Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
Nimeletewa barua ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kujiuzu kazi ya ualimu, aliyeniletea bila shaka akidhani siijui barua hii.
Nimeamua kumwandikia kumpa fikra zangu na kumweleza historia nzima ya barua hii ambayo inaitwa ''Uamuzi wa Busara.'':
''Hii barua ni maarufu ila kilichopungua ni vipi Mwalimu Nyerere alifikia katika uamuzi mgumu kama huu wa kuacha kazi na kuamua kuwa mtumishi wa TANU chama kichanga cha siasa kilichoasisiwa miezi minane tu iliyopita.
Chama ambacho kilikuwa kikiendeshwa kutoka fedha za wafadhili wake wanne: John Rupia, Waziri Dossa Aziz na ndugu wawili Abdulwahid na Ally Sykes.
Bahati mbaya barua aliyoandikiwa Mwalimu na mwajiri wake hapa haipo lakini nayo pia ni barua maarufu.
Toka alipochaguliwa kuwa Rais wa TAA tarehe 17 April 1953 mkakati uliokuwa umepangwa na Hamza Mwapachu na Abdul Sykes ilikuwa ni kuunda TANU na kudai uhuru wa Tanganyika.
Sasa haikutegemewa kuwa Rais wa TANU atadai uhuru wa Tanganyika akiwa mfanyakazi wa Kanisa.
Huu ulikuwa muhali mkubwa na hili viongozi wa TANU wakilijua na Abdul na Nyerere walishalizungumza kabla na ukweli ni kuwa kabla ya safari ya kwanza ya UNO Februari 1955, Nyerere alitaabika sana na fikra ya kuacha kazi.
Ujasiri wa kuacha kazi Mwalimu hakuupata kwa kule kuzingirwa na watu wenye uwezo hawa viongozi na wahisani wakubwa wa TANU.
Ujasiri wa kuacha kazi aliupata siku aliporudi UNO na akapokewa na umma ambao ulikuwa haujapatapo kuonekana Dar es Salaam.
Siku ile ndiyo Nyerere alitambua kuwa ana watu wanaomuunga mkono na wana mapenzi ya kweli na yeye na TANU na wanataka kuwa huru na wamemkubali yeye kama kiongozi wao.
Kwa upande wa serikali ya Gavana Edward Francis Twining walitanabai ule ukweli kuwa sasa siku zao Tanganyika zilikuwa zinahesabika.
Kwa upande wa mwajiri wa Mwalimu Nyerere, yaani Kanisa iliwadhihirikia kuwa mtumishi wao alikuwa amewasababishia mgongano mkubwa sana wa maslahi kwani Kanisa na Serikali walikuwa na ushirikiano mkubwa katika kuitawala Tanganyika.
Kubwa zaidi lililowashangaza ni kuwa ni ile jamii waliyokuwa wameinyima elimu kwa hila za ukoloni za wagawe uwatawale.
Waislam wameunda chama na kumweka kiongozi Mkatoliki aongoze mapambano ya kuikomboa Tanganyika.
Mkakati huu ulikuwa na maana gani?
Mwalimu alikuwa alama ya umoja na alama ya kuwaita walio mfano wa yeye kuingia TANU na kuunga mkono juhudi za kudai uhuru wa Waafrika wa Tanganyika.
Barua ile aliyoandikiwa Nyerere na mwajiri wake ilisomwa na Abdul Sykes mtu aliyekuwa karibu sana na Nyerere na Abdul alisisitiza kuwa Nyerere aache kazi lakini barua ile akapendekeza ijadiliwe na Halmashauri Kuu ya TANU chini ya Mwenyekiti Clement Mohamed Mtamila na ilikuwa nyumbani kwake Mtamila ndipo barua ile ilipojadiliwa na uamuzi ukawa Nyerere aandike barua ya kujiuzulu kazi.
Nyerere aliandika barua ya kujiuzulu na akaja mjini Dar es Salaam sio mwalimu wa shule tena na kwa muda akaishi nyumbani kwa Abdul Sykes Mtaa wa Aggrey na Sikukuu.
Katika Halmashauri Kuu ya TANU mmoja kati ya wajumbe wale alikuwa Tatu bint Mzee.
Yapo mengi sana katika historia ya TANU na historia ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambayo wengi hawayajui.
Picha ya kwanza juu ni barua ya Mwalimu Nyerere na picha ya pili hapo chini ni wa kwanza kulia ni Bi. Tatu bint Mzee akifuatiwa na Bi. Titi Mohamed na wa kwanza kushoto ni Bi. Chiku bint Said Kisusa wakimsindikiza Julius Nyerere Uwanja wa Ndege safari ya kwanza UNO.