Kama wewe ni mzaliwa wa juzi tu, usibishi wanachokueleza waliokuwepo wakati huo. Mimi mwenyewe nilikuwepo. Ngoja nikupashe japo kwa ufupi ilivyokuwa.
Hans Pope alikuwa Regional Police Commander wa Mkoa wa Ziwa Magharibi, ambao siku hizi unaitwa Mkoa wa Kagera. Intelijensia ilipata habari kwamba Idd Amin atashambulia Tanzania. Kwa hiyo Tanzania itume jeshi Bukoba kwa tahadhari. Kwa sababu ya vita baridi vilivyokuwa vikiendelea kati ya nchi za Magharibi na Mashariki, Nyerere alikataa kufanya hivyo kwa kuogopa kuambiwa anachochea vita.
Kweli Amin akashambulia, na kwa kuwa hakukuwa na jeshi upande wetu, polisi ndio wakajitokeza kupambana naye, wakiongozwa na RPC Hans Pope. Polisi wetu wakazidiwa nguvu na wanajeshi wa Amin. Hans Pope akauawa, na hapo ndipo Amin akasema Tanzania wanasaidiwa na Wachina, akitaja sura ya mchotara Hans Pope kama mfano. Sehemu ya Tanzania iliyopo upande wa pili wa Mto Kagera, akaiteka na kuvunja daraja walilokuwa wakivukia Watanzania wa pande mbili hizo za Mto Kagera. Amin akaomba aingizwe kwenye Guiness Book of Records kwamba ameteka sehemu ya nchi ndani ya dakika 15 tu. Nyerere alikaa kimya kwa siku tatu akisubiri matamko ya nchi zingine kulaani kitendo hicho cha Amin, na kila siku alikuwa anakwenda kanisani. Sana sana matamko yalitolewa na nchi za Magharibi ni kuiomba Tanzania 'to act with restraint'. Siku ya tatu, ndipo Nyerere akatumia uwezo wake mkubwa wa kuhamasisha. Akalihutubia Taifa kwa kusema kwamba joka limeingia nyumbani mwetu. Tuna kazi moja tu ya kulitoa nje. Sababu tunayo; nia tunayo; na uwezo tunao. Bahati nzuri Amin mwenyewe ametusaidia kwa kuutangazia ulimwengu kwamba ameteka sehemu ya nchi yetu. Hivyo, hakuna mtu wa kutulaumu kwamba tunaenda vitani. Hapo ndipo jeshi letu likaingia mzigoni. Wakawa wakipiga risasi kutoka upande wetu wa mto huku mainjinia wakilikarabati daraja, mpaka lilipotengemaa ya kutosha kuweza kupitisha silaha. Baada ya kuikomboa hiyo sehemu iliyokuwa imetekwa, ndipo Museveni akakazana na askari wake, akisaidiwa na jeshi letu, mpaka Kampala ilipotekwa na Amin kuikimbia nchi. Baada ya vita Nyerere akatangaza kubadili jina la mkoa kutoka Ziwa Magharibi kuwa Kagera. Mkoa wa Mara ulikuwa ukiitwa Ziwa Mashariki. Nao ukabadilishwa jina kuwa Mara.
Kwa hiyo, maelezo ya Askofu Bagonza ni ya kweli kabisa.