Mwaka 2017 Askofu Severine Niwemugizi wa jimbo katoliki Rulenge alitoa ushauri kwa Rais Magufuli kuhusu mchakato wa katiba mpya.
Askofu alisema ni vizuri mchakato wa katiba mpya ukaendelea.
Siku chache baada ya kutamka hayo, Askofu alifuatwa na maofisa wa uhamiaji na kumtaka afike ofisini kujieleza. Maofisa walitilia shaka uraia wake na kwahiyo walitaka vithibitisho vya kuwa Severine Niwemuhizi ni raia wa Tanzania. Ifahamike kuwa Askofu Niwemugizi aliwahi kuwa Rais wa baraza la maaskofu katoliki (TEC) kuanzia mwaka 2000 hadi 2006 na baadae kuwa makamu wa Rais wa baraza hilo mwaka 2010 hadi 2015.
Baada ya wito wa maofisa wa uhamiaji, Askofu alitii amri bila shuruti. Alitakiwa kukabidhi hati ya kusafiria, kitambulisho cha kupiga kura na cheti cha kuzaliwa. Nyaraka zote hizo zilizuiwa na idara ya uhamiaji na kwahiyo Askofu hakuweza kusafiri wala kupiga kura (kama kungekuwa na uchaguzi).
Kwa mujibu wa Baba Askofu Severine Miwemugizi, alizaliwa tarehe 3 Juni 1956 katika kitongoji cha Kayanza, kijiji cha Kabukome, kata ya Nyarubungo, wilaya ya Biharamulo. Alibatizwa katika parokia ya Katoke, Biharamulo, akasoma shule ya msingi Katoke na baadae sekondari ya Nyakato, Bukoba. Safari yake ya utumishi ilianzia Seminari kuu ya Ntungamo, Bukoba kisha akaendelea Seminari ya Kipalapala huko Tabora.
Askofu Severine Niwemugizi alirudishiwa nyaraka zake mwaka 2020, siku chache kabla ya uchaguzi mkuu.
Kesho Ijumaa, Askofu Severine Niwemugizi ataongoza misa ya mazishi ya aliyekuwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano ya Tanzania, John Pombe Joseph Magufuli.