Kupitia Mtandao wa X, Askofu Mwamakula amesema Kuna taarifa kuwa aliyekuwa Meya wa Ubungo, Boniface Jacob amenyakuliwa na defenda akiwa kikaoni Sinza, Dar es Salaam na haijulikani kapelekwa wapi. Sisi Askofu Mwamakula tunatoa wito kama ni Polisi wamemchukua waseme maana huyo ni kiongozi wa jamii hawezi kunyakuliwa kama mwizi.
Wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikisema kada wake aliyekuwa meya wa zamani wa Ubungo, Boniface Jacob 'Boni Yai' amekamatwa na Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi wa Kinondoni, Mtatiro Kitwinkwi amesema hana taarifa.
Akizungumza na Mwananchi kamanda Kitwinkwi kuhusu sakata hilo amesema: “Hapana, sina taarifa.”
Taarifa za Jacob kukamatwa, zimeanza kusambaa mitandaoni dakika chache zilizopita leo Jumatano, Septemba 18, 2024 na kwamba amekamatiwa Sinza, jijini Dar es Salaam.
Mwananchi limemtafuta, Wakili wa Chadema, Hekima Mwasipu ambaye amesema yupo njiani kuelekea Kituo cha Polisi cha Osterbay.
“Ni kweli amekamatwa na polisi waliovalia sare na wengine wamevalia kiraia maeneo ya Sinza. Walikuwa na defender na tuna taarifa kuwa amepelekwa Osterbay polisi na mimi niko njiani nakwenda.”