RUFAA YA MGOMBEA WA CHADEMA KUPINGA
UAMUZI WA MSIMAMIZI. RUFAA HII IMETUPILIWA MBALI NA KIKAO CHA TUME KILICHOKUWA KIMEKAA GEITA. NIKIIPATA MAELEZO YA TUME NITAYAWEKA
MAELEZO YA RUFAA DHIDI YA UTEUZI WA MGOMBEA UBUNGE OSCAR RWEGASIRA MUKASA(CCM) YENYE KUPINGA UAMUZI WA MSIMAMIZI WA UCHAGUZI JIMBO LA BIHARAMULO MAGHARIBI YA KUTUPILIA MBALI PINGAMIZI LANGU DHIDI YA MTAJWA HAPO JUU
I. MGOMBEA OSCAR MUKASA SI RAIA WA TANZANIA
SABABU ZA MAAMUZI YA MSIMAMIZI
Sababu za msimamizi kukubaliana na utetezi wa Oscar Mukasa kuhusu uraia wake ni:
a) KWAMBA Amewasilisha maelezo kuwa baba yake amezaliwa kijiji cha Byamtemba kata ya Nsunga(Bila kuwasilisha kielelezo/ushahidi wowote)
b) KWAMBA Baba yake amekuwa mfanyakazi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania(kwa kuwasilisha kiambatanisho C; barua ya Tuzo ya kustaafu)
c) KWAMBA Ameambatanisha cheti chake(Oscar Mukasa) cha kuzaliwa Bukoba Mjini(Kielelezo A)
d) KWAMBA Ameambatanisha pasi yake(Oscar Mukasa) ya kusafiria(kielelezo E)
e) KWAMBA mtu anayetoa hoja anawajibika kuthibitisha ukweli wa hoja na kwamba hakuna vielelezo vyovyote vilivyotolewa(na mleta pingamizi) kuthibitisha hoja hiyo
SABABU ZA RUFAA YANGU KWA TUME DHIDI YA MAAMUZI YA MSIMAMIZI
Nakata rufaa dhidi ya maamuzi hayo ya msimamizi kwa sababu zifuatazo ambazo naomba Tume ya uchaguzi izizingatie kila moja kwa uzito wake:
1) Oscar Mukasa(muwekewa pingamizi) hajawasilisha ushahidi, wala kielelezo chochote kuwa baba yake amezaliwa katika kijiji cha Byamtemba kata ya Nsunga. Aidha hakuna kielelezo chochote ambacho Oscar Mukasa amewasilisha kuthibitisha kuwa Mama yake Apollonia Kokuterekeza si mganda. Hivyo msimamizi hakupaswa kuyakubali maelezo hayo yasiyokuwa na ushahidi wowote; hivyo:
i) Tume ya uchaguzi izingatie kwamba wazazi wake Oscar Mukasa walihamia kijiji cha Byantemba kata ya Nsunga mwaka 1971; hivyo wasingeweza kuzaliwa mahali ambapo walikuwa hawajahamia bado kama Oscar Mukasa alivyoeleza katika utetezi wake
ii) Tume izingatie kuwa katika maelezo yangu nilieleza kuwa kabla ya kufika Nsunga walianzia Bunyoro(Uganda), wakapita kakoki na Kakuto. Inafahamika pia kuwa walifika Nsunga wakitokea eneo la Minziro. Niko tayari kuleta mashahidi na ushahidi wao katika kikao cha rufaa na Tume.
iii) Tume izingatie kuwa baba yake na mama yake Oscar Mukasa si watanzania.
2) Baba yake(Oscar Mukasa) kufanya kazi serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hakuthibitishi wazazi wake kuwa raia wa Tanzania kwa kuwa:
i) Tume izingatie kuwa hakuna kielelezo chochote kilichowasilishwa kuthibitisha kuwa baba yake alikuwa mtumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia mwaka 1960 kama Oscar Mukasa(mwekewa Pingamizi) alivyoeleza kwenye maelezo yake(Kiambatanisho C alichowasilisha hakitaji mwaka alioanza kazi wala mwaka aliokuja Tanzania)
ii) Tume izingatie kwamba kuwa mtumishi wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania si ushahidi wa kielelezo cha kuwa raia wa Tanzania. Kwa kuwa wakati huo na hata sasa wako watumishi wa serikali ambao si raia wa Tanzania. Aidha, hakuna mahali katika Tuzo ya kustaafu aliyowasilisha kama ushahidi(Kielelezo C) ambapo pametajwa kuwa Baba yake(Oscar Mukasa) alikuwa raia wa Tanzania.
iii) Tume izingatie kwamba barua ya Tuzo ya kustaafu(Kielelezo C) si nyaraka ya ushahidi wa kuzaliwa. Nyaraka zinazothibitisha kuzaliwa ni cheti cha kuzaliwa, hati ya kiapo cha kuzaliwa(affidavit) na maelezo yaliyotolewa kwa kiapo kwa sababu hiyo. Hivyo, msimamizi wa uchaguzi hakupaswa kabisa kuchukulia barua hiyo kama ushahidi wa kuwa baba yake Oscar Mukasa ni Tanzania.
3) Oscar Mukasa kuambatanisha cheti chake cha kuzaliwa Bukoba Mjini(Kielelezo A) hakuthibitishi uraia wa Oscar Mukasa ambaye amezaliwa na wazazi wasiokuwa watanzania:
i) Tume izingatie kuwa Sheria ya Uraia ya mwaka 1995 imeweka wazi kwamba mtu ambaye amezaliwa na wazazi ambao wote wawili si watanzania; si mtanzania. Na akitaka kuwa mtanzania anawajibika kuwasilisha maombi rasmi(Kifungu cha 5(1)(2)(a) na 6). Hata kama mmoja wa wazazi wake angekuwa mtanzania bado angelazimika alipofikisha miaka 18 kutangaza kuwa raia wa Tanzania(Kifungu cha 7(1) na 7(4)(b) na 9).
ii) Tume izingatie mtiririko na hukumu ya kesi ya Amani Kaborou dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali na Msimamizi wa Uchaguzi ya mwaka 1996. Kesi hiyo iliamulia mahakama ya rufaa, chini ya jopo la majaji Nyalali(aliyekuwa jaji mkuu), Kisanga na Mfalila Ikumbukwe kuwa kesi hii ilihusu uraia wa aliyekuwa mgombea ubunge wa CCM Kigoma Mjini Azim Premji. Hoja katika kesi hii zinaweza kutumika katika suala la uraia wa Oscar Mukasa ambaye alizaliwa mwaka 1970 ambapo sheria ya mwaka 1961 ilikuwa ikitumika kabla ya kutungwa kwa sheria ya uraia ya mwaka 1995.(Rejea Tanzania Law Report 1996 Ukurasa wa 156 na kuendelea)
4) Oscar Mukasa kuambatanisha pasi yake ya kusafiria si ushahidi wa mwisho wa kuwa raia wa Tanzania; kwa kuwa wazazi wake si watanzania; hivyo:
i) Tume izingatie kwamba pasi ya kusafiria hutolewa kutokana na na taarifa za kuzaliwa ambazo muombaji huwasilisha. Hivyo zinapotolewa taarifa potofu(misrepresentation) hati ya kusafiria hutokea zikatolewa kimakosa kwa raia wa nchi nyingine kama ilivyotokea kwa Oscar Mukasa.
ii) Tume irejee mifano ya kutangazwa kutokuwa watanzania kwa raia wa nchi nyingine ambao walikuwa na pasi za kusafiria za Tanzania(Mf. Balozi Amani Bandora, Madlin Castico, Jenerali Ulimwengu na Abrahaman Kinana).
5) Hoja yangu niliyoitoa nimeithibitisha ukweli wake kwa maelezo ya kina yanayohusisha matukio ambayo yamefahamika kuwa yametokea na watu ambao wanajulikana; hivyo:
i) Tume izingatie kwamba Oscar Mukasa(muwekewa pingamizi), ndiye mwenye wajibu wa kuwasilisha vielelezo na ushahidi kuwa wazazi wake na yeye ni raia wa Tanzania.
ii) Tume izingatie kwamba fomu na. 9B, ya pingamizi dhidi ya uteuzi wa wagombea ubunge imeelekeza kuwa maelezo ya ziada yanaweza kuambatanishwa. Katika pingamizi dhidi ya Oscar Mukasa niliambatanisha maelezo ya nyongeza kama ilivyohitajiwa. Msimamizi alipaswa kunitaka kuleta vielelezo vya ziada kama angehitaji badala ya kufanya maamuzi bila kuzingatia kikamilifu maelezo niliyowasilisha.
6) Msimamizi wa uchaguzi amekubali ushahidi uliodokezwa na vielelezo kutajwa bila nakala ya vielelezo vyenyewe kuwepo:
i) Tume izingatie kwamba maamuzi yalifanyika bila vielelezo vifuatavyo vilivyotajwa kuwepo- Taarifa ya uhamiaji kutoka Afisa Uhamiaji wa Mkoa wa Kagera(Kielelezo B) na Kivuli cha Taarifa ya ndoa ya wazazi wa Oscar Mukasa(Kielelezo D)
ii) Tume izingatie kwamba pamoja na vielelezo hivyo kutokuwepo, maudhui na maelezo yake msimamizi wa uchaguzi ameyatumia kufanya maamuzi.
iii) Tume izingatie kwamba Oscar Mukasa(muwekewa pingamizi) amekiri kwa maandishi yake kuwa vielelezo B na D havipo vinafuatiliwa; msimamizi wa uchaguzi hakupaswa kuukubali ushahidi ambao haupo kwenye kumbukumbu. Hivyo, tume ibatilishe maamuzi ya msimamizi wa uchaguzi yaliyofanywa bila vielelezo.
iv) Tume isivikubali vielelezo hivyo, hata kama vikiletwa katika hatua ya baadaye kwa kuwa havikuwepo wakati maamuzi ya msimamizi yanafanyika. Kwenye rufaa hapawezi kuwa na uwasilishaji upya wa ushahidi ambao haukuwepo wakati maamuzi ya awali yanafikiwa.
v) Tume isivikubali vielelezo B na D kwa sababu KUFUATILIWA kwa vielelezo husika inaweza kuhusisha kughushi ama kuandaa vielelezo ambayo havikuwepo
vi) Tume izingatie kwamba taarifa ya ndoa ya wazazi wa Oscar Mukasa(Kielelezo D)- ndoa inaweza kufungwa popote na raia wa nchi yoyote na cheti cha ndoa hakiwezi kutumika kuthibitisha uraia wa mtu.
vii) Taarifa ya Afisa Uhamiaji wa Mkoa wa Kagera(Kielelezo B) si nyaraka inayoweza kutumiwa kama kielelezo cha kuthibitisha kuzaliwa kwa wazazi wa Oscar wala uraia wao na wa mtoto wao.kwani kuna uwezekano mkubwa wa raia wa Nchi nyingine kuingia katika Nchi nyingine kwa njia zisizo halali na kuendelea kuishi bila idara ya uhamiaji kuwa na taarifa za mtu huyo.
Katika rufaa yangu naomba;
a) Tume ikubaliane nami kuwa sababu nilizozieleza zinathibitisha bila ya shaka kwamba wazazi wa Oscar si raia wa Tanzania na hivyo Oscar Mukasa si raia wa Tanzania
b) Tume ibatilishe maamuzi ya msimamizi wa uchaguzi ya kutipilia mbali pingamizi langu kwamba Oscar Mukasa si raia.
c) Tume itengue uteuzi wa Oscar Mukasa kuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Biharamulo Magharibi kwa kuwa si raia wa Tanzania.
d) Pamoja na nusura yoyote ambayo Tume itaona inasitahili kutolewa dhidi ya Oscar Mukasa na msimamizi wa uchaguzi.Jimbo la Biharamulo Magharibi.
II. HANA SIFA ZA KUWA MGOMBEA UBUNGE
SABABU ZA MAAMUZI YA MSIMAMIZI WA UCHAGUZI
Sababu za msimamizi wa uchaguzi kukubaliana na utetezi wa Oscar Mukasa(muwekewa pingamizi) kuhusu kutokuwa kwake na sifa za kugombea ubunge ni:
a) KWAMBA,Mahali alipozaliwa muweka pingamizi panajieleza wazi kuwa ni Bukoba
b) KWAMBA,Katika fomu zilizowasilishwa kwake(msimamizi wa uchaguzi) zimejazwa mji wa BUKOBA isipokuwa fomu moja ambayo mgombea huyo(Oscar Mukasa) alifuta maneno yote yasiyohusika na mahali alipozaliwa na kuacha neno MJI.
c) KWAMBA,Maelezo yaliyotolewa na muwekewa pingamizi(Oscar Mukasa) katika kikao cha chama chake(CCM) hayakuthibitishwa kwa kuwa hakuna ushahidi uliotolewa.
SABABU ZA RUFAA YANGU KWA TUME DHIDI YA MAAMUZI YA MSIMAMIZI WA UCHAGUZI
Nakata rufaa juu ya maamuzi hayo ya msimamizi kwa sababu zifuatazo ambazo naomba tume ya uchaguzi izizingatie kila moja kwa uzito wake:
1) Lengo la sehemu B ya maelezo binafsi ya mgombea katika fomu ni kupata maelezo yenye kuweza kumtambulisha kikamilifu mgombea. Kifungu 3 na cha 4 katika sehemu hiyo, kila kimoja pekee na kwa ujumla wake vinapaswa kumtambulisha kwa ukamilifu mgombea. Hata hivyo, maelezo ya mahali alipozaliwa Oscar Mukasa(muwekewa pingamizi) hayajitoshelezi wala kujieleza kwa uwazi:
i) Tume izingatie kuwa katika fomu yake no. 8B ya uteuzi ukurasa wa nne, sehemu B ya maelezo binafsi- amejaza kipengele cha 3- neno BUKOBA na kipengele cha 4- cha kujaza halmashauri ya jiji/manispaa/mji/wilaya- HAKUJAZA CHOCHOTE wala KUKATA CHOCHOTE. Hivyo, fomu hiyo haieleweki, haijakamilika, wala haijitoshelezi kumtambulisha kikamilifu mahali alipozaliwa. Kwa ujumla, vipengele husika na fomu yenyewe haitoi maelezo kamili ya mgombea ubunge Oscar Mukasa.
ii) Tume izingatie kwamba kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi ya mwaka 1985 kifungu cha 40(1)(a) na (c) sababu za pingamizi na mgombea kuenguliwa ni pamoja na maelezo kutojitosheleza kumtambulisha mgombea na mgombea kutoa maelezo ambayo yanamfanya aenguliwe.
2) Oscar Mukasa(Muwekewa Pingamizi) na Msimamizi wa Uchaguzi; wote wamekiri na kukubaliana na maelezo ya kwenye pingamizi langu kwamba fomu ya uteuzi iliyobadikwa haikuwa imekamilika kutokana na kutojazwa kipengele cha 4:
i) Tume izingatie kwamba fomu ya uteuzi ni ile iliyopokelewa na kupitiwa na msimamizi wa uchaguzi na kubandikwa hadharani. Fomu hiyo, ndiyo fomu rasmi ya uteuzi wa Oscar Mukasa.
ii) Tume izingatie kwamba fomu hii ya uteuzi ndio iliyotazamwa na kusomwa na umma wa wapiga kura wa Biharamulo Magharibi na ndiyo rejea ya wagombea kuweka pingamizi. Tume isizingatie nakala za fomu ambazo zilikuwa kwenye kabati ama mikononi mwa mtu mmoja mmoja kwa kuwa hazikuwekwa hadharani, hazijaonwa na wagombea wengine wala hakukuwa na fursa ya kuweka mapingamizi kwa kutumia fomu hizo.
iii) Tume izingatie kwamba fomu ya Oscar Mukasa haikukamilika kwa kutokuwa na maelezo yote yanayohitajika
iv) Tume ibatilishe uamuzi wa msimamizi wa uchaguzi wa kukubaliana na utetezi wa Oscar Mukasa kwamba makosa kwenye fomu moja hayawezi kutengua mgombea kwa sababu makosa hayo ni makosa katika fomu rasmi ya uteuzi.
v) Tume isikubali fomu isiyokamilika kwani kufanya hivyo itakuwa ni kuliruka pingamizi(pre emptying) nililoweka.ikumbukwe kwamba mamlaka ya Tume yanayotolewa kwa mujibu wa sheria ya kuweza kupokea fomu za mgombea ambazo hazijakamilika yanatumika pale tuu mgombea husika anapokuwa ameiomba Tume kufanya hivyoa kabla ya uteuzi Oscara Mukasa hakuiomba Tume kuwasilisha fomu ambazo hazijakamilika kabla ya uteuzi.( Tume irejee maamuzi juu ya Rufaa ya Sambwee Shitambala, Uchaguzi wa Marudio Mbeya Vijijini; 2009).
3) Fomu ya uteuzi ambayo ilibadikwa hadharani kwenye sehemu B, kipengele cha nne; haikukatwa neno lolote kati ya halmashauri ya jiji/manispaa/mji na wilaya kama ambavyo Oscar Mukasa(muwekewa pingamizi) ameeleza katika utetezi wake:
i) Tume izingatie kwamba maelezo ya kwamba maneno yasiyohusika yalikatwa na kubaki neno MJI hayana ukweli
ii) Tume izingatie kwamba niko tayari kuleta mashahidi na ushahidi kama itahitajika kuhusu suala hili
iii) Tume izingatie kuwa maelezo hayo pia si utetezi wa kutojaza Kipengele cha nne, ambacho kilipaswa kujazwa tena kwa herufi kubwa badala ya kukatwa pekee.
iv) Tume izingatie kuwa Kipengele cha 3 na cha 4, katika sehemu B ya maelezo ya mgombea kila kimoja kinasomwa pekee na kina ulazima wake. Hivyo, kubaki sehemu ya mji katika kifungu cha nne, na kutokujaza jina la mji katika kipengele hicho hakupaswi kuhalalishwa kwa kuunganisha na kipengele cha tatu.
v) Tume izingatie kwamba Kipengele cha 4 kwenye fomu kinalengo la kumtaka mgombea abainishe jina la Halimashauri alikozaliwa ,hivyo basi kwa kuacha bila kujaza inamfanya Oscar Mukasa asiweze kutambulika kuwa amezaliwa Halimashauri gani ,na hivyo maelezo yake kutokutosha kumtambulisha kikamilifu.
4) Msimamizi wa uchaguzi hakupaswa kuukubali utetezi wa Oscar Mukasa(muwekewa pingamizi) na kufanya maamuzi kwa kuzingatia fomu nyingine badala ya fomu ya uteuzi ambayo ilibandikwa hadharani.:
i) Tume izingatie kuwa fomu ya uteuzi pamoja na nakala zake zilijazwa na mtu mmoja ambaye ni Oscar Mukasa na kukaguliwa na Msimamizi wa Uchaguzi na waliridhika kuwa zimekamilika na nakala nyingine zinafanana na fomu ya uteuzi.
ii) Tume izingatie kuwa Kitendo cha Msimamizi kudai kuwa nakala za fomu ya uteuzi zilizo kwenye kabati lake na nakala ya Oscar Mukasa zimejazwa tofauti na fomu ya uteuzi inaashiria kuwa Msimamizi wa Uchaguzi na Oscar Mukasa wameshirikiana kughushi nakala za fomu.jambo ambalo kisheria ni kosa la jinai.
iii) Tume izingatie kwamba kwa mujibu wa maelekezo na mada kwa wasimamizi wa uchaguzi na wawakilishi wa vyama vya siasa kipengele cha 7 kinachohusu taratibu za uteuzi(Uk. 4 na 5) ni wajibu wa msimamizi wa uchaguzi kuhakikisha kuwa fomu zimejazwa kikamilifu. Msimamizi anapitia fomu, na kufanya uteuzi kwa kuidhinisha na kubandika fomu ya uteuzi hadharani. Hivyo, msimamizi hakupaswa kuhalalisha kufanya uteuzi wa mgombea ambaye fomu yake haijakamilika.
iv) Tume izingatie kwamba inapaswa kufanya maamuzi kwa kurejea fomu ya uteuzi iliyobandikwa hadharani na maelezo ya kukiri kwa Oscar Mukasa(muwekewa pingamizi) na Msimamizi wa uchaguzi kwamba fomu hiyo haijakamilika kujazwa. na hivyo fomu hiyo si kamili.
5) Msimamizi hakuwa sahihi kuamua kwamba maelezo yaliyotolewa na muwekewa pingamizi(Oscar Mukasa) katika kikao cha chama chake(CCM) hayakuthibitishwa kwa kuwa hakuna ushahidi uliotolewa, na kwamba mrufani hawezi kuwa amesikia maelezo hayo kwa kuwa hakuwepo katika kikao husika:
i) Tume izingatie kuwa kwa mujibu wa maelekezo ya kwenye fomu 9B ya pingamizi, nilipaswa kuwasilisha maelezo ya nyongeza na nilifanya hivyo kwa kueleza ushahidi wa maneno aliyoyasema, mahali alipoyasema na tarehe ambayo aliyasema. Hivyo msimamizi hakuwa sahihi kuamua kuwa hakuna ushahidi uliowasilishwa ikizingatiwa kuwa maelezo ni sehemu ya ushahidi unaotambulika kisheria.
ii) Tume izingatie kuwa msimamizi alipaswa kuitisha ushahidi wa vielelezo kama angehitaji kabla ya kufanya maamuzi ya kukubaliana na utetezi wa maelezo matupu yaliyotolewa na Oscar Mukasa(muwekewa pingamizi)
iii) Tume izingatie kwamba katika kikao cha CCM cha tarehe 24 Mei 2009 cha kura za maoni, Oscar Mukasa alijieleza kuwa amezaliwa wilaya ya BIHARAMULO huku katika fomu yake ya uteuzi amejaza Neno BUKOBA. Utofauti huu wa maelezo kuhusu mahali alipozaliwa na ushahidi wa utata wa mahali alipozaliwa. Tume itambue kwamba hata katika mkutano wake wa kampeni Biharamulo mjini wa tarehe 10/06/2009 katika uwanja wa stendi, Oscar Mukasa wakati akielezea historia yake na ya wazazi wake hakueleza kabisa yeye na wazazi wake wamezaliwa wapi.
iv) Tume izingatie kwamba msimamizi wa uchaguzi hakupaswa kukubaliana na utetezi wa Oscar Mukasa(muwekewa pingamizi) kwamba nisingeweza kufahamu alivyojieleza ndani ya kikao cha CCM kwa kuwa sikuwepo na mimi si mwanachama wa CCM kwa kuwa; upo uwezekano wa taarifa ndani ya vikao vya CCM kupatikana lakini pia mkutano husika ulirekodiwa kwenye mkanda wa video na kurushwa katika kituo cha runinga(Biharamulo Cable Television) tarehe 25, 26 na 27. Hivyo, maelezo yake kwenye mkutano huo yamesikika si tu na mimi bali wapiga kura wote waliotazama televisheni siku hizo.
Katika muktadha huo, Katika rufaa yangu naomba;
a) Tume ikubaliane nami kuwa sababu nilizoeleza zinathibitisha bila ya shaka kwamba fomu ya uteuzi ya Oscar Mukasa(muwekewe pingamizi) haikujazwa kwa ukamilifu, sio fomu kamili
b) Tume ikubaliane nami kuwa sababu nilizoeleza zinathibitisha bila ya shaka kwamba maelezo yaliyotolewa kwenye fomu ya uteuzi ya Oscar Mukasa(muwekewe pingamizi) hayajitoshelezi kumtambulisha kama mgombea ubunge.
c) Tume ikubaliane na pingamizi langu kwamba Oscar Mukasa(muwekewa pingamizi) hana sifa za mgombea Ubunge kutokana na mapungufu katika fomu yake ya uteuzi.
d) Tume ibatilishe maamuzi ya msimamizi wa uchaguzi ya kutipilia mbali pingamizi langu kwamba Oscar Mukasa hana sifa za kugombea ubunge.
e) Tume itengue uteuzi wa Oscar Mukasa kuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Biharamulo Magharibi kwa kuwa hana sifa za kugombea ubunge.
f) Tume ichukue hatua dhidi ya msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Biharamulo Magharibi kwa kitendo chake cha kushirikiana na Oscar Mukasa kubadilisha nakala ya fomu ya uteuzi ili kudanganya umma kuwa fomu ilijazwa kwa usahihi.
g) Pamoja na nusura yoyote ambayo Tume itaona inasitahili kutolewa dhidi ya Oscar Mukasa na msimamizi wa uchaguzi.Jimbo la Biharamulo Magharibi.