwa umekosea."

Dada akashukuru, kisha akawauliza wangependelea vinywaji gani wakati wakingojea Miranda aje. Wote wakaagiza maji ya kunywa. Dada akawapatia, na punde Miranda akatokea.

"Kinoo, umenikumbuka sasa! Yani wewe kama huna dili, hun'tafuti sio?" Miranda alisema akitabasamu. Wakakumbatiana na Kinoo na kusalimiana.

"Nakuona una ugeni."

"Yah! Huyu anaitwa Sarah na huyu Sasha."

Wakapeana mikono ya kutambulishana. Kinoo akamtambulisha Miranda na kisha wakateta habari za masiku ya kutokuonana.

Baada ya habari hizo, Kinoo akaeleza lililo kuu. Akamwambia Miranda kwamba Sara na Sasha wameazimia kuungana nao.

Jambo hili likamshtua Miranda, lakini hakufanikiwa kulionyesha. Akaomba apate faragha kidogo na Kinoo.

"Una akili timamu wewe Kinoo?" Miranda akastaajabu. "Umewaamini nini hao wanawake kuwafakamia kuwajaza huku?"

"Nina akili zangu timamu, Miranda," Kinoo akajipambanua. "Najua ninachokifanya. Mimi sio mwehu mpaka kukuambia hivyo. Ninawaamini kwa asilimia zote. Hawana la kufanya kwa sasa. Wanaweza wakawa asset nzuri sana kutusaidia."

"Unadhani BC atatuelewa kirahisi hivyo?" Miranda akauliza. Kinoo akamsogelea mwanamke huyo na kumshika bega.

"Najua BC anakuamini sana. Endapo ukiuweka ulimi wako vizuri, hawezi akakataa."

"Lakini, Kinoo," Miranda akatia shaka. "Mbona ni haraka hivyo? Mbona ghafla ghafla hivyo? Kuna nini?"

Kinoo akashusha pumzi ndefu na kutazama chini. Akarudisha macho yake kwa Miranda na kumwambia:
"Sarah ana mimba yangu."

Miranda akakodoa. "Wasema?"

***
 
*ANGA LA WASHENZI -- 57*

*Simulizi za series*

ILIPOISHIA

"Najua BC anakuamini sana. Endapo ukiuweka ulimi wako vizuri, hawezi akakataa."

"Lakini, Kinoo," Miranda akatia shaka. "Mbona ni haraka hivyo? Mbona ghafla ghafla hivyo? Kuna nini?"

Kinoo akashusha pumzi ndefu na kutazama chini. Akarudisha macho yake kwa Miranda na kumwambia:
"Sarah ana mimba yangu."

Miranda akakodoa. "Wasema?"

ENDELEA

"Sarah ana mimba yangu," Kinoo akasisitizia. Miranda akashusha pumzi ndefu na kuulaza mgongo wake kitini.

Akatikisa kichwa chake akimtazama Kinoo. Akamlaumu kwa jambo hilo la kipumbavu, kamwe hakulitegemea kwa mtu kama yeye.

"Unajua wazi situation yetu. And blindly you are about to make a family!" Miranda akalalama. Hawakuongea sana na Kinoo, akamtaka mwanaume huyo aende, amwache peke yake.

Kinoo akaendaze akiongozana na wanawake wake aliokuja nao. Walijipaki kwenye gari, Escudo ya grey, wakatimka.

"Umefanikiwa?" Sasha akamuuliza Kinoo baada ya kuacha makazi ya Miranda kwa hatua kadhaa. Kinoo akashusha pumzi ndefu. Macho yake yalikuwa yanatazama mbele lakini akiwa amezama fikirani.

"Ni jambo la kuchukua muda," Kinoo akajibu. "Lakini litakuwa sawa tu," akawatoa hofu.

Hawakuongea tena kwa muda. Sauti ya gari tu ndiyo ikawa inavuma na kuita.

**

Jona akatazama saa yake mkononi. Muda ulikuwa umeenda sasa. Alishamaliza kula na sasa akaona ni vema akienda kumwona Nade kama vile daktari alivyomwambia kwamba atakuwa macho kipindi cha kula chakula cha mchana.

Akanyanyuka na kulipia bili yake ya chakula, na kwa hatua nzito akajongea mpaka kwa daktari moja kwa moja. Yeye hakuwa anangojea msururu wa wagonjwa kwa kutumia kofia yake ya kazi.

Akiongozana na nesi, akaenda mpaka alipolazwa Nade, akamkuta mwanamke huyo akiwa anakula.

Nade akatabasamu kwa mbali kumtia Jona machoni. Ni kama vile alikuwa anataraji ujio wa mwanaume huyo. Alionekana bado hana nguvu, ila ilikuwa kheri. Akamkaribisha Jona kula.

"Nashukuru," Jona akasema kwa tabasamu la bati. Kisha "Nimefurahi kukuona," akasema akimtazama Nade machoni.

Nade akatabasamu kimaumivu. Jona hakumwongelesha tena, akamwacha amalize kwanza kula.

"Daktari kaniambia umekuwa na mawazo sana hapa karibuni, nini shida?" lilikuwa swali la kwanza Jona kuuliza.

Nade akajilaza kwanza kitandani. Akawa kimya kwa muda. Mara macho yake yakaanza kulowana na hatimaye kuvujisha machozi.

Kuna kitu kilikuwa kinamsumbua kifuani. Jona aliliona hilo. Hakutaka kumlazimisha kuongea, akamngojea kwa wakati wake sahihi.

"Nisamehe sana, Jona," Nade akasema akitazama dari. Macho yake bado yakiendelea kuvuja kama mto.

"Nimekukosea sana, najua hilo. Umekuwa ukinipa mkono wakati mimi nikikukabidhi kisu. Umetetea uhai wangu lakini mimi nikifanya jitihada kuupokonya wa kwako. Nisamehe sana. Sistahili hata msaada wako."

Uso wake ukawa mwekundu. Mafua yakaanza kumtambalia, na kwikwi za kilio zikampalia.

Akamwomba sana Jona msamaha. Jona akamsihi hana haja ya kufanya hivyo kwani alishamsamehe, hata hivyo alifanya hayo kwasababu za ushawishi wa bosi wake, marehemu Eliakimu.

"Nataka tu uniweke bayana kile ambacho bosi wako alikuwa ananificha. Naomba unisadie kwenye hilo," Jona akampendekezea, lakini hakutaka kumpa presha mwanamke huyo kutokana na hali yake, akamtaka apumzike, na utakapofika muda basi wataongea kwa urefu na mapana.

Lakini Nade akakataa.

"Tuongee tu hata sasa," akateta kwa sauti ya chini ya msisitizo. Uso wake ulikuwa mzito ukizongwa na majuto ya kujiona mkosefu. "Huna haja ya kungoja, Jona, ntakwambia hata sasa."

Kisha akakaa kimya. Bado macho yake yakimwaga machozi.

Kwa uchungu mkubwa, akaanza kufunguka kinagaubaga. Akamweleza Jona ni kwa namna gani Eliakimu alivyokuwa anacheza mchezo wa damu kwa kutumia mkono wa serikali.

Namna gani alivyokuwa anashiriki magendo na biashara haramu na vitu hivyo vikamvunisha pesa nyingi mno. Namna alivyokuwa akishirikiana na magenge ya wauaji, madawa ya kulevya, utakatishaji wa fedha na kadhalika na kadhalika nyuma ya pazia.

Na ni kivipi alivyokuwa anatumkika kama mkono wa kushoto wa bwana Eliakimu akitumwa kuwamaliza maadui zake, na hata wale washirika wake waliomzulumu baada ya kupiga dili.

Akamweleza Jona yote kumhusu BC na Sheng. Namna anavyowafahamu, na jinsi walivyoshirikiana na hao watu kutimiza kazi kadhaa za kimagendo, ikiwamo kuingiza nchini makemikali yaliyokatazwa, pia hata madawa ya kulevya.

"Tulifanya hivyo kwa siri sana tukitambua wazi BC na Sheng walikuwa ni maadui wakubwa kibiashara, lakini tukafanikiwa kula na vipofu."

Akamwambia pia Jona ni kwasababu gani walikuwa wanamuwinda Miriam, na kwanini basi mwanamke huyo alikuwa anatakiwa kuuawa japokuwa ni mke wa Eliakimu.

"Kwanza Miriam hakuwa anampenda Eliakimu hata kidogo. Eliakimu alikuwa analijua hilo, lengo la mkewe lilikuwa ni kurithi tu mali zake pindi atakapofariki ama kumuua. Ilifikia kipindi Miriam akawa anatembea na mshirika mmoja wa kibiashara wa Eliakimu, mwanaume huyu akiitwa Nyokaa, mfanyabiashara wa madini Arusha.

Nyokaa alikuwa amekorofishana na Eliakimu kwasababu za kibiashara. Kila mmoja akawa anataka kulipa kisasi kwa mwenzake kwa kutuhumiana kurudishana nyuma, lakini kiuhalisia ni Eliakimu ndiye alikuwa na makosa. Aliingia dili na Nyokaa, mwisho wa siku akamsaliti kwa kuchukua kiasi fulani cha mzigo wake na kumdanganya ulipotelea njiani kwasababu za kiusalama.

Kulipiza kisasi na kurejesha fedha yake nyingi, akafanikiwa kumlaghai Miriam ili amtumie kunyooshea biashara zake kwa mtandao wa Eliakimu."

Jona akakuna kidevu chake. Akajikuta anapata kiu ya kutaka kujua zaidi na zaidi kadiri alivyokuwa anaelezwa.

Akataka kujua kwanini Nade hakutumwa kummaliza Nyokaa baada ya kuyatambua hayo. Nade akamwambia asingeliweza hilo kwani Nyokaa ana jeshi kubwa la watu.

Si rahisi kumkamata kama kutamka.

"Tulikuwa tunataka kumrejesha tu Miriam kwani alikuwa anajua mengi kumhusu Eliakimu, kwahiyo kuwa mikononi mwa adui, ilikuwa ni hatari sana."

Lakini zaidi, Eliakimu asingeweza kutekeleza mipango na mambo yake yote haya akiwa peke yake. Hilo lilikuwa bayana.

Ni lazima kuna watu vitengo na maeneo mbalimbali aliokuwa anasaidiana nao.

"Ni watu wengi mno," akasema Miranda. "Kila mtu na eneo lake, kila mtu na kitengo chake. Kila mtu akicheza nafasi yake kutimiza maagizo ya Eliakimu. Na kwasababu alikuwa anatoa pesa nono, haikumuwia vigumu kuwakamata."

Sasa Jona akaona kuna haja ya kutia nguvuni watu hao wote, lakini ushahidi ni muhimu sana kwenye hili. Ataupataje? Na atawapatia wapi watu wote hawa waliokuwa wanashirikiana na Eliakimu?

"Usijali," Nade akamtoa hofu. "Eliakimu alikuwa ana orodha ya watu wake wote aliokuwa anafanya nao kazi, pamoja pia na mawasiliano yao."

Akamwelekeza Jona wapi atavipata.
"Chumbani kwake, kwenye droo za kitanda, utakuta nyaraka zake zote humo. Ufunguo wa droo hizo huwa anauweka ndani ya moka zake ndefu nyeusi kwenye stendi ya viatu."

Jona akashukuru kwa taarifa hizo. Lakini kabla hajaondoka, akamsihi mwanamke huyo asimweleze mtu mwingine yoyote juu ya habari alizoongea naye. Nade akamhakikishia hilo kwa kuapia na maisha yake.

"Sitakusailiti tena kwa sasa."

Jona akaenda zake.



***
 
*ANGA LA WASHENZI -- 58*

*Simulizi za series*

ILIPOISHIA

Akamwelekeza Jona wapi atavipata.

"Chumbani kwake, kwenye droo za kitanda, utakuta nyaraka zake zote humo. Ufunguo wa droo hizo huwa anauweka ndani ya moka zake ndefu nyeusi kwenye stendi ya viatu."

Jona akashukuru kwa taarifa hizo. Lakini kabla hajaondoka, akamsihi mwanamke huyo asimweleze mtu mwingine yoyote juu ya habari alizoongea naye. Nade akamhakikishia hilo kwa kuapia na maisha yake.

"Sitakusailiti tena kwa sasa."

Jona akaenda zake.

ENDELEA

Lakini kama ilivyo ada, nje ya hospitali Jona akaonekana na Alphonce aliyekuwa ameketi ndani ya gari lake. Mwanaume huyu akamtazama Jona akiishilia, kisha akashuka garini na kuzama ndani ya hospitali.

Moja kwa moja akaonana na daktari na kumtaka afanye vile alivyokuwa anataka, amweleze yale yote Jona aliyoyafanya hapo. Kama haitoshi, akambana pia na nesi, ila bahati si kwake nesi wa zamu, yule aliyekuwa na Jona, alikuwa tayari ameshaondoka.

Akaagiza aonane na Nade.

Akaongozwa na nesi kupelekwa huko chumbani. Akamkuta Nade akiwa amelala. Akamwamsha.

"Naweza nikaongea na wewe machache?" Alisema kwa sura ya bati kisha akamtazama Nesi kwa uso wa kumwomba nafasi. Nesi akaenda zake.

Nade akamtazama Alphonce kwa macho makali akinyanyuka. Akakunja ndita zake na kuuliza:

"Kumbe ni wewe?"

Mwanamke huyu alikuwa anamtambua vilivyo Alphonce! Tayari kichwani kwake akajua mambo si shwari.

Alphonce akatabasamu. Akatoa leso kwenye koti lake la suti kisha akajifuta viganja vyake.

"Ndiyo ni mimi. Bila shaka ni muda mrefu umepita," akasema kwa sauti nzito.

"Unataka nini hapa?" Nade akamuuliza. Alphonce akamkazia macho mwanamke huyo.

"Unajua nataka nini, Nade. Mimi ni polisi, umesahau?"

"Polisi gani wewe?" Nade akastahamaki. "Wewe ni muuaji tu uliyevaa sare za polisi. Hujawahi kuwa polisi hata siku moja!"

Alphonce akaguna. Na mara akatabasamu.

"Sijaja hapa kulumbana na wewe, Nade. Nina mambo mengi ya kufanya, kwahiyo tafadhali jali muda wangu nia--"

"Sitakuambia kitu!" Nade akamkatiza. "Usitarajie nitakwambia lolote lile, Alphonce. Kwa hilo sahau."

"Utakuwa unatania!" Alphonce akastaajabu. "Unajua wazi mimi na wewe tupo behewa moja. Unadhani kutokuniambia kitu kutakuweka wewe salama? Embu acha ujinga. Hii ni kwa ajili yetu wote. Niambie nini Jona alikuwa anataka toka kwako na kwanini alikuwapo nyumbani kwa Eliakimu siku ya tukio?"

Nade akatabasamu. Akatabasamu tena zaidi.

"Alphonce, naona hunielewi. Nimechoka na haya mambo, nipo tayari kufa lakini siyo kuendelea kufanya makosa yaleyale. Niliyofanya yanatosha, usidhani ntakusaidia wewe ukayaendeleze. Enough is enough!"

"Acha upumbavu Nade!" Alphonce akafoka. Sura yake sasa ilibadilika na lile tabasamu la mwanzoni halikuwapo tena. "Acha ujinga wewe mwanamke! Unataka kwenda kuozea jela? Do you know how serious this matter is?"

Nade akatabasamu akimtazama mwanaume huyo. Akamshika mkono na kumwambia kwa upole:

"Yamekwisha, Alphonce. Kila zama zina mwisho wake. Umeshachelewa. Jiandae kwa anguko lako."

Alphonce akapandwa na hasira kali. Akamkaba mwanamke huyo mpaka alipohakikisha amekufa. Akawaza nini cha kufanya, akawaza ni nini Nade atakuwa amemwambia Jona.

Kichwa chake kikazunguka kwa msongo wa mawazo. Akanyanyuka na upesi akatoka ndani ya chumba. Hakuonana na daktari wala nesi, akanyookea moja kwa moja ndani ya gari lake..

Akaliwasha na gari lilivyoanza kwenda ndipo akapata akili juu ya nini cha kufanya. Aliamini Jona atakuwa ameelekea nyumbani kwa Eliakimu. Maneno ya Nade yalimshawishi aamini hivyo.

Akaamua kueleka huko pasipo ajizi.

***

Klak! Klak! - Klak! Klak! Kitasa kikalia pasipo mlango kufunguka. Jona akajaribu kuupush kwa uzito wake, akashindwa. Mlango ulikuwa mgumu na mzito.

Basi akarudi nyuma na kuukita teke, ukavunjika! Akazama ndani ya chumba hiki cha Eliakimu na kuanza kupekuapekua kwa macho yake.

Kitanda kilikuwa hovyo. Na kulikuwa kuna nguo kadhaa juu yake. Kabati la nguo lilikuwa limefungwa nusu, dirisha nalo likiwa limesukumwa kidogo.

Haraka Jona akatazama droo za kitanda. Akazisogelea na kujaribu kuzifungua kama zipo wazi. Akaona zimefungwa. Akapata tumaini.

Akachukua ufunguo kule alipoelekezwa na Nade kisha akafungua droo hizo. Ndani akakuta mafaili kadhaa, akayapekua kwa haraka haraka na kuyakusanya. Akatoka ndani ya chumba.

Kushika korido, akakutana uso kwa uso na Alphonce aliyekuwa amesimama mlangoni.

"Habari yako?" Alphonce akasalimu kinafki. Kisha akatabasamu na kuuliza:

"Nimekushtua, unh?"

Jona akasonga mpaka sebuleni akitembea kwa kujiamini.

"Kivuli changu kitawezaje kunishtua?" Akauliza akisimama. Kati yao kulikuwa na hatua kama nne tu zikiwatenganisha. "Najua umekuwa kivuli changu ukinifuata kila ninapoenda. Nakutarajia kila ninapotoa mguu."

Kukawa kimya kidogo wakitazamana kwa macho ya tahadhari. Alphonce akatazama mkono wa Jona, kisha akayarudisha macho yake usoni mwa mwanaume huyo.

"Umekuja kufanya nini hapa?" Akauliza.

"Hiyo si kazi yako," akajibu Jona.

"Nani amekuruhusu kuja hapa?" Alphonce akauliza tena. "Hii kesi haikuwa yako bali ya inspekta Faridi."

"Najua," Jona akajibu. "Hii kesi ni yangu pia kwani nami nahusika ... actually, nimewasiliana pia na Faridi juu ya hili."

Kukawa tena kimya. Akili zao zilikuwa zinaongea mengi kuliko midomo.

"Kwahiyo basi, ungeniwia radhi ukanipisha niende zangu," Jona akapendekeza. Alphonce akamtazama mwanaume huyo kwa kuminya macho kisha akamtaka amkabidhi kile alichokuwa amekishika mkononi.

"Kwanini nikukabidhi? Wewe unahusika na kesi hii?"

Alphonce hakujibu hayo, badala yake akaendelea kumsisitizia Jona amkabidhi yale mafaili. Na sasa akamtishia endapo asipifanya anachokitaka.

Jona akacheka.

"Unadhani unaweza ukanifanya kitu?" Akamuuliza. "Ni mara ngapi umejaribu kuniua ukashindwa?"

Alphonce akabinjua lips zake asiseme kitu.

"Au unadhani sifahamu hilo? Ukamuua na mfanyakazi mwenzangu pia ... yote nayafahamu. Usidhani mimi ni mjinga, Alphonce. Nangoja muda wangu ufike," Jona alisema kwa sauti makini akiwa amezamisha mkono wake wa kushoto mfukoni.

Alphonce akaguna kidharau.

"Wakati gani huo Jona? Unadhani unaweza ukapigana na ukuta?" Kisha akacheka. "Kutaka kujua vingi, kulimuua paka. Kwanini usicheze kwa mujibu wa ala ya muziki?"

Akaongezea:

"Jona, hakuna mtu aliye upande wako. Tambua hilo. Unatakiwa kubaki jeshini, lakini acha kufuata nyayo za wakubwa zako, ikiwemo mimi kwani kamwe hautafanikiwa!"

Jona hakusema kitu ila moyoni alikuwa anapasuka.

"Uliacha jeshi, mbona umerudi? Kwa mwerevu angejifunzia hapo."

Jona akasaga meno. Alikabwa na hasira kali, lakini akipambana asiionyeshe. Bado kuna kitu alikuwa anakitaka toka kwa Alphonce.

"Mliteketeza familia yangu, mkaharibu kila kitu changu. Niliwakosea nini?"

Alphonce akacheka. "Nimeshakueleza, Jona. Na ukiendeleza ukaidi, mkono huu ulioteketeza familia yako, utakuteketeza na wewe pia!"

"Nani alikutuma, Alphonce?" Jona akauliza. Macho yake yalikuwa mekundu kama bendera.

"Sina muda wa kuzoza tena, Jona," Alphonce akamjibu. Kisha akamuamuru:
"Nipe hayo mafaili au niyachukue kwanguvu?"

Jona akayaweka mafaili mezani.

"Haya hapa. Chukua."



***
 
Back
Top Bottom