Mara nyingi ukitembea mitaa ya uswahilini, utakuta wananchi wameanika unga na katikati ya mkeka walioanikia unga wameweka kipande kikubwa cha mkaa.
Misukule chakula chao kikuu ni pumba au unga uliochanganywa na maji, mara chache hulishwa nyama za watu endapo mmoja wao atafariki, nyama yake hukatwakatwa na kulishwa misukule. Kwa kawaida misukule hufungiwa ndani wakati wa mchana, na usiku ndio hufunguliwa kwenda kufanya kazi mashambani, viwandani, ujambazi, ulozi nk. Kuna nyakati wenye misukule hukosa chakula cha kuwalishia misukule, hivyo huachiwa mchana kuingia mitaani kujitafutia chakula. Wanapokuwa mitaani wakikuta unga umeanikwa, wanaushambulia kwa kuchota na kula. Moja ya mafundisho wanayopewa ni kuwa wakiona kitu chochote cheusi, wasikisogelee na kama wanaona kinakuja upande waliopo wanatakiwa waondoke mara moja katika eneo hilo.
Ukiona unga na mikaa imewekwa juu yake mitaani kwako, jua kuwa eneo hilo ni maskani ya wachawi wa nchi, na kama unaishi maisha ya hovyo hovyo, hakika wewe ni msukule mtarajiwa.