Hotoba ya Waziri wa fedha kuhusu matumizi na mapato ya serikali mwaka 2020/2021
======
Mwenendo wa Mapato
Katika bajeti ya mwaka 2019/20, Serikali ilitarajia kukusanya jumla ya shilingi trilioni 33.11 kutoka katika vyanzo vyote vya ndani na nje ambapo hadi Aprili 2020 kiasi cha shilingi trilioni 26.13 kimekusanywa sawa na asilimia 93.2 ya lengo la mwaka.
Mwenendo wa Matumizi
Makadirio ya matumizi kwa mwaka wa fedha 2019/20 yalikuwa shilingi trilioni 33.11 ambapo shilingi trilioni 20.86 ni matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 12.25 ni matumizi ya maendeleo. Katika kipindi cha Julai, 2019 hadi Aprili 2020, jumla ya shilingi trilioni 24.85 zimetolewa sawa na asilimia 88.6 ya lengo. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 17.22 zilikuwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ambazo zinajumuisha shilingi trilioni 5.83 kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa umma, shilingi trilioni 2.91 kwa ajili ya matumizi mengineyo na shilingi trilioni 8.48 kwa ajili ya kugharamia deni la Serikali na mahitaji mengine ya Mfuko Mkuu.
Tathmini ya Uhimilivu wa Deni la Taifa
Serikali imeendelea kusimamia deni la Taifa kwa mujibu wa Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada Sura ya 134 kwa lengo la kuhakikisha linakuwa himilivu muda wote. Tathmini ya uhimilivu wa deni la Taifa iliyofanyika Desemba, 2019 ilibainisha kuwa deni ni himilivu kwa muda mfupi, wa kati na mrefu. Katika tathmini hiyo, viashiria vinavyopima uwezo wa nchi kukopa vinaonesha kuwa: Katika mwaka 2019/20, uwiano wa thamani ya sasa ya deni lote kwa Pato la Taifa ni asilimia 27.1 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 70; uwiano wa thamani ya sasa ya deni la nje kwa Pato la Taifa ni asilimia 16.3 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 55; na uwiano wa thamani ya sasa ya deni la nje kwa mauzo ya nje ni asilimia 103.9 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 240.
Hali ya Umaskini
Hali ya umaskini wa kipato na usio wa kipato iliendelea kupungua ambapo kiwango cha umaskini wa mahitaji ya msingi (basic needs poverty) kimepungua kutoka asilima 28.2 mwaka 2011/12 hadi asilimia 26.4 mwaka 2017/18. Kiwango cha umaskini kimepungua katika maeneo yote ya mijini na vijijini ambapo katika maeneo ya mijini, umaskini ulipungua kutoka asilimia 21.7 hadi asilimia 15.8 na maeneo ya vijijini ulipungua kutoka asilimia 33.3 hadi asilimia 31.3. Aidha, kina cha umaskini (poverty depth) kilipungua kutoka asilimia 6.7 mwaka 2011/12 hadi asilimia 6.2 mwaka 2017/18 na ukali wa umaskini (poverty severity) ulipungua kutoka asilimia 2.3 hadi asilimia 2.1. Wastani wa matumizi ya kaya kwa mwezi yameongezeka kutoka shilingi 258,751 hadi shilingi 416,927.
Kupungua kwa umaskini kumetokana na juhudi kubwa zilizofanywa na Wananchi na Serikali yao kupambana na umaskini wa kipato na usio wa kipato. Juhudi za Serikali zinahusisha: uwekezaji katika miundombinu wezeshi kwa shughuli za uzalishaji mali na biashara ili kukuza uchumi na hatimaye kuongeza pato la wastani kwa kila Mtanzania; kusimamia na kuboresha sekta ya fedha; kuongeza upatikanaji wa huduma za msingi kama vile afya, elimu, maji na umeme hususan maeneo ya vijijini; na kuendelea kutekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya jamii (TASAF) ili kuongeza kipato chao na kuwawezesha kupata mahitaji ya msingi.
Hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa TASAF III ni pamoja na: kutambuliwa na kuandikishwa kwa kaya takribani 1,084,018 zenye wanakaya 5,217,985 katika vijiji na mitaa 9,785 kwenye Halmashauri 159 Tanzania Bara na kaya 34,490 zenye wanakaya 196,301 katika shehia 204 za Zanzibar. Aidha, ruzuku ya fedha shilingi bilioni 968.73 imehawilishwa katika kaya hizo. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 935.94 ni kwa Tanzania Bara na shilingi bilioni 32.79 ni kwa Zanzibar. Kazi nyingine zilizofanyika ni pamoja na kutekeleza miradi 8,384 ambayo imezalisha ajira za muda kwa kaya 230,738 Tanzania Bara na kaya 14,555 katika miradi 251 kwa Zanzibar. Aidha, miradi 47 ya kuendeleza miundombinu katika sekta za elimu, afya na maji Tanzania Bara na miradi 8 katika sekta za elimu na afya kwa Zanzibar imekamilika.
Ulipaji wa Madai
Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kulipa madai ya wakandarasi, wazabuni, watoa huduma na watumishi. Tangu Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli iingie madarakani hadi Aprili, 2020 Serikali imelipa madai mbalimbali yenye jumla ya shilingi trilioni 3.2. Vile vile, Serikali imelipa madai ya kimshahara ya watumishi wa Umma ya jumla ya shilingi bilioni 114.5. Azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuendelea kuhakiki na kulipa madai yote ya watoa huduma, wazabuni, wakandarasi na watumishi kwa lengo la kuchochea shughuli za kiuchumi na kudhibiti madai hewa bila kuathiri mitaji na utendaji kazi katika sekta binafsi.