Kama haijawa shared. Sina interest ni kupashana taarifa tu. Lakini kama kuna maswali ya kikanuni nitajaribu kujibu.
na Mwandishi Wetu
UAMUZI wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Samuel Sitta kujaribu kumaliza mzozo kati ya Mbunge wa Mkuranga, Adam Malima (CCM) na mfanyabiashara maarufu, Reginald Mengi, sasa umeingia hatua mpya inayoweza kukigharimu Chama Cha Mapinduzi.
Hali hiyo kwa kiwango kikubwa imesababishwa na uamuzi wa Malima ambaye ndiye aliyeanzisha mzozo huo, kumshitaki Sitta kwa Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, hatua ambayo tayari wachunguzi wa mambo wanaiona kuwa ni jitihada za kujaribu kumdhibiti Spika huyo wa Bunge.
Hatua hiyo ya Malima kuamua kuwakwepa Mwenyekiti wa Wabunge wa CCM, Edward Lowassa ambaye ni Waziri Mkuu na Katibu wa Wabunge wa CCM, Ali Ameir Mohammed, imeanza kutafsiriwa kuwa na lengo lililojificha la kumhujumu Sitta, ambaye mwenendo wake unaonekana dhahiri kuwakera baadhi ya vigogo ndani ya chama hicho tawala.
Aidha, uamuzi wa Malima kuamua kumshitaki Sitta nje ya utaratibu na kanuni za Bunge, nao umesababisha kuibuka kwa maswali mengi miongoni mwa wabunge, ambao baadhi yao wameshaanza kukiona kitendo hicho kuwa ni cha kulidhalilisha Bunge kimamlaka (Contempt of Parliament).
Wabunge kadhaa wa CCM na wale wa upinzani, waliozungumza na gazeti hili kwa wiki nzima sasa, wamekuwa wakieleza kushangazwa kwao na hatua hiyo ya Malima, ambayo wengi wao wanasema inatiwa nguvu ya kuwapo kwa shinikizo kutoka kwa kiongozi mmoja wa juu serikalini.
Tumeshangazwa na hatua hiyo ya Malima, ambayo kimsingi ni Contempt of Parliament na tunachokitarajia sasa ni kuona mbunge huyo akiitwa mbele ya Kamati ya Haki Maadili na Madaraka ya Bunge ili ahojiwe sababu za kufanya hivyo, alisema mmoja wa wabunge hao.
Wakati wabunge hao wakieleza kushangazwa na hatua hiyo, wanasema wamekuwa wakifuatilia kwa karibu maamuzi ya viongozi wakuu wawili, ambao ni sehemu ya Bunge, Rais Jakaya Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Taifa wa CCM na Lowassa kwa mamlaka yake ya uenyekiti wa wabunge wa CCM.
Baadhi ya wabunge waliozungumza na Tanzania Daima wamesema kwamba, kati ya viongozi hao wakuu wawili, Lowassa ndiye atakayetakiwa kuwa mwangalifu zaidi katika kulishughulikia suala hili, kutokana na jina lake kuwa miongoni mwa watu wanaotajwa kuwa sehemu ya jambo lililomfikisha Malima kuchukua hatua hiyo.
Kumbukumbu zinaonyesha kwamba, katikati ya mzozo kati ya Mengi na Malima, jina la Lowassa liliwahi kutajwa na Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo (CHADEMA).
Kutajwa kwa jina la Lowassa, kulikuja wakati shauri kati ya watu hao wawili lilipokuwa likishughulikiwa na Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.
Ndesamburo ambaye alikuwa mmoja wa wajumbe katika kamati hiyo, alitangaza kujitoa baada ya kudai kupata taarifa kutoka kwa Mengi zilizokuwa zikieleza kuwa, wajumbe takriban wote wa kamati hiyo ya Bunge walikuwa wamehongwa.
Mbunge huyo wa Moshi Mjini, ambaye alizungumza hayo mbele ya waandishi wa habari, alikaririwa akisema Mengi alikuwa amemweleza kuwa, taarifa za wana-kamati hao kuhongwa alikuwa amezipata kutoka kwa Lowassa.
Habari nyingine ambazo Tanzania Daima imezipata hivi karibuni kabisa kutoka miongoni mwa wabunge wengine zinaeleza kuwa, hatua ya sasa ya Malima imezusha mijadala mikali ya chini kwa chini kwa siku kadhaa sasa, ambayo baadhi ya mijadala hiyo inayataja majina ya viongozi wengine kadhaa kuhusika.
Mbunge mmoja kijana wa CCM aliyezungumza na Tanzania Daima kwa sharti la jina lake kutoandikwa gazetini, alisema tayari kundi la wabunge wengine wa chama hicho, wameshaanza kujiandaa kumlinda spika ambaye wanamwelezea kuwa mwanasiasa asiyewabagua wabunge.
Sisi tunajua kabisa kuwa kile ambacho Sitta alikieleza mapema kabisa kuwa atakuwa Spika wa Speed and Standard (Kasi na Viwango) kimekuwa ni kero kwa baadhi ya wana CCM ambao wanaiona hatua hiyo kuwa ni ya kujitafutia umaarufu na kwa kweli huo ndiyo msingi wa chuki dhidi yake, alisema mbunge huyo.
Mbunge huyo alisema tangu habari zilipoanza kusambazwa kuwa Malima alikuwa amewasilisha barua ya malalamiko kwa Makamba kuhusu mzozo wake na Mengi, wabunge kadhaa wa chama hicho wamekuwa wakikutana ili kuweka msimamo wa pamoja kuhusu jambo hilo.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, miongoni mwa maazimio waliyoyafikia ni kuhakikisha kuwa wanafanya kila linalowezekana kuhakikisha Bunge linaheshimiwa, na Spika anapata fursa ya kutimiza wajibu wake pasipo kutishwa na mtu yeyote.
Sisi tumeshawishika kuamini kuwa Sitta anaonewa na watu wenye malengo binafsi ya kumharibia kazi na wanaotaka apoteze uhuru wake wa kimamlaka wa kuliendesha Bunge pasipo kuingiliwa. Tumejipanga kumlinda kwa hali yoyote na kuwa tayari kuwaangusha wale wenye nia mbaya naye, alisema mbunge mwingine wa CCM anayetoka Kanda ya Ziwa.
Kundi la wabunge wa CCM linalojenga hoja za kuiua hoja hiyo ya Malima, limeorodhesha vifungu vya Katiba ya Jamhuri na kanuni za Bunge ambazo wanaamini kuwa wakizitumia, wataweza kuikwamisha ajenda ya siri ya Malima ya kummaliza Sitta kisiasa.
Habari kutoka ndani ya duru za wabunge wa CCM zinaeleza kuwa, moja ya vifungu walivyotumia ni sheria namba 3 ya mwaka 1988, iliyo katika Ibara ya 24 (D) ambayo inapinga kuhojiwa kwa mamlaka ya Spika na chombo kingine chochote nje ya Bunge.
Aidha wabunge hao wamepanga pia kutumia kanuni namba 60 ya Bunge iliyo katika toleo la mwaka 2004 ambayo pia inatoa mamlaka kwa maamuzi ya Bunge kutohojiwa na chombo kingine cha nje.
Walipoulizwa sababu hasa za kufikia hatua hiyo, wabunge hao walisema taarifa walizonazo zilikuwa zikionyesha kuundwa kwa mtandao mpya ndani ya mtandao wa wana CCM wenye lengo la kuhakikisha Sitta anawekwa katika mazingira magumu kabisa kikazi.
Wabunge hao ambao walifikia hatua ya kuwataja kwa majina baadhi ya viongozi wa CCM na serikali walio nyuma ya sakata zima la Mengi na Malima, walisema kumekuwa na mahusiano mabaya kikazi kati ya Sitta na baadhi ya viongozi serikalini.
Katika mazingira ya kutatanisha, tangu Ndesamburo atoe tuhuma nzito za rushwa ambazo sasa zimewasilishwa katika Taasisi ya Kupambana na Rushwa (Takuru) si Lowassa wala Mengi waliowahi kujitokeza hadharani kutoa kauli.
Hatua hiyo wakati fulani ilisababisha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kilazimike kumwandikia barua Waziri Mkuu, Lowassa kikimtaka atoe tamko kuhusu kuhusishwa kwenye tuhuma za rushwa kwa wajumbe wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge zilizotolewa na Ndesamburo.
Barua ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Wilbroad Slaa ya Januari 15, 2007, ilieleza kushangazwa na ukimya wa Lowassa pamoja na tuhuma hizo nzito zilizotolewa na Ndesamburo.
Jitihada za gazeti hili kuwasiliana ama na Lowassa mwenyewe au mwandishi wake wa habari, Said Nguba wakati huo ili kupata maoni yake kuhusu suala hili ziligonga ukuta.
Hata hivyo, ofisa mmoja wa juu serikalini, aliyezungumza na Tanzania Daima kwa sharti la kutotajwa jina, alisema Waziri Mkuu alikaririwa (wakati huo) akiyaelezea maneno hayo ya Ndesamburo kuwa yasiyo na ukweli wowote.
Alipotakiwa na Tanzania Daima aeleze hatua ambazo Lowassa amepanga kuzichukua dhidi ya suala hilo ambalo kauli yake inahusishwa, ofisa huyo alisema, vyombo vinavyohusika vitalishughulikia.
Sisi tunajua ni kwa nini Ndesamburo kasema maneno hayo. Tunajua kila kitu kinachoendelea kuhusu jambo hili. Ni vyema tukanyamaza. Waziri Mkuu anajua anachofanya, hawezi akasema maneno ya namna hiyo. Ipo siku ukweli utabainika, alisema ofisa huyo wa serikali alipotafutwa na Tanzania Daima.
Badala yake, ofisa huyo wa serikali alieleza pia kushangazwa kwake na ukimya wa Mengi ambaye ndiye aliyetajwa na Ndesamburo kumwambia maneno hayo, kuendelea kukaa kimya pasipo kutamka hadharani iwapo ni kweli alifikisha maneno hayo au la.
Ninyi mnamtafuta Waziri Mkuu atoe tamko, mbona hatujasikia Mengi akisema hadharani ni kweli kuwa alimwambia Ndesamburo maneno haya? Si yuko na anapatikana, mbona amekaa kimya, alihoji ofisa huyo.
Hata hivyo wakati wa kikao cha Bunge cha mwanzoni mwa mwaka huu, Sitta aliamua kulitolea uamuzi suala hilo kwa kufanya kile ambacho gazeti hili lilikielezea kuwa ni kushindwa kwake kumaliza mzozo kati ya Mengi na Malima.
Sitta akitumia falsafa yake ya siku zote; Hekima za Spika, alitangaza rasmi kuwaita ofisini kwake Dar es Salaam katika siku itakayopangwa, lengo likiwa ni kutafuta suluhu ya kudumu.
Na kwa kuwa, busara zangu zinanituma kwamba, njia nzuri na iliyo bora ya kuyashughulikia na kuyamaliza malalamiko ya watu hawa wawili, ni kwa usuluhishi (reconciliation) kati yao, alisema Sitta wakati akisoma maamuzi yake.
Sitta alisema, alikuwa amelazimika kufikia uamuzi huo, baada ya kubaini kuwa, watu hao wawili, kila mmoja alikuwa ametenda kosa la aina fulani, tangu sakata hilo liibuliwe na Malima mwezi Agosti mwaka jana.
Maamuzi hayo yalitokana na malalamiko ya Mengi, aliyowasilisha kwake (Spika) Agosti 6, mwaka jana, akilalamika kwamba, Agosti 2, 2006, wakati akichangia hoja ya Bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo Bungeni, Malima pamoja na mambo mengine, alishutumu matumizi mabaya ya Kituo cha Televisheni cha ITV pamoja na mmiliki wake ambaye ni Mengi.
Katika matamshi yake, Malima alikishutumu kituo hicho kwa kutumia muda mwingi kutangaza habari zinazomhusu mmiliki wake wakati kikitoa muda mchache kutangaza masuala ya kitaifa yanayowahusu Rais na Waziri Mkuu.
Kwa maneno yake, Malima alisema: Nimewahi kushuhudia Rais wa Jamhuri ya Muungano ana habari nzito kwenye Taarifa ya Habari ya saa 2:00, anapewa dakika moja na nusu, Waziri Mkuu anataka kuzungumzia njaa anapewa dakika moja na nusu. Watoto wa Primary wanakuja kutoka Zanzibar kutembelea Kiwanda cha Coca-Cola wanapewa dakika 10. Mmiliki wa TV anakwenda kuongea na watoto wa madrasa Msasani kwa ajili ya kugombana na sheikh mmoja anapewa dakika 10.
Mengi aliyachukulia matamshi hayo kuwa shutuma dhidi yake zilizotolewa katika eneo ambalo hawezi kujitetea, na kwamba shutuma hizo dhidi yake na ITV hazikuwa na ukweli wala msingi wowote.
Baada ya matamshi hayo ya Mengi yaliyotolewa na ITV na Radio One, Malima aliomba muongozo wa Spika kuhusu hatua stahili anazopaswa kuchukua yeye binafsi kama mbunge kuhusu matangazo ya IPP Media dhidi yake au hatua zinazoweza kuchukuliwa na Bunge, kwa niaba yake.
Baada ya kupitia hoja hizo kwa kulinganisha na sheria, taratibu na kanuni zilizopo, Sitta alibainisha kuwa, wote wawili walikuwa wametenda makosa.
Kwa upande wa Malima, Spika alisema kuwa, mbunge huyo alikuwa amelidanganya Bunge, kwani takwimu alizozitoa kuhusu taarifa za habari za ITV hazikuwa sahihi.
Maamuzi hayo ya Sitta, ndiyo yaliyosababisha Malima afikie hatua ya kuandika barua kwa Makamba akiyapinga.