Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
- Thread starter
- #221
Ndugu zanguni nimeandika kitu kidogo:
"Hukaa mara nyingi sana nikajiuliza na si katika kujipigia tarumbeta bali ni katika kufikiri kuwa ingekuwaje kama Kleist Sykes asingeandika historia ya maisha yake kabla ya kufariki kwake mwaka wa 1949.
Mzee Kleist katika mswada wa kitabu alioacha kaeleza mambo mengi kuanzia jinsi baba yake na vijana wenzake wa Kizulu walivyochukuliwa na Hermann von Wissman kutoka kijiji cha Kwa Likunyi Mozambique hadi Pangani kama askari mamluki kuja kupigana na Abushiri bin Salim Al Harith na Mtwa Mkwawa.
Mzee Kleist akaeleza pia jinsi alivyokutana na Dr. Kweggiyr Aggrey mwaka wa 1924 na kumshawishi kuasisi African Association (AA).
Kutokana na mswada huu wa Mzee Kleist ndipo hii leo tukayajua majina yote ya waasisi wa AA.
Hii AA ndiyo ikawa TAA mwaka wa 1948 mwaka mmoja kabla ya kifo cha Kleist Sykes na mwaka wa 1954 ikageuzwa na kuwa TANU chama cha kupigania uhuru wa Tanganyika.
Katika kuundwa kwa TANU mwaka wa 1954 watoto wote watatu wa Mzee Kleist walihusika, wawili, Abdulwahid na Ally wakiwa wajumbe wa mkutano wa uasisi wa chama na Abbas wakati ule akiwa kijana mdogo akiwa nje ya chumba cha mkutano akisubiri kutumwa kufanya hili na lile katika shughuli za mkutano ule.
Lakini hadi TAA kufika pale ilipofika kuasisi TANU kupigania uhuru wa Tanganyika, mchango wa Abdul na Ally Sykes haumithiliki.
Hauna kifani si tu kwa kuwa walikuwa wafadhili wakuu bali Abdul Sykes ndiye aliyempokea Julius Nyerere na kumweka katika uongozi wa TAA mwaka wa 1953 na mwaka unaofuatia TANU ikaundwa.
TANU imeundwa ndani ya jengo ambalo lilijengwa kila siku ya Jumapili kati ya mwaka wa 1929 hadi 1933 kwa wanachama kujitolea nguvu zao.
Mipango yote ya kuendea kuunda TANU ilikuwa ikifanyika nyumbani kwa Abdul Sykes Mtaa wa Stanley na Sikukuu.
Hii ndiyo nyumba Julius Nyerere alikuja kuishi mwaka wa 1955 baada kuacha kazi ya ualimu.
Abdul Sykes anaeleza anasema kuwa yeye alipokuwa mtoto baba yake alikuwa akimchukua kwenda pale New Street ulipokuwa unafanyika ujenzi ule na ameona kwa macho yake lile jengo likijengwa.
TANU ilipoundwa kadi 1000 za mwanzo zilinunuliwa na Ally Sykes na kadi no. 1 ya TANU Ally Sykes alimwandikia TANU Territorial President Julius Kambarage Nyerere no. 2 akajiandikia mwenyewe na no. 3 akamwandikia kaka yake Abdulwahid, kadi no. 4 Dossa Aziz, kadi no. 5 Denis Phombeah, kadi no. 6 Dome Okochi Budohi na kadi no. 7 akamwandikia mdogo wake Abbas na kuendelea na wengineo.
Nini ikimetokea hadi historia ya TANU ikawa imeandikwa na haya yote yakawa yamefutwa kiasi kuwa hadi hivi ninavyoandika TANU yenyewe chini ya uongozi wa Julius Nyerere hadi kufikia CCM chini ya Nyerere ikawa haitambui historia hii?
Abdul Sykes amefariki mwaka wa 1968 maziko yake yalihudhuriwa na umma wa watu wa Dar es Salaam si kwa sababu ya TANU bali kwa umaarufu wake binafsi.
Magazeti ya TANU The Nationalist na Uhuru hayakuandika taazia wala kueleza kuwa marehemu alikuwa na mchango mkubwa katika kuunda TANU na kupigania uhuru wa Tanganyika.
Ally Sykes kafariki mwaka wa 2013 CCM haikushughulika kwa lolote kueleza mchango wake katika kuunda TANU na kupigania uhuru wa Tanganyika.
Mimi ndiye niliyesimamishwa pale nyumbani kwake Mbezi Beach kumzungumza Ally Sykes na mchango wake katika kuunda TANU na kupigania uhuru wa Tanganyika.
Hapakuwa na rambirambi kutoka CCM.
Maziko ya Abbas Sykes yamefuata mkondo ule ule wa kaka zake wawili.
Kazikwa na ndugu zake watu wa Dar es Salaam.
CCM haikuwakilishwa na yeyote ingawa Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete alihudhuria maziko na akawa amekaa pembeni na Balozi Abdul Faraj, rafiki ya Abbas Sykes toka utoto wao.
Inakuwaje CCM inaikataa historia yake yenyewe?
Hii nini maana yake?
Kipi kisichopendeza katika historia ya kina Sykes?
Ni kuwa baba yao kaasisi harakati au ni kwa kuwa Abdul Sykes kampokea Nyerere?
Kipi hasa kisichowapendeza?
Juu ya haya yote Rais Kikwete katika kusheherekea miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika aliwatunuku Abdul na Ally Sykes, ''Medali ya Mwenge wa Uhuru,'' kwa mchango wao katika kuunda TANU na kupigania uhuru wa Tanganyika."