Breaking news: ndege yatua na tumbo Kilimanjaro airport

Breaking news: ndege yatua na tumbo Kilimanjaro airport

Ndege iliyotajwa kuwa Embraer 125, yenye usajili 5H-HLL, imetua kwa dharura katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) leo, Oktoba 4, 2026, baada ya kuripotiwa kupata hitilafu kwenye mfumo wa magurudumu ya kutua.

Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) imethibitisha kutokea kwa tukio hilo, huku taarifa za awali zikieleza kuwa ndege hiyo ilikuwa ikitokea Seronera ikiwa na abiria 26.

Kwa mujibu wa taarifa za awali kutoka kwa mashahidi na watu waliokuwa karibu na shughuli za uendeshaji wa uwanja, ndege hiyo iliripotiwa kugonga mnyama aina ya pundamilia, hali inayodaiwa kusababisha hitilafu kwenye gurudumu la kutua upande wa kushoto.

Ndege hiyo ilifika KIA majira ya saa 5 asubuhi, ambapo rubani aliwasiliana na mnara wa uwanja na kuomba msaada wa kuthibitisha iwapo magurudumu ya kutua yalikuwa yameshuka kikamilifu.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, ndege ilifanya upitaji wa chini ili kuruhusu wahudumu wa mnara na marubani wa ndege nyingine waliokuwa ardhini kukagua hali ya mfumo wa magurudumu.

Baada ya kuthibitishwa kuwa mfumo wa magurudumu ulikuwa katika hali iliyowezesha kutua, ndege iliruhusiwa kuendelea na zoezi hilo huku vikosi vya zimamoto na uokoaji vikiwa tayari katika eneo la uwanja.

Wakati wa kutua, rubani alitua kwa tahadhari kubwa, ambapo gurudumu la upande wa kushoto, ambalo lilikuwa limehusishwa na hitilafu hiyo, lilitenguka wakati wa kutua na kusababisha ndege kuburuza uvungu kwenye njia ya kutua.

Abiria wote 26 na wafanyakazi 04 waliokuwa ndani ya ndege hiyo walifanikiwa kushuka salama na hakuna taarifa za majeraha zilizoripotiwa.

Tukio hilo limeanza kuchunguzwa na Tanzania Civil Air Accident Investigation Branch (TCAAIB) ili kubaini chanzo halisi cha hitilafu na mazingira yaliyosababisha tukio hilo.

Taarifa zaidi kuhusu chanzo cha tukio na matokeo ya uchunguzi zitatolewa na mamlaka husika baada ya uchunguzi kukamilika.
1791137827198.jpg
 
Hii Ndege ndogo ya EM120 imetua kiwanjani hapo saa tano na dk 50 asubuhi, na kuondolewa saa kumi na dk 16 jioni na kusababisha kiwanja kifungwa kwa muda......Sasa tatizo kama hilo likitokea kwa ndege kubwa kama B787, B777 au 747 si itachukua siku kadhaa?...Yale mazoezi ya dharula ambayo hufanyika mara kwa mara ni kichaka tu cha kura mapesa...Kiwanja KIA kinapaswa kuwa na runway za zaidi ya moja ili kuepukana na changamoto kama hizi.
 
Back
Top Bottom