HOJA TANZU ZA LAZARO NYALANDU; MAJIBU DHAIFU YATOKAYO; MSTARI MWEKUNDU WA CCM...
CCM sasa katika matukio yote mfuatano ya kisiasa wanaishi katika tamathali ya "KATA PUA UUNGE WAJIHI".., wahenga wanaposema 'kata pua uunge wajihi' ni sawa na kutoa mnofu wa pua na kuunga kwenye sehemu nyingine ya uso iliyoharibika ili ionekane nzuri. Kwa maana nyingine, ni kutoa au kupunguza kitu mahali na kwenda kufidia pengine. Dhana ya methali hiyo ni kulinda heshima yako hata kama itakugharimu..
Tuachane na hilo (wahenga wanamiliki mengi kwenye ndimi zao)..., tuelekee kwenye kujadili hoja ya msingi...
Katika bandiko langu la 31-10-2017 saa 13:17 ambalo nilijaribu kufafanua uimara na umadhubuti wa hoja za Lazaro Nyalandu, nikauliza maswali tanzu na mwisho nikatoa ushauri kwa taasisi ya kisiasa ya CCM kuhusu namna ya kushughulika na hojaji za Lazaro Nyalandu .., bahati sana nakutana na dhambi ya kusigina hoja za Nyalandu kwa kuchepuka. Huku ni kukosa uwezo wa kujibu hoja.
Wameshindwa kushambulia hoja za Lazaro Nyalandu za kujiondoa CCM na kuachana na nyadhifa zake zote ikiwa ni sambamba na ubunge wake. watu wasiopenda alichokifanya Nyalandu wanashambulia nafsi ya Nyalandu na sio kushambulia hoja tanzu alizotoa Lazaro Nyalandu.. Kuna tofauti hapo.., Bado kuna eneo kubwa Nyalandu anaendelea kuwa 'mbabe' katika hojaji zake.. Hazijashambuliwa kinagaubaga.
Hadi sasa CCM kama taasisi wamemjibu Lazaro Nyalandu kwa kutumia HOJA LEMAVU (hoja ambazo kwa kuzitazama juu-juu) huonekana zenye mashiko lakini ndani yake ni pumba, hazina mashiko. Na wafuasi wa CCM wao wamejibu hoja za Nyalandu kwa kutumia HOJA MFUNGAMANO., hoja hizi hujengwa kwa misingi jumuisho...
DHANA YA HOJA;
HOJA; hujengwa katika misingi ya kauli imara zenye kueleweka na kimsingi kauli ni sentensi. Sentensi zinazojenga hoja ni zile zibebazo fikra zinazoweza kuwa za kweli au si za kweli. Sio kila sentensi inaweza kutumika kujenga hoja..
KUFIKIRI KIMANTIKI; ni kufikiri kwa kutumia tamathali na kutoa hoja. Ni pamoja na kutafuta ukweli/ushahidi uliodhahiri wa kuthibitisha ukweli au kuonesha uongo wa jambo husika.
MANTIKI; ni utaratibu mzuri wa kufikiri. Ni fani ya elimu inayojishughulisha na utoaji wa hoja. Na kwa kuwa kutoa hoja ni kufikiri, tunaweza kusema kuwa mantiki ni taaluma inayojihusisha na kufikiria juu ya kufikiri.
KUTOA HOJA: Kutoa hoja ni kutumia ukweli unaojulikana ili kuthibisha ukweli mwingine au kuonesha uongo wa jambo. Kwa mantiki nyingine, kutoa hoja ni kutafuta ushahidi uliodhahiri wa kuthibitisha ukweli au kuonesha uongo wa jambo.
MAJIBU YA CCM YANAACHA ALAMA ZA USHINDI WA NYALANDU
Mara baada ya Lazaro Nyalandu kutangaza kuachana na siasa za CCM na kuomba kujiunga na CHADEMA, katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole aliibuka na kauli ya CCM na kumshambulia Nyalandu na kuacha kushambulia HOJA na sababu zilizotolewa na Nyalandu.. Simshangai sana Polepole kwa sababu ndio uwezo wake, amefika kwenye kilinge cha mwisho katika kufikiri..
Humphrey Polepole anasema CCM imeondokewa na watu wazito ns bado ipo salama hivyo Nyalandu sio kati ya hao wazito ni mwanachama wa kawaida. Polepole anasema kwamba kasi ya serikali ya awamu ya tano ndio msingi wa Nyalandu kukimbia CCM... Na kisha wanasema Nyalandu ni mwanasiasa asiekuwa na ushawishi ndani na nje ya chama... Sasa tujadili hojaji za CCM...
CCM wanasahau haraka sana; haijapita hata miaka 3 tangu mwenyekiti wa CCM apande jukwaani Singida na kumnadi Lazaro Nyalandu (3-10-2015) leo wanakuja na matoleo ya kashfa, uchafu wa Lazaro Nyalandu.. Wanataka wananchi waamini porojo..., siku mgombea wa CCM anamnadi, hatukufahamu uchafu wake!?
Kwamba huyu Lazaro Nyalandu huyu ambae alichukua fomu ya kugombea urais ndani ya CCM.., alipita salama kwenye kamati ya maadili, Kamati kuu hadi NEC pasipo na kuandikiwa au kutajwa kwa uchafu au ufisadi wake, isipokuwa leo ndio watu wa CCM wametambua hayo... Siasa uchwara.., tafsiri ya HOJA LEMAVU.
Leo mnataka kusema Lazaro Nyalandu ni mwanasiasa mwenye bahati. Mmesahau ni mbunge tangu 2000. Sitaki kuamini kwamba katika vipindi vyote vinne vya uchaguzi, Lazaro Nyalandu alikuwa anapigiwa kura za bahati. Labda sasa mteuleze, nani kati yenu hapigiwi hizi kura za bahati.
Kwamba Lazaro Nyalandu ni mwanasiasa asiekuwa na msisimko; sasa tuulizane sambamba, huyu mwanasiasa asiekuwa na "msisimko" kwanini anasababisha vilio na mijadala mikubwa hivyo kutoka upande aliohama!? Kwanini CCM wanaumizwa kuondoka kwa mwanasiasa asiekuwa na msisimko!? Dhana ya HOJA MFUNGAMANO.
Kwamba CCM wanakujankwa umma na taarifa za kutunga kwamba Nyalandu alikuwa kwenye hatua za kuchukuliwa hatua za kinidhamu kutokana na mwenendo wake na kauli zake za hivi karibuni.. Hii ni tafsiri ya CCM kupoteza mwelekeo.., kama maamuzi yalikuwepo, kwanini Nyalandu alikuwa hajachukuliwa hatua? Vikao vilivyomvua uanachama ni vipi, tujulishwe..
Lazaro Nyalandu amekuwa waziri katika serikali, amekuwa mbunge kwa vipindi 4 tofauti, amekuwa mjumbe wa NEC, amekuwa mwenyekiti wa UVCCM mkoa, Ujumbe wa kamati ya siasa ya wilaya, ujumbe wa wabunge wote CCM.., hivyo kama uko timamu hauwezi kusema Nyalandu ni mwanasiasa asiekuwa na ushawishi.., labda kama ushawishi ni kuunga mkono hoja..
SPIKA WA BUNGE NA MKANGANYIKO WA WAZI;
Awali Lazaro Nyalandu alithibitisha kwamba amejiuzuru nafasi zake zote za uongozi ndani ya CCM na bungeni..., na akasema ameandika barua kumjulisha Spika wa bunge kuhusu hatua zake hizo..., spika anasema hajapokea barua hiyo.. Inashangaza.
Bahati mbaya sana hata Spika wa bunge hatambui kuhusu katiba ya JMT ibara ya 71(1)(f) kwamba "ukikosa sifa za kuwa mwanachama wa chama cha siasa unapoteza sifa za kuwa mbunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania"..., kwamba Spika wa bunge hatambui hilo? Kwamba anataka kuona barua ya katibu mkuu wa CCM kuthibitisha kwamba Nyalandu sio mwanachama wa CCM tena!?
Basically, Lazaro Nyalandu alitangaza kujiondoa CCM kabla ya chama hicho kupeleka barua kwa Spika ya kumvua uanachama, hivyo automatically NYALANDU kwa kujiondoa kwake CCM alikuwa sio tena mbunge maana sio mwanachama wa CCM, hata pasipo kuwajibika kuandika barua kwa Spika wa bunge, huyu sio mbunge tena... Hata hii dhana ndogo Spika wa bunge ameshindwa kuitumia?
Taarifa ya bunge kwa umma ina tofautiana na kauli ya Nyalandu kwa umma na hata kauli ya awali ya CCM kwa umma. CCM walisema Nyalandu kajiuzuru kwa kushindwa na kasi, Nyalandu mwenyewe alisema kajiuzuru na sababu kadhaa lakini bunge linasema Nyalandu amevuliwa uanachama na CCM. Bunge limetoa taarifa yenye ukakasi zaidi hadi sasa..,
HOJA ZA NYALANDU ZIPATE KUJIBIWA.., TUSIKWEPESHE CHEPE;
Lazaro Nyalandu ametoa sababu zake kadhaa za kwanini ameamua kuachana na CCM.., nilifikiri sasa huu ni wakati wa CCM ambayo imetuhumiwa kupoteza mwelekeo kumpa majibu sahihi Nyalandu... Sio kutuletea porojo.., tunawashangaa sasa...
¶ Kutoridhishwa na mwenendo wa hali ya kisiasa nchini, ikiwa pamoja na ukiukwaji wa haki za binadamu,
¶ Ongezeko la vitendo vya dhuluma wanavyofanyiwa watanzania wenzake.
¶ Kutokuwepo kwa mipaka ya wazi kati ya MHIMILI ya dola (serikali, bunge na mahakama)
¶ Kukosekana uhuru katika utendaji kazi wa bunge kuisimamia serikali kwa mujibu wa KATIBA.
¶ Mchakato wa katiba mpya kuhodhiwa na kufichwa na CCM kwa maslahi binafsi ya chama hicho. Na hakuna uhitaji wa katiba mpya.
¶ Hakuna namna MHIMILI ya dola inaweza isiingiliane na kujitegemea ikiwa hakuna katiba mpya itakayoainisha mipaka na ukomo wa wazi kwa MHIMILI ya Dola.
¶ CCM Imepoteza Mwelekeo wake wa kuisimamia serikali kama ilivyo kuwa awali. Kuisimamia katika nyanja ya Kisiasa, kiuongozi, kiuchumi.
¶ CCM imekuwa chini ya miguu ya DOLA badala ya chama kushika hatamu na kuikosoa serikali inapobidi kama mwalimu Nyerere alivyotaka.
CCM acheni porojo, jaribu kupambana na hoja za Nyalandu na sio Nyalandu kutokuwa MWANACHAMA, PIA Bunge lisiendelee kuufanya umma uamini hoja za Nyalandu kwamba limehodhiwa na Serikali..
____________________________
[emoji767] Martin Maranja Masese (MMM), 02—11—2017