Baadhi ya Wanafunzi katika Chuo cha SAUT wapata wasiwasi baada ya matokeo yao kutopandishwa na Wahadhiri

Baadhi ya Wanafunzi katika Chuo cha SAUT wapata wasiwasi baada ya matokeo yao kutopandishwa na Wahadhiri

Joined
Aug 31, 2026
Posts
1
Reaction score
0
Kuna wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) Mwanza ambao wanakabiliwa na changamoto katika upandishaji wa matokeo yao ya Continuous Assessment (CA).

Wanafunzi hao wamefanya mitihani yote, majaribio pamoja na kazi mbalimbali walizopewa na wahadhiri katika masomo yao. Hata hivyo, hadi sasa baadhi yao hawajapandishiwa matokeo yao, hali ambayo imewaacha katika sintofahamu kuhusu hatima ya masomo yao.

Wanafunzi hao wamekuwa wakiwafuatilia wahadhiri wa masomo husika ili kupata ufafanuzi kuhusu matokeo yao. Kwa mujibu wa malalamiko yao, baadhi ya wahadhiri wamekuwa wakiwajibu kwa lugha isiyofaa kupitia ujumbe mfupi wa simu (SMS), na hata pale wanafunzi wanapokwenda ofisini kwa ajili ya kufuatilia suala hilo, hawapati majibu ya kuridhisha.

Hali hii imezua hofu na wasiwasi miongoni mwa wanafunzi, kwani baadhi yao wanahisi huenda kucheleweshwa au kutopandishwa kwa matokeo kunatumika kama njia ya kuwaweka katika mazingira ya kushawishiwa kutoa rushwa ya fedha au rushwa ya ngono ili matokeo yao yaweze kupandishwa.

Malalamiko haya yanaelezwa zaidi kuhusisha baadhi ya wahadhiri wanaofundisha Sheria, hususan katika mazingira yanayowahusu wanafunzi wanaokamilisha mwaka wao wa nne wa masomo.

Wanafunzi hao wanasema wana ushahidi wa mawasiliano mbalimbali, ikiwemo SMS na nyaraka nyingine, ambao wanaweza kuuwasilisha kwa mamlaka husika kwa ajili ya uchunguzi.

Kutokana na uzito wa suala hili, Serikali pamoja na mamlaka zinazohusika na usimamizi wa elimu ya juu zinapaswa kulifuatilia na kulichunguza suala hili kwa kina. Wazazi na walezi wanatumia fedha nyingi kugharamia elimu ya watoto wao, hivyo si haki mwanafunzi kuonekana hajafaulu au kuchelewa kuhitimu kutokana na kutopandishwa kwa matokeo ambayo anadai ameyapata kwa kufanya mitihani, majaribio na kazi zote alizopewa.

Ni muhimu uchunguzi wa haki na huru ufanyike ili kubaini ukweli, kuwawajibisha watakaobainika kukiuka taratibu, na kuhakikisha wanafunzi wanapata haki yao ya kielimu bila kulazimishwa kutoa fedha au kufanyiwa vitendo vya unyanyasaji wa aina yoyote.
 
Back
Top Bottom