Maana ya shikamoo ni hii ambayo inatumika sasa na Waswahili, hiyo uliyoitoa haipo katika kamusi tunazotumia. Inawezekana ilikuwa inatumika zamani wakati wa utumwa, lakini lugha hubadilika, maneno hubadilika na halikadhalika maana za maneno nazo sio tuli.
Tanzania hakuna utumwa, huu ni mfumo wa maisha na hauwezi kuamuliwa na uwepo wa neno moja tu katika lugha nzima. Kung'amua uwepo wa utumwa ni lazima tuchunguze mifumo ya maisha ya Watanzania na sio kutazama neno moja kisha kuhitimisha.
Watu wazima huwa 'wanalilia' hiyo shikamoo kwa kuwa ndio utaratibu wa jamii kuwa salamu hii itatoka kwa mdogo kwenda kwa mkubwa. Kama ambavyo tu mtu huyu huyu mzima anavyolilia kupishwa siti kwenye daladala wakati haijaandikwa popote.
Baraza la Kiswahili la Taifa hutunga sera ya Lugha pamoja na kuishauri Serikali masuala mbalimbali yanayohusu lugha. Kiswahili hakishangazi, bali kina namna yake ya pekee ya kutazama salamu (Salamu kama kujuliana hali, na salamu kama ishara ya heshima). Wanaofahamu lugha ya kibantu yenye dhana hii pia wanaweza kuja kutufahamisha. Ukishangaa ya Kiswahili inabidi ushangae pia na Kifaransa ambapo majina yake huwa na jinsia (eti kuna gari la kike na la kiume... Inachekesha eeh?)
Kupendelea kutumia aina fulani ya salamu ni haki yako, lakini isije kukugharimu ukweni siku moja (natania tu).
Hoja yako umeiwasilisha vema, karibu sana.