Nimemsikia Katibu Mwenezi na Itikadi wa CCM akimzungumzia Mzee Warioba. Kwanza, nitangaze mgogoro wa Maslahi. Nampenda huyu kijana. Huwa ni mnyenyekevu na msikivu. Haaniki madhaifu yake kama sisi wengine. Akisema jambo napenda kumsikiliza.
Anasema Mzee Warioba astaafu vizuri. Pia kwamba Mzee Warioba ana chuki na viongozi. Nimetafakari haya kuhusu maneno ya Kihongosi:
1. Mzee aliishastaafu. Si sehemu ya serikali hata kama ni mwanachama wa CCM. Mzee huyu ndiye mstaafu halisi na PEKEE. Wengine mbaodhani wamestaafu, bado hawajastaafu ndio maana wako kimya maana wanafungwa na kanuni ya uwajibikaji wa pamoja (Collective Responsibility).
2. Mzee Warioba hana CHUKI na viongozi. Anawapenda kama Baba wa Taifa alivyowapenda kina Ali Hassan Mwinyi, Horace Kolimba, John Malecela na Edward Lowasa. Kama raia na mstaafu wa kweli aliwaambia ukweli kwa upendo kuliko kujificha na kunung’unika pembeni. Mzee Warioba ana UPENDO mkubwa kwa viongozi walio zamu.
3. Badala yake, Mzee Warioba anaweza kuwa anachukiwa ama na viongozi au na CCM. Kwa kuwa msemaji wa chama kasema, ni sahihi kuamini kuwa ipo chuki mahali fulani. Imani ya 8 ya TANU na CCM inasema, “Nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko”. Mzee Warioba bila hofu wala aibu amesimamia UKWELI, HAKI na UWAZI. Kama kwa kufanya haya anastahili kulipwa maonyo haya, namshauri ayapokee bila kinyongo.
4. Vyama VYOTE vya siasa hapa nchini, ni vyama vya viongozi kuliko kuwa vyama vya wanachama. Mzee Warioba ni muumini aliyepitwa na wakati kwa kuamini vyama ni mali ya wanachama. Hata hivyo, kuna siku vyama VYOTE vitawajitaji akina Mzee Warioba wengi ili madhambi ya viongozi yabakie ni ya viongozi na yale ya serikali yasiwe madhambi ya vyama. Vyama viongoze, visiongozwe. Tafakari.
Nampongeza rafiki yangu Kenani lakini nahisi hoja hii ameishika kichwa chini na miguu juu. Akipenda amtembelee Mzee Warioba. Ajifunze na kumfundisha pia. Enzi zetu, tulipenda kumtembelea na kujifunza kujenga hoja. Angefufuka hayati Mohamed Seif Khatibu angekueleza.
Ila ninakupongeza, unajitahidi kujenga Hoja