*ANGA LA WASHENZI II -- 51*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Akatazama, hola! Patupu!
Akahisi miguu imemwishia nguvu. Akahisi mwili umekuwa wa baridi kama barafu. Akahisi haja zote kwa mpigo!
Bam! Bam! Bam! Mlango ukabamizwa tena na tena.
ENDELEA
Akajikakamua na kuuendea. Alipofungua akakutana na mwanadada Miranda. Moyo wake ukapiga fundo kubwa, ila akajitahidi kubana hisia.
"Miranda!" akaigiza kutahamaki. "mbona bila taarifa mama?"
Miranda hakujibu. Akazama ndani na kwenda kuketi kitini. Akakunja nne.
"Habari yako?"
"Salama," akajibu Miranda na kisha akauliza, "vipi wewe?"
"Mimi niko poa tu," akasema Kinoo. Ila kiuhalisia hakuwa salama. Hata uso wake ulimsaliti. Alijawa na hofu. Na kwa namna fulani alikuwa anasutwa roho.
Akajichekesha.
"karibu bana. Naona Leo umeamua kun'tembelea!"
"Kinoo," Miranda akait kisha akamtazama mwanaum hiyo machoni na kumuuliza, "mkeo yupo wapi?"
Kinoo akatazama kando na kando kisha akasema, "sijui ameenda wapi. Ametoka kidogo."
"Una uhakika?"
"yah! Hayupo ndani. Vipi kwani kuna shida yoyote?"
"Hamna shida kwangu. Ila shida ipo kwako."
"shida gani?"
Miranda hakusema kitu. Akabaki akimtazama Kinoo kwa sekunde kadhaa. Akatazama chini na kisha akashusha pumzi ndefu.
"Kinoo," akauvunja ukimya kwa kuita. "Kama isingalikuwa wewe ni jamaa yangu niliyetoka nawe mbali, hata sasa ningekuwa nishakumaliza. Sijui ni nini kimekukalia kichwani mpaka ukadiriki kututoa sadaka kiasi hiki."
Kinoo akakunja sura kwa mkanganyiko.
"Sijakuelewa. Ni nini unamaanisha?"
"Unajua kila ninachokisema hapa, Kinoo. Wewe si mgeni hata kidogo. Unajua ulichokitenda na kama nakusingizia, nitazame unambie haujui."
Kinoo akatazama chini.
Kukawa kimya kwa sekunde kadhaa.
"Ni yule mwanamke, sio?" Miranda akauliza. Kabla hajapewa jibu, akaendelea kunena, "tangu alipoingia mwenye maisha yako nilijua vitu havitakuwa kama vilivyokuwa hapo awali. Nilifahamu fika, na ndiyo maana hata kukushirikisha tena kwenye mambo yangu nilisitisha."
Akanyamaza. Kinoo bado alikuwa anatazama chini.
"sasa yupo wapi hiyo mwanamke? unajua hata alipo hivi sasa? ila mimi nipo hapa. Nipo hapa kama nilivyokuwapo tangu nyuma. Je kama ningaliuawa, nani angalikuwa nawe hapa?"
Kinoo hakusema kitu. Ila macho yake yalianza kuwa mekundu.
"Hata pesa si hajakuachia?" Miranda akaendelea kunena. "Amekuacha kama alivyokukuta ... Nimeshangaa sana ni kwa namna gani alivyokufanya mjinga. Ulikuwaje mjinga kiasi hiki ndugu?"
Kimya. Miranda akasimama.
"Nakutakia maisha mema," akasema na kwendaze kuelekea mlango, ila Kinoo akamdaka mkono na kumsihi akae. Sasa macho yake yalikuwa mekundu zaidi.
"Miranda," akaita. "Nisamehe sana. Nastahili kuadhibiwa vikali. Siku zote umekuwa mkarimu na kama dada kwangu ila nikachagua kukuangamiza. Nimekabwa na hayà, hata uwepo wangu ni unafki mtupu.
Tafadhali, naomba uniangamize. Nami nimeridhia kwa hali zote."
"Sina haja ya kukuua, Kinoo," Miranda akajisemea. "Nina damu nyingi za kuziangamiza ila yako si mojawapo. Niliona tu tuachane kwa amani. Kila mtu akawa na maisha yake. Inatosha."
Ila Kinoo bado hakuwa radhi kumruhusu Miranda aende zake. Akiwa amemng'ang'ania mkono akamsisitiza amsamehe. Na yupo tayari kufanya lolote lile kama nauli ya msamaha wake."
Baada ya hiyo kauli, Miranda akaketi na kusema,
"Kuna kazi ya kufanya. Upo tayari?"
**
Saa nane mchana ...
"Kwahiyo una mpango gani na hiyo mimba?" Aliuliza Sasha kisha akapooza koo lake na kinywaji kikali.
Walikuwa wameketi sebuleni. Nyumba hii ni kubwa na ya kupendeza. Samani zake pia ni za gharama kubwa.
"Sijui nafanyaje!" Akasema Sarah. Alikuwa amejilaza kiuchovu kochini. "Siwezi kusema niitoe. Ni kubwa sasa. Ni hatari!"
Sasha akanyamaza kwanza. Akajinywea mafundo mawili kisha akasema, "kwahiyo utaubeba huo mzigo mpaka lini?"
Sarah akabinua mdomo. "Mpaka pale nitakapoutua. Hamna namna."
"You are not serious!" Sasha akang'aka. "Alafu huyo mtoto unakuja kumwambia baba yake nani?"
"Amekufa."
Sasha akacheka.
"Anyway, inabidi ufanye namna. Mimi sijaona haja ya kubeba mzigo huo. Na kuhusu ukubwa wa mimba, sio shida. Madaktari wapo, wazuri tu ninaowaamini. Nakupa muda wa kufikiri, utanambia. Sawa?"
Sarah hakujibu. Alitazama zake kando. Sasha akanywa mafundo kadhaa na kumaliza chupa yake, ndipo Sarah akanena, "kwahiyo itakuwaje kuhusu Kinoo?"
"Itakuwaje?" Sasha akatahamaki. "Itakuwaje nini? Haitakuwa kitu."
"Kwahiyo atabaki hai?"
"Aaahm yah! Atabaki hai ndio. Ila kwa muda."
"Unamaanisha nini kwa muda?"
Sasha akanyamaza kana kwamba hakusikia. Sarah akarudia kuuliza, "una maanisha nini? Mtamuua?"
"Bado unampenda? Mbona unajali sana?"
Sarah hakujibu. Macho yaliyomtazama dada yake yalionyesha anataka majibu na si maswali.
"Ana nafasi moja tu ya kujitetea. Kama asipotoa taarifa yenye kuzaa matunda hivi sasa, nadhani Sheng atamuangamiza."
"Ila taarifa anazotoa ni sahihi!" Sarah akang'aka.
"Sijakataa. Ila hazizai matunda. Na Sheng anawaza kuwa huenda akitoa taarifa huwapasha pia na wenzake!"
"Hapana. Hafanyi hivyo!"
"Sijabisha, Sarah. Ila ndivyo ambavyo nimekwambia kuhusu Sheng."
Kukawa kimya kidogo.
"Ole wako umwambie Kinoo haya n'lokwambia," Sasha akatahadhari.
**
Saa nne usiku ...
"Una uhakika?" Aliuliza Sheng akiongea na simu.
"Ndio, nina uhakika. Na mara hii sitataka pesa yako mpaka pale utakapohakikisha maneno yangu."
"Sawa. Tutawasiliana." Sheng akakata simu.
Baada ya kama lisaa limoja akawa na wajakazi wake kumi na mbili. Wakajiweka kwenye chombo cha usafiri na kwenda zao.
Wakanyookea eneo fulani mbele ya hoteli. Tutaita eneo hili hoteli ila haikuwa na hadhi hiyo, ila ilizidi hadhi ya guest house au lodge.
Hapo baada ya kukaa ndani ya gari kwa muda kidogo, wakatoka wanaume wanne na kuzama ndani ya hoteli.
Punde kidogo sauti za bunduki zikavuma! Wanaume wengine watatu wakatoka garini na kuzama ndani. Milio mingine ikavuma. Kisha kukawa kimya.
Sasa kwenye gari wakawa wamebakia wajakazi watatu tu pamoja na Sheng. Hawakuwa wanaelewa nini kinaendelea ndani. Na Sheng, kwa kuhisi kuna jambo halipo sawa, akawazuia watumishi wake wasiende tena ndani.
Wakangoja hapo kwa muda kidogo. Lakini katika hali ya ajabu, mara hoteli nzima ikazima taa na kuwa kiza!
Na mwanga uliporejea, Sheng akashuhudia watu wakiwa wamesimama mbele ya gari! Na watu hao walikuwa wamebebelea bunduki kubwa mikononi mwao, wakiwanyooshea!
"Shuka upesi garini!" Amri ikasikika. Sheng akatazamana na watumishi wake. Hakuwa tayari kutii amri ya yeyote. Basi wale wafanyakazi, katika namna ya kipekee, wakamziba Sheng, kisha mwanaume huyo wa kichina, akasukuma gia na kukanyaga mafuta kwa pupa!
Gari likamchupa kuwafuata wale watu waliowanyooshea bunduki. Na kabla watu wale hawajanusuru roho zao, wakagongwa na kusinywa!
Sheng akaangua kicheko. Na kama haitoshi, akarudisha tena gari na kuwasinya tena aliowagonga.
Kisha akashuka na kuwatazama. Usoni mwake alikuwa na tabasamu.
"Hakuna mtu wa kupambana na ..." kabla hajamalizia kauli yake hiyo, akakaukiwa na maneno ghafla baada ya kugundua aliowaua ni miongoni mwa wafanyakazi wake.
Lakini iliwezekanaje hili?
Hakujua kumbe wafanyakazi wake hao walikuwa wametolewa mhanga. Viunoni walikuwa wamefungiwa mabomu na hata bunduki walizokuwa wamebebelea hazikuwa na risasi hata moja.
Kabla hajafanya jambo, akashangaa kuona alama ya kitaa chekundu cha bunduki kikiwa kifuani mwake. Na kisha akaamriwa na mtu ambaye hakumwona,
"Weka mikono yako juu!"
***