VIDEO - Tanzania Yabugizwa 5-1 na Brazil, Maximo Apigwa Chini
Mwarami Mohamed kipa wa Tanzania akiwa amekaa chini baada ya kutunguliwa na Wabrazili Monday, June 07, 2010 8:10 PM
Mpira umeisha na matokeo ni ya kusikitisha, Tanzania ambayo jana ilifungwa 1-0 na Rwanda leo imepokea kipigo kingine cha nguvu toka kwa Brazili kwa kubamizwa 5-1. Wakati huo huo kibarua cha Maximo kimeota mbawa na sasa nafasi yake itachukuliwa na kocha toka Denmark. Tanzania imeshindwa kutamba mbele ya Brazili na kukubali kubamizwa mabao 5-1 kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.
Kutokana na viingilio vikubwa, uwanja haukujaa kama ulivyotarajiwa na bila shaka TFF itakuwa kwenye mahesabu makali ya kurudisha pesa zao walizotumia kuwaleta Brazili.
Kocha wa Brazili, Dunga aliingiza kikosi chake kamili cha wachezaji 11 akikosekana kipa wake namba moja Julio Cesar ambaye aliumia mgongo katika mechi na Zimbabwe ambayo Zimbabwe ilifungwa 3-0.
Tanzania ikicheza mbele ya rais Jakaya Kikwete ilionyesha mchezo mzuri na kujaribu kuwamudu Wabrazili lakini makosa madogo madogo na udhaifu wa kipa Mwarami Mohamed ndiyo yaliyopelekea Tanzania kubugizwa magoli mengi.
Mshambuliaji hatari wa Brazili, Robinho aliifungia Brazili magoli mawili wakati Kaka naye baada ya takribani mwaka mzima akiwa na ukame wa magoli katika timu ya taifa, alifanikiwa kuzingisha nyavu za Tanzania.
Kiungo wa Brazili, Ramires aliyeingia uwanjani kipindi cha pili, aliifungia Brazili magoli kuhitimisha karamu ya magoli ya Brazili.
Goli la Tanzania lilifungwa na Jabir Aziz kwenye dakika ya 87. Jabir alienda hewani na kuunganisha kwa kicha mpira wa kona na kumuacha kipa wa Brazili, Gomes akigaragara huku mpira ukitinga nyavuni.
Pamoja na kufungwa na Brazili, Tanzania imekuwa ndio nchi ya kwanza kuchafua rekodi ya Brazili ya mechi sita bila nyavu zake kutingishwa. Timu ya mwisho kuzamisha mpira kwenye nyavu za Brazili ilikuwa ni Bolivia mnamo oktoba mwaka 2009.
Wakati huo huo TFF imemtema kocha wa Tanzania, Marcio Maximo ambaye nafasi yake sasa itachukuliwa na kocha toka Denmark, Jan Borge Poulsen mwenye umri wa miaka 64.
Poulsen ameingia mkataba wa miaka miwili na ataanza kuinoa rasmi Taifa Stars kuanzia mwezi wa nane.
Kama ungependa kujikumbusha matukio muhimu ya mechi na magoli yote sita katika mechi hii, basi angalia VIDEO hii chini.
VIDEO - Tanzania 1-5 Brazili Bonyeza hapa kuiona Video
NIFAHAMISHE Tanzania news portal .: Habari za Tanzania :.