R.B
JF-Expert Member
- May 10, 2012
- 6,296
- 2,575
Askofu Niwemgizi wa jimbo Katoriki jimbo kuu Rulenge amesema ataongoza kampeni ya kura ya hapana kupinga katiba mpya.
Askofu atangaza kufia katiba
• Ni Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki
• Aahidi kuhamasisha waumini waipigie kura ya hapana
NA JOSEPHAT ISANGO
WAKATI Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk. Alli Mohamed Shein, wakitarajiwa kukabidhiwa Katiba iliyopendekezwa na Bunge Maalumu la Katiba, Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC) ambaye pia ni Askofu wa Jimbo la Rulenge- Ngara, Mhashamu Severini Niwe Mugizi,amewataka Watanzania waikatae, na kwamba yupo tayari kufa kwa ajili ya kupigania katiba bora.
Askofu Niwe Mugizi amesema haungi mkono Katiba iliyopendekezwa kwa kuwa haina ukweli wala uadilifu. "Wao walibadili kanuni ili kupata yanayowapendeza. Mimi nawasihi kwa unyoofu, ingawa najua sasa suala la kudai katiba mpya ni kelele ambayo haitaisha, tuwe na upendo na nchi yetu na viongozi wetu, lakini pale wakifanya yasiyofaa tuwaambie ukweli bila woga. Niko tayari kufa kwa ajili ya kusema ukweli kwa sababu tumetangaziwa vita," alisema.
Akizungumza na mamia ya waumini wa Kanisa hilo kwenye Kituo cha Hija cha Katoke Jimbo la Rulenge-Ngara majuzi, Askofu huyo alisema kwa kuwa katiba hiyo imepitishwa kwa mabavu na hila, yeye hawezi kuhamasisha waumini wake waiunge mkono. Ameifananaisha katiba hiyo inayopendekezwa na nyumba iliyoezekwa kwa dhahabu lakini imejengwa kwenye msingi wa mchanga. "Haiwezi kudumu," alisema.
Aliwaeleza kuwa alishamwambia hata Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kwamba iwapo katiba mpya haitazingatia mambo ya msingi yaliyopendekezwa na Watanzania atawahamasisha waumini kupiga kura ya hapana "Naawambia kabisa, katiba ile ni wazi walipaswa kuboresha, na ndiyo ilikuwa kazi yao. Kweli kuna vitu wameboresha, kuna vitu wameongeza ongeza pale, lakini kuna vitu vya msingi sana wameviondoa. Mimi binafsi siafiki kabisa," alisema.
Alisema kwa mfano, katiba inayopendekezwa haitoi uthibitisho wa kulinda uhai wa kuishi tangu kutungwa mimba bali inasema kila mtu ana haki ya kuishi. "Siafiki siafiki hata kidogo. Watu walipendekeza vitu fulani viwepo kwenye katiba, mfano mgombea binafsi watakwambia wameweka kwenye katiba lakini ukiangalia masharti yaliyowekwa ni magumu kiasi kwamba mgombea binafsi hawezi kufaulu.
"Nasema, sitaki kurefusha, na wameshasikia hadi imefika mahali sisi maaskofu tukaitwa wapuuzi tuliofanya kazi isiyo na utukufu, lakini tuwaambie kuwa sisi hatukutumwa na wanasiasa kufanya kazi tunayofanya. Pale ambapo ukweli na uadilifu vinakosekana hatupaswi kukaa kimya. Mchakato wote wa katiba haukuwa na uadilifu na ukweli, ndiyo maana mimi siafiki," alisema.
Askofu huyo aliwashauri waumini kupiga kura wakiwa na dhamiri hai, huku akiwatahadharisha watakaopiga kura za ndiyo halafu mambo yakakwama siku za usoni wasilaumu kuwa askofu hakuwaambia.