Na Sammy AwamiBBC News, Dar es Salaam
Haki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Rais wa Tanzania John Magufuli amekuwa akikosolewa kwa mashambulizi yake ya mara kwa mara dhidi ya "mabeberu" na tangazo lake la hivi karibuni kuwa maombi na sala vimeondosha virusi vya corona katika taifa hilo.
Lakini suala hilo la kukosolewa huenda lisimsumbue kwa kuwa katika kipindi chake cha miaka mitano ya urais, amekuwa akijipambanua kama mzalendo wa kiafrika na mcha Mungu ambaye yupo kwenye mapambano dhidi ya mataifa ya magharibi ambayo yanataka kupora rasilimali za taifa hilo la Afrika Mashariki.
"Nataka watanzania mjue kuwa mna rais jiwe kweli. Siwezi tishwa na sitishiki," bwana Magufuli alisema Machi 2018.
Magufuli ana matumaini kuwa kazi yake inajieleza na itamsaidia kushinda uchaguzi ujao mwezi Oktoba na kurejea madarakani kwa muhula wa pili.
captionBwana Magufuli amekosoa sana wawekezaji wa nchi za magharibi na China
Moja ya mpambano mkubwa wa rais Magufuli ilikuwa dhidi ya kampuni kubwa ya madini ya Barrick Gold Corp ya nchini Canada.
Alitaka serikali ichukue udhibiti wa 60% katika migodi mitatu ya kampuni hiyo ili kukomesha "unyonywaji" wa rasilimali za Tanzania.
Magufuli mwenye miaka 60 sasa alianzisha majadiliano na Barrick ambayo yalionekana kama mzozo wa ng'ombe na sungura, na ijapokuwa serikali yake ilikubali kuchukua 16% ya hisa, mazungumzo hayo yalitosha kupeleka ujumbe kuwa mambo hayakuwa kama zamani nchini humo.
Akataa mradi wa 'mwendawazimu' na China
Baada ya kuingiwa makubaliano mapya baina ya Barrick na serikali mwezi Januari bosi wa kampuni hiyo Mark Bristow alisema mbele ya rais Magufuli kuwa: " Kilichofanyika hapa ni changamoto kwa sekta ya madini na kwetu sote kuanza safari ambayo tutapata pamoja ama kukosa pamoja."
Akiongea katika hafla hiyo, rais Magufuli hakuonesha tu upande wake wa kizalendo bali ucha Mungu, na kusema: " Namshukuru Mungu kwa mafanikio ya makubaliano haya."
captionBwana Magufuli amehamasisha maombi ya pamoja wakati wa janga la corona
Rais Magufuli pia amesitisha miradi miwili mikubwa baina ya nchi yake na China: ujenzi wa reli ya kisasa ya umeme ya kati na ujenzi wa bandari kubwa ziadi Afrika Mashariki katika eneo la Bagamoyo kwa gharama za dola bilioni 10.
Magufuli alisema ni "mwendawazimu" tu ndiye angekubali masharti ya mradi huo ambayo yaliingiwa na serikali ya mtangulizi wake Jakaya Kikwete ili kujenga bandari hiyo.
Magufuli pia amekuwa akilaumu ubinafsi wa viongozi na kushindwa kutanguliza maslahi ya taifa kama chanzo cha nchi hiyo kutopiga hatua kubwa kimaendeleo.
Lakini ni mataifa ya magharibi ambayo rais Magufuli amekuwa akiyatilia mashaka zaidi, na amekuwa akiwatuhumu "vibaraka" wa mataifa hayo ndani ya nchi yake - ambao ni mchanganyiko wa wanasiasa wa upinzani, watetezi wa haki za binadamu na waandishi wakosoaji - kwa kupigania maslahi ya "mabeberu".