Bariadi,
Ahsante kwa link ya Bibi Titi.
Nimeisoma lakini kwa kweli hamna kitu mle ndani.
Hivi ndivyo nilivyoanza utangulizi kwa kitabu changu kuhusu Bibi Titi Mohamed (1926-2000):
''Ni vigumu kusema ni lini nimekuja kumfahamu Bi. Titi Mohamed. Nimefumbua macho nikikuwa
katika mitaa ya Dar es Salaam ya miaka ya 1950 na 1960 nikimuona na kumfahamu kuwa huyu
ndiye Bi. Titi. Mwanamke shupavu na kiongozi wa TANU.
Haikunipitikia kwa wakati ule nikiwa bado kijana mdogo wakati mwingine nikimuona katika mikutano
ya TANU pale Mnazi Mmoja au Jangwani kuwa ipo siku nitakaa nitafiti historia ya mashujaa wa uhuru
wa Tanganyika na Bi. Titi awe mmoja wa mashujaa wangu ambao nilataka sana kuandika maisha yao.
Siku moja tu kabla ya kifo cha Bi. Titi nilikuwa nikihojiwa na mwanafunzi wa kike wa Kitaliana kutoka
Chuo Kikuu cha Napoli, Italia ambae alikuwa akifanya utafiti kuhusu nafasi ya wanawake katika harakati
za kudai uhuru wa Tanganyika.
Binti huyu alikuwa alinihoji kuhusu Bi. Titi na akataka kujua kwa nini hatajiki katika historia ya TANU na
kwa nini wanawake wenzake aliokuwa nao katika harakati za kudai uhuru wanaonekana kutopenda
kueleza habari za Bi. Titi.
Nilimfahamisha binti yule kuwa sisi Watanzania tuna historia rasmi ya uhuru wa Tanzania ambayo
tunatakiwa kuienzi. Historia hiyo inaanza na Mwalimu Nyerere na kuishia na Mwalimu Nyerere.
Historia hiyo imewatoa wazalendo wengi katika historia pamoja na Bi. Titi. Binti huyo alikuwa na
masikitikokuwa wakati alipofanya mipango ya kutaka kwenda kumuhoji Bi. Titi akamkuta mgonjwa
kwa hiyo hakuweza kufanya mahojiano.
Nilimfahamisha mtafiti huyu yale niliyokuwa nayajua kuhusu Bi. Titi kisha tukaagana. Siku ya pili
nikapata habari kuwa Bi. Titi amefariki.
Kama alivyokuwa akisema mwenyewe marehemu, ‘Yote kuhusu mimi yameshaandikwa nyie waandishi
wa leo mtaandika nini ?'
Ni kweli Bi. Titi kaandikwa sana lakini waliomuandika hawakummaliza, kwa kuwa hawakummaliza ndiyo
maana na mimi nimepata nguvu ya kuweza kumuandika lau kama kwa muhtasari. Kwa hakika wengi wa
waandishi hao walikuwa wageni ; na wale waandishi wazalendo walipomwandika Bi. Titi walimwandika
kwa mtazamo wa agenda zao na vilevile bila kuwa na ujuzi wa historia ya Dar es Salaam katika miaka
ya 1950.
Wageni walimtazama Bi. Titi kwa jicho la ugeni mimi nataka kumwandika Bi. Titi kama alivyokwenda na
historia ya kudai uhuru. Nataka kumueleza Bi. Titi tokea mwanzo alipokuwa na Mwalimu Nyerere.
Nyerere akibandua hatua yake unyayo wa Bi. Titi unafuatia.
Nataka kumuandika Bi. Titi jinsi alivyopanda kutoka msichana mdogo wa Ki-Dar es Salaam akiwa na
miaka 26 hadi kufikia umaarufu mkubwa kabisa. Kisha ghafla nyota yake ikachujuka akaanguka na
akaishia kufungwa kifungo cha maisha kwa kosa la uhaini ambalo hadi kufa kwake alikana kuhusika.
Nataka kumuandika Bi. Titi jinsi alivyotoka kifungoni akiwa fukara mali yake yote imepotea na jinsi
alivyoyakabili maisha ya upweke na kutengwa. Nataka kumuandika Bi. Titi jinsi kwa ufundi mkubwa
na subra ya hali ya juu alivyomtegemea Mungu kama nilivyopata kumsikia akisema na Mungu akaitika
dua zake na kamrudishia siyo mali zake tu bali hata na hadhi yake.
Mtaa aliopewa kwa heshima yake ambao alinyang'anywa ukaja kurudishwa jina lake. Na wale waliomfanyia
khiyana ile wakiwa wa hai na hawana uwezo wa kufanya lolote.
Vipi Bi. Titi akaja kuuguzwa na kuzikwa na walewale watu waliolitangazia taifa kuwa alikuwa msaliti na
ta'azia zao baada ya kifo chake zikajaa maneno ya kumsifu. Ilikuwaje ikawa hivyo?
Nikiwa mtu mzima nilifanyiwa mihadi ya kuzungumza na Bi. Titi katika ya miaka ya 1990 nyumbani kwake
Upanga. Baada ya kusalimiana na kuniuliza nilikotoka nilimfahamisha wazazi wangu. Nilishangaa kuwa
alikuwa anamfahamu baba yangu vizuri sana hata akanieleza wajihi na umbo lake.
Nilimfahamisha kuwa nilikuwa nataka kuandika maisha yake. Bi. Titi akanikatalia kwa njia ya kistaarabu
kabisa. Kwa hekima kubwa sana aliweza kunitoa katika mazungumzo ya harakati za siasa za kudai uhuru
na akaelekeza fikra zangu katika senema ya watoto
Cinderella niliyokuta akitizama pamoja na wajukuu
zake.
Kwa wale ambao walikuwa karibu na Bi. Titi watakuwa wanajua jinsi alivyokuwa fasaha wa kuzungumza
na jinsi alivyokuwa hodari wa kushinikiza hoja zake. Niliishia kunywa soda na kutazama ile senema katika
TV kisha tukaagana.
Lakini kwangu mimi nilikuwa nimefarajika sana. Miaka michache iliyopita rafiki yangu mmoja alikuwa anamuoa
binti ya ndugu yake Bi. Titi na harusi hii ilifanyika nyumbani kwa Bi. Titi Temeke. Hali niliyomkutanayo pale
Upanga ilikuwa tofauti sana na nilivyomuona Upanga mara tu alivyotoka kifungoni.
Kabla sijaondola Bi. Titi alinifahamisha kuwa hazina yake ya nyaraka za wakati wa kudai uhuru pamoja na picha
zake nyingi za kihistoria zilichukuliwa na askari wapelelezi wakati walipokuja kufanya upekuzi katika nyumba yake
kwa ajili ya tuhuma za kupindua serikali zilizokuwa zimemkabili katika miaka ya 1970.
Nilisikitishwa na hili kwa kuwa nilijua yeyote atakaekuja kuandika habari za Bi. Titi atakuwa amekosa zana za
kumsaidia kumwandika mama huyu kwa usahihi.''