*ANGA LA WASHENZI II --47*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Kichwa hiki kilikuwa cha bwana Graham, bwana aliyeenda zake asubuhi ya siku hii kwenda kutimiza agizo la Bwana Brown la kummaliza Miranda na Jona.
Kwenye mdomo wake alikuwa ana karatasi yenye ujumbe.
ENDELEA
Bwana Brown akatahamaki haswa kuona haya. La haula! Akatoa karatasi hiyo mdomoni mwa kile kichwa cha bwana Graham na kukisoma.
‘Don't you ever do that again!' Kikaratasi kiliandikwa vivyo. Bwana Brown akakichanachana kwa hasira akiwa amepaliwa na ghadhabu kuu kifuani mwake.
Akang'ata meno na kutazama huku na kule. Mbili haikuwa inakaa wala tatu haikuwa inasogea. Alikasirika mno na akawaza mawazo kadhaa kichwani mwake. Nani aliyemuua Graham?
Jona asingeweza kufanya haya, aliamini hilo. Wala si yule rafiki yake, yaani Marwa. Hakuwa na uwezo huo wa kumwangusha mtu kama Graham.
Hapa ni Miranda pekee.
Kichwa hiki na huu ujumbe anamaanisha nini? Bwana Brown aliwaza. Ina maana Miranda amekaidi maagizo yake? Ina maana ...
Ina maana Miranda ameamua kumkingia kifua Jona?
Bwana Brown akajikuta anatabasamu katika haya. Alimtuma kijakazi wake amletee sigara yake kubwa na alipoitia kinywani akainyonya kwanguvu na kutema moshi kando.
Alivuta sigara hii kama kichaa. Nadhani unajua huwa anafanya hivi akiwa kwenye hali gani. Alipovuta sigara mbili na kuzimaliza ndiyo angalau kichwa chake sasa kikatulia.
Akawaza na kukubaliana mambo kadhaa na kichwa chake. Ahitaji tena kufanya kazi na WASWAHILI. Sasa kazi zake atazifanya na waingereza wenzake tu.
“where is Randon? Call him for me!" Aliagiza kwa mdomo wake mkavu utemao moshi. Punde kidogo kijana mrefu, mwili mpana ndani ya suti kana kwamba mwanasheria mahakamani, akawasili.
Akasimama kwa ukakamavu akimtazama bwana Brown.
“from today, you will be my assistant supervisor. You will monitor your colleagues and make sure all things are under control," alisema Bwana Brown kisha akamtaka mwanaume huyo awaite wenzake wote hapo.
Akalitekeleza hilo na ndani ya muda mfupi, wakawasili na bwana Brown akawaambia juu ya uteuzi wake. Wote wakaafiki.
Sasa bwana Brown akampatia kazi bwana Randon. Kazi yake ya kwanza. Yeye pamoja na wenzake wawili, hivyo jumla watatu.
Kazi hiyo ikiwa ni kummaliza Jona na Miranda. Hakuwapa hata muda wa kujivuta. Akaagiza ndani ya masaa matano kazi iwe imekwisha!
**
Saa kumi jioni ...
Gari la Miranda, Range rover sport, ilitua mbele ya nyumba ya Kinoo, bwana huyo akashuka wakaagana na kisha akaenda zake ndani.
Hakumkuta mkewe, ila punde akawasili akiwa amebebelea mfuko mweusi wa rambo. Alisema ametokea sokoni.
Na alipoketi akamuuliza kuhusu ile gari kama ni ya Miranda. Alipojibu ndiyo. Akamuuliza, “umefanikisha ile ishu?"
“ishu gani?" Kinoo akatoa macho.
“naweee! Ina maana tuliyoongea jana umeshayasahau?" Sarah akatahamaki.
“nini tuliongea jana?" Kinoo akauliza. Sarah akasonya na kisha akanyanyuka na kujiendea zake pasipo kusema kitu. Kinoo akabaki akiduwaa.
Akawaza kidogo kabla hajashusha pumzi ndefu na kwenda zake kujinywea maji. Akarejea sebuleni kisha akatulia kwa muda kidogo. Hapa akakumbuka ‘ujinga' alioufanya jana usiku wa manane pamoja na mkewe.
Akatikisa kichwa chake na kuzama zaidi kwenye mawazo. Akawaza sana hatma yake na maisha haya. Akafikiria kile Miranda alichomwitia, kuwa ameamua kuachana na Bwana Brown na anamtaka wafungue ukurasa mpya wa maisha yao.
Akawaza sana na mwisho wa siku hakuona anga nyeupe kabisa. Maisha yalikuwa yanaelekea kuyumba. Kila kitu BC ndiye anatia mkono, leo wakiwa ‘yatima' mambo yataenda?
Ni wazi yatachukua muda. Na hata zaidi, roho zao zitakuwa rehani kwani vipi kama bwana Brown akiazimia kuwasaka na kuwamaliza?
Akashusha pumzi.
“Sarah!" Akaita akiwa amelaza kichwa chake kitini. Mkewe akaja pasipo kuitika.
“mke wangu, nimefikiria kuhusu lile jambo tuliloliongea jana usiku, na nimeona lile wazo lako ni vema. Mambo hayapo kwenye mstari na huenda tukicheza tukakosa yote haya."
Sarah akatabasamu. Bado hakutia neno.
“nimeshapata ninachokitaka," alisema Kinoo. “nimeshajua wapi wanapoelekea pia kuweka makazi yao mapya. So kilichobakia hapa ni kutoa tu siri hiyo tupate cash tufanye mambo mengine. Ikiwezekana tuondoke kabisa katika mji huu!"
Hapa sasa Sarah akafungua kinywa, “hayo ndiyo maamuzi ya kiume sasa?"
Akamkumbatia mumewe kwa furaha.
“Shetani akikosa namna, humtuma mwanamke."
***
Saa kumi na mbili jioni kuelekea saa moja usiku ...
Gari aina ya Toyota Prado nyeusi ilitoka kwenye makazi ya bwana Brown Curtis ikiwa katika mwendo wa wastani.
Gari hiyo ilivuma na barabara kwa dakika tano, ikafika mahali pa kona ili kuishika barabara iliyonyooka kwenda mpaka huko kuitafuta town.
Ilipokata kona hii ... Mambo yakabadilika haraka mno! Badala ya kukutana uso kwa uso na barabara, gari hii ya bwana Brown ikakutana uso kwa uso na kifo!
Ni katika namna ya ajabu. Mbele limesimama gari, Subaru, ikiwa imetanua mbawa zake kama mwewe anayetaka kupaa. Na kwenye mbawa hizo walikuwa wamesimama wanaume sita kwa ujumla. Kumbuka ni hatua chache tu toka kwenye kona.
Wanaume hawa kila mmoja alikuwa amebebelea bunduki aina ya short machine gun (SMG) ambazo zimejawa na risasi za kutosha. Na tayari zimesha-kokiwa kwa ajili ya kazi.
Ee bwana weh!
Baada ya kitendo kilichochukua sekunde tatu tu cha gari la Bwana Brown kuchomoza, ikaanza kunyesha mvua za risasi haswa. Gari liliminiwa ‘njugu' za kutosha. Kioo kilikuwa nyang'anyang'a. Uso wote wa gari uliharibika vibaya mno.
Kioo kilikuwa chekundu kwa damu.
Gari lilitulia likifuka moshi.
Hakukuwa na alama ya uhai.
Wale wanaume baada ya hili tukio lililodumu kwa dakika tano tu, wakajitweka ndani ya gari lao na katika zile mbio uzionazo runingani kwenye mashindano, wakatimka!
***
“Good job. Are you sure he was in?" Sheng aliuliza.
“hapana. Tulichokifanya ni kumiminia tu risasi gari lake katika namna ambayo haitamwacha salama yeyote aliye ndani."
Si haba kwa Sheng. Aliwapongeza vijana wake kwa kufanya kazi hiyo vema, mengine atayaona kwenye taarifa ya habari.
Ila kabla hajawaruhusu vijana hao waondoke, simu yake ya mezani ikaita. Akapokea na kuiweka sikioni.
“yes ... Serious? ... Tell me the address ... Ok!"
Alipokata simu akatabasamu na kuwatazama vijana wake wa kazi. Akawaambia kuna kazi ya kufanya imepatikana. Na kazi hii haitakiwi kulala hata kidogo.
Akawatajia eneo ambalo inabidi wakafanye tukio. Na kazi hiyo ni kummaliza Jona na Miranda! Taarifa imeshatolewa juu ya wapi wanapopatikana.
Basi vijana wale wakiongozwa na ‘waskaji' wake Lee, wakapokea agizo hilo na kuahidi kulitekeleza. Bwana Sheng akawaahidi endapo watatekeleza kazi hiyo, kila mmoja atapata kiasi cha milioni hamsini taslimu!
Pesa shetani. Nani asingetaka mambo haya?
***
Usiku wa saa tano ...
Usiku wa saa sita ...
Sheng alitazama saa yake. Ilikuwa vema haimdanganyi. Akachukua mvinyo na kuumiminia kweye glasi. Akagida na kuumaliza wote kabla hajamiminia tena glasini.
Akapiga simu. Iliita. Haikupokelewa. Akaendelea kunywa zake kinywaji. Baada ya punde chache, akasikia hodi mlangoni. Akasimama upesi na kuendea mlango.
Alipofungua alikutana na sura ngeni. Zaidi akakutana na mdomo wa bunduki.
*****