Doctor Mama Amon
Platinum Member
- Mar 30, 2018
- 2,311
- 3,513
Andreas Schedler ni mwandishi wa kitabu kinachojadili mbinu mbalimbali za kuchakachua chaguzi za kidemokrasia.
Kitabu hicho kinaitwa "The Politics of Uncertainty: Sustaining and Subverting Electoral Authoritarianism." Tafsiri yangu ya jina hili ni “Siasa za Hofu: Kupanda na Kushuka kwa Udikteta Uliovaa Ngozi ya Demokrasia.”
Naambatanisha hapa nakala pepe ili ujisomee na kujifunza namna ya kujilinda. Lakini kabla hujajisomea, hebu pitia tahakiki yangu fupi ya kitabu hicho.
TAHAKIKI FUPI
Profesa Andreas aliandika kitabu hicho mwaka 2015, na kikachapishwa na kampuni ya Oxford University Press, kikiwa na kurasa zinazosomeka 493. Lengo la kitabu ni kueleza jinsi serikali za kidemokrasia zinavyoingia madakani kwa kutumia mbinu za kidikteta.
Kitabu kimegawanyika katika sehemu kuu nne. Kuna utangulizi, nadharia ya “siasa za hofu” inayoeleza matumizi ya mbinu za kidikteta kkwa siri ndani ya nchi za kidemokrasia, matumizi ya nadharia hii katika nchi mbalimbali duniani, na viambatanisho kadhaa.
Katika kitabu hiki Andreas anasema kwamba, bila kujali kwamba kuna mifumo ya kidemokrasia inayolindwa kisheria na kikatiba, serikali nyingi huchakachua mifumo ya kidemokrasia kutumia njia mbali mbali zisizoweza kuonekana kwa mtu ambaye hajavaa miwani ya nadharia inayomwezeaha kutambua ukatili huo.
Andreas anadai kwamba, watawala hawa wanaweza kuruhusu uchaguzi wa vyama vingi kuonekana kwamba unafanyika, lakini wakachakachua viwango vya uchaguzi huo, kwa kutumia ufundi mkubwa wa ujambazi wa kisiasa usioonekana kwa urahisi.
Anasema kuwa, serikali zote za kidemokrasia zinazoingia madarakani kwa kutumia mbinu za kiimla, husumbuliwa na matatizo ya aina mbili. Kwanza, kuna hofu ya usalama (“insecurity of the future”). Hofu hii inatokana na ukweli kwamba watawala huingia madarakani baada ya kuwakwaruza watu wengi wanaopishana nao njiani. Muda wote wanahisi watakuja kulipiza kisasi.
Pili, kuna hofu inayotokana na mashaka juu ya uwezo wao wa sasa wa kuwazuia wabaya wao wenye dhamira ya kuwaondoa madarakani. Mara zote wanajikuta hawana taarifa zinazotosheleza mahitaji yao ya kujua kama wako salama (“opacity of the present”).
Kwa sababu ya hofu hizi mbili, watawala huchukua hatua za kukabiliana na maadui wa kufikirika kwa kuchakachua mifumo ya kidemokrasia iliyopo katika kila hatua.
Katika msimu wa uchaguzi, Andreas anasema, hofu ya serikali hujitokeza katika ngazi mbili.
Katika ngazi ya kwanza, kuna hofu dhidi ya mashambulizi ya wapinzani yanayoweza kufanyika dhidi ya serikali kabla ya msimu wa uchaguzi kufika, yaani kwa “kuchezea kanuni za mchezo wa uchaguzi.”
Katika ngazi hii, serikali hujaribu kujitetea kwa kuwanyang’anya wapinzani madaraka kupitia mbinu mbalimbali zinazopindisha kanuni hizo.
Mbinu hizo hulenga kuchakachua angalau maeneo saba. Kuna bunge, mahakama, vyombo vya habari, asasi za kiraia, mfumo wa uchaguzi, mfumo wa vyama vya siasa, na mfumo wa ugatuzi wa madaraka.
Katika ngazi ya pili, kuna hofu dhidi ya mashambulizi ya wapinzani yanayoweza kufanyika dhidi ya serikali “ndani ya msimu wa uchaguzi.”
Katika ngazi hii, serikali hujaribu kujitetea kwa kuwanyang’anya wapinzani madaraka kupitia mbinu kadhaa. Kuna ushawishi wa hoja, ushawishi wa hisia, kuficha fomu za uteuzi wa mgombea, kukataa kufanya uteuzi wa mgombea, kumnyima mgombea fursa ya kufanya kampeni kwa kumsababishia usumbufu wa kila aina ikiwemo kumfunga, kutochapisha jina la mgombea aliyefanya kampeni kwa ufanisi hadi mwisho, na kukataa kutangaza wapinzani walioshinda.
Kwa mujibu wa nadharia ya Andreas, ushindi unaopatikana katika ngazi moja, unaweza kuponyoka katika ngazi ya pili. Ndio kusema kwamba, pamoja na kwamba, serikali inaweza kufanikiwa kuwabana wapinzani kabla ya uchaguzi, lakini msimu wa uchaguzi unaweza kufuta kabisa ushindi huo, kama wapinzani wakijipanga vizuri.
Andreas ametupatia mifano kutoka sehemu nyingi duniani kuthibitisha anayoyasema. Kama hivi ndivyo, hali ikoje hapa kwetu Tanzania, na tufanyeje?
Mama Amon,
Sumbawanga Kusini,
Toleo la: 07 Septemba 2020 @ 7.00 pm.