SAKATA LA KILINDI NA MAUAJI YA KILINDI NA MAUAJI YA KIJIJI CHA MADINA - HANDENI, KUPOTEA (KUULIWA) KWA RAJAB OMARI MTANA
Rajab Omar Mtana alikuwa ni mwanakijiji wa kawaida tu akiishi kijijini Lulago, Handeni kama wanavijiji wengine wanavyoishi na alikuwa na biashara yake kuuza hiliki kama mkulima wa zao hilo.
Siku moja akaja mnunuzi mfanyabiashara ya hiliki nyumbani kwake kununua hiliki na akamuuzia.
Yule mfanyabiashara alipokuwa anatoka na gari yake akasimama kwenye kizuizi cha kulipia ushuru.
Alipotakiwa kulipa ushuru akasema kuwa si hiliki yote amenunua katika kijiji hicho kwa hiyo hawezi kulipa ushuru wa hiliki yote.
Hapo palitokea ubishi na mfanyabiashara yule akagonga lile geti na akaondoka.
Hii ikapelekea kwa wakusanyi ushuru kwenda nyumbani kwa Rajab Omar Mtana kumkamata na kumweka chini ya ulinzi katika ofisi ya serikali ya kijiji hadi hapoatakapolipa ushuru ambao yule mfanyabiashara alitakiwa alipe.
Ndugu zake Rajab Omar Mtana wakenda pale ofisini kwa nia ya kumtoa ndugu yao na hapo pakatokea vurugu na mapigano.
Katika mapigano hayo, mgambo ambae ndiye aliyekuwa akishughulika na kudai ushuru akauawa.
Kisa hiki cha ushuru wa hiliki ndicho kilichozua balaa kubwa la mauaji na uchomwaji moto nyumba za Waislam wa Madina na kuvunjwa kwa misikiti na vijiji ambavyo vilikuwana idadi kubwa ya wakazi wake Waislam.
Baada ya haya Mkuu wa Mkoa wa Tanga Chiku Galawa akatoa amri kuwa hapana ruhusa tena ya sehemu ile kuwa makazi kwakisingizio kuwa hizo ni kambi za ugaidi.
Huyu bibi alisema mengi ambayo takriban yote yamedhihirika kuwa hayana ukweli mathalan kuwa kuna Al Shabab, mahandaki ya vita, silaha za kutungulia ndege nk. nk.
Alizungumza na Radio Nuur, Tanga nami nilikwenda hadi Radio kuomba nipatiwe hayo mazungumzo yake lakini Radio Nuur waliogopa kunipa juu ya kuwaeleza kuwa Bi. Chiku kazungumza radioni kwa hiyo kazungumza na dunia nzima.
Hawakuthubutu kunipa lakini nilizungumza na watu waliomsikia.
Katika Waislam waliokamatwa na kufunguliwa mashtaka mahakamani Handeni ni huyu kijana Rajab Omari Mtana.
Baada ya kukaa rumande alipata dhamana yeye pamoja na wenzake na akawa nje.
Mwezi uliopita Rajab Omar Mtana alirejea kijijini kwake.
Wakati anakaribia kuingia kijijini alisimamishwa na askari wa kijiji akapekuliwa na akanyang'anywa simu yake na fedha taslimu.
Baada ya mkasa huu walimwachia na yeye akaendelea na safari yake.
Lakini nyumba yake ilikuwa imevurugwa haifai kuishi mtu kwa hiyo alifikia kwa dada yake.
Akiwa nyumbani kwa dada yake alifatwa na watu wa serikali ya kijiji usiku akatolewa ndani na kuanza kupigwa kwa bakora na kisha kwa mapanga.
Kujitetea kijana huyu alikimbia huku akifukuzwa.
Asubuhi kulipokucha palionekana damu nyingi sana.
Taarifa ilitolewa polisi lakini hakuna kilichofanyika.
Polisi walitoa taarifa (SON/RB346/2014) Dada yake na mumewe walikamatwa na kushitakiwa katika ''mahakama'' ya hapo kijiji na wakapigwa faini ya kila mtu shs. 20.000.
Kosa lao ni kumleta kijijini mtu asiyetakiwa.
Sasa ni mwezi mmoja Rajab Omar Mtana hajulikani alipo na inasadikiwa ameuawa na wale waliokuja kumtoa nyumbani kwa dada yake.
Ndugu yetu Rajab ametafutwa kote hadi leo hajapatikana na waliompiga na kumjeruhi wako huru nje hawajaguswa wala kuhojiwa na polisi.
Wakati Sheikh Chambuso alipokuwa akinihadithia mkasa huu ilinijia picha ya kisa cha vijana watatu waliouliwa na Klu Klux Klan Mississippi katika miaka wa 1960 wakati wa ubaguzi wa rangi Marekani.
Waliuliwa kama vile mtu kauwa paka msumbufu na hakuna lolote lililofanyika hadi zilipotiwa juhudi za ziada kutoka nje ya Mississippi ndipo wauaji wakatiwa mbaroni.
Mauaji ya Madina yamepita hivi hivi hakuna aliyesimamishwa mbele ya vyombo vya dola.
Uwezekano mkubwa ni kuwa na mauaji haya yatafata mkondo ule ule. Jambo la kusikitisha ni kuwa mauaji haya yamelenga watu wa dini moja.
Je, viongozi wetu wako hadhiri na mbegu hii wanayoiacha imee?
Rajab Omar Mtana alikuwa ni mwanakijiji wa kawaida tu akiishi kijijini Lulago, Handeni kama wanavijiji wengine wanavyoishi na alikuwa na bi...
mohamedsaidsalum.blogspot.com