Nyakati za nyingi hofu
Winner Chimba
Nyakati za nyingi hofu, hizi zimetufikia
Kirusi kama siafu, vile kinanyemelea
Twajiona wote wafu, japo bado twatembea
Nani tumgeukie, Isipokuwa Rabana
Kifo kinatuvizia, kila tunapotembea
Hakitaki kuachia, kambi kimejiwekea
Sana kinatunukia, woga kinatuachia
Nani tumtegemee Isipokuwa Rabana?
Niwawazapo wazazi, woga unanivamia
Yakiwapata maradhi, kipi kitachotokea
Magonjwa ya nyemelezi, wanayo nakumbukia
Nani atusaidie, kama sio mwenye enzi?
Wangu binti na kijana, sana ninawawazia
Shuleni wanapokwenda, bila hata barakoa
Vipi wakiambukizwa, hofu inanivamia
Sina wa kumgeukia, isipokuwa Rabana
Mtandaoni kiingia, mawazo nipunguzie
Nakutana na tanzia, mara huyu mara yule
Wazee watangulia, nani tumkimbilie?
Nani atatufariji, Isipokuwa Rabana?
Wanaanguka magwiji, walosheheni hekima
Wajuzi na wabobezi, ya maarifa hazina
Wetu wazazi na walezi, walotulea vijana
Nani tutamlilia, isipokuwa Manani
Wenye nguvu vijana, nao wajiondokea
Madaktari sanasana, kazini wanajifia
Nguvu kazi ya taifa, bure inapotelea
Nani atusaidie, Isipokuwa Mwenyezi?
Ka mshumaa wanazima, bila hata kutuaga
Nyoyo zimetuzizima, waondoka ghafla ghafla
Na tulie kimyakimya, wanasema wa siasa
Hawataki kusikia, vilio vikizidia
Hawataki kusikia, amani twaichafua
Eti tukiomboleza, taharuki tunazua
Tanzia hawazitaki, eti zinawachefua
Nani tumkimbilie, Isipokuwa Rabana?
Viongozi wa taifa, wale tulowachagua
Wasomi walobobea, nao pia wamefyata
Tafiti wameziacha, wafata ya kusikia
Wamegeuka vioja, sinema kutufanyia
Wote wamejificha, hawana la kutwambia
Wale tulowategemea, sasa wametukimbia
Wametuacha wakiwa, nani atatutetea?
Nani atatutetea, Isipokuwa Rabana?
Nani atutegemeze, isipokuwa Rabana
Hofu tumuelezee, asiyechoshwa na waja
Machozi tummwagikie, kwake mwingi wa faraja
Hayupo mwingine tena, Isipokuwa Rabana
Azielewa simanzi, kamwe hatatukataa
Tukumbate kifuani, machozi atayafuta
Tumwelezee huzuni, yeye anategemeka
Ndiyo yeye tumaini, Hakuna mwingine tena
Tusiache tahadhari, bora sana kujikinga
Wasiwasi ni akili, hata wakitusimanga
Wengine kuwafikiri, huo ndio uungwana
Hayo yote tukifanya, Mola atatusitiri.