CCM yatumia Sh10b kununua magari
YASEMA MECHI BILA MAZOEZI HAKUNA USHINDI,YASISITIZA KULIPA KODI
Mwandishi Wetu
IMEBAINIKA kwamba CCM imetumia takriban Sh70 milioni kununua gari moja kati ya magari 150 aina ya Land Cruiser Hardbody yaliyoagizwa kwa ajili ya kufanikisha mradi wa kuimarisha chama" hicho, lakini bei halisi ya magari hayo ni zaidi ya Sh107 milioni.
Uchunguzi wa Mwananchi unaonyesha kuwa CCM itatumia zaidi ya Sh10 bilioni kununua magari yote 150 ambayo yatasambazwa kwenye wilaya zote nchini kufanikisha shughuli za kisiasa za chama hicho tawala.
Taarifa za kuingizwa kwa magari hayo zilifichuliwa na katibu mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa wakati alipoituhumu CCM kuwa imeingiza magari 200 na kukwepa ushuru wa takribani Sh600 milioni.
Dk Slaa alitoa tuhuma hizo wakati akihutubia kwenye moja ya mikutano ya Operesheni Sangara mkoani Tanga, lakini CCM ikamkosoa kuwa idadi ya magari iliyoagiza ni 150 na kwamba kiwango cha ushuru ni kikubwa zaidi ya alichokitaja.
Lakini tofauti hiyo ya bei halisi ya magari hayo na kiasi cha fedha kilichotajwa na CCM kuwa kimetumika kugharamia ununuzi wa magari na ushuru, kinaweka maswali kuhusu ukweli wa sakata hilo.
CCM imeeleza kuwa imeshaingiza magari 74 kutoka Japan wakati mengine 76 yapo bandarini yakisubiri kukamilika kwa taratibu za kulipia ushuru ili yatolewe wakati wowote kuanzia leo.
Uchunguzi wa Mwananchi unaonyesha kuwa CCM pamoja na kulipa ushuru imenunua gari moja kwa Sh70,451,619.7. Lakini taarifa kutoka kampuni inayouza magari hayo hapa nchini (Toyota Tanzania Limited) zinaonyesha kuwa gari moja la aina hiyo pamoja na kulipia ushuru linauzwa kwa Sh107,813,905, ikiwa ni tofauti ya Sh37,362,285.3.
Katibu wa masuala ya uchumi na fedha wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec), Amos Makalla alibainisha wakati akiongea na waandishi wa habari kuwa chama hicho kimetumia Sh3,493,354,830 kununua magari hayo na imetumia Sh1,720,065,031 kulipia ushuru.
"Kwa magari hayo 74, tumelipa Sh3,493,354,830, sasa kama wewe ni mwanamahesabu mzuri jumlisha na ushuru tuliolipa wa Sh1,720,065,031 utajua gharama zote," alisema Makalla, ambaye alikuwa kiongozi wa tatu kutoa ufafanuzi wa tuhuma za Dk Slaa baada ya kutanguliwa na katibu wake mkuu, Yusuf Makamba na katibu wa itifaki wa Nec, John Chiligati.
"Ukitaka kujua bei ya gari moja aina ya Toyota Landcruiser Hardbody tuliyonunua, chukua kiasi hicho gawanya kwa 74."
Kwa maana hiyo, jumla ya fedha zilizotumika kununua na kuingiza magari hayo ni Sh5,213,419,861, ambayo ukiigawanya kwa 74 unapata Sh107,813,905, ambazo zilitumika kununulia gari moja kati ya hayo 150.
Kwa maana nyingine, gharama za magari 76 yaliyo bandarini zinakadiriwa kufikia Sh5,354,323,100.5 bilioni zikujumuishwa na ushuru wa Sh1,766,553,275.1 bilioni unaotarajiwa kulipwa kwa ajili hiyo.
Lakini utafiti uliofanywa Toyota Tanzania Limited, ambayo ni wakala wa magari hayo nchini unaonyesha kuwa bei ya sasa ya gari aina ya Toyota Landcruiser Hardbody ni Sh107 milioni baada ya kulipiwa ushuru na kukamilisha taratibu nyingine.
Kiwango hicho kinafanya tofauti ya bei iliyotumiwa na CCM na ile ya kampuni ya Toyota ni takribani Sh33 milioni. Makalla hakupatikana baadaye jana kutoa ufafanuzi kama magari waliyoagiza ni mtumba au ni mapya. Pia wakala aliyeagizia magari CCM hakuweza kupatikana jana.
Mwaka 2005, CCM pia iliagiza shehena ya magari aina ya Mahindra ambayo pia yaliamsha tuhuma kuwa chama hicho tawala kilikwepa kodi wakati wa kuyaingiza.
Makala alithibitisha kuwa magari mengine 76 yataanza kutolewa bandarini muda wowote kuanzia leo, pindi TRA itakapokamilisha taratibu na nyaraka husika zitakazoiwezesha CCM kulipia ushuru.
"Tumeyaleta (haya magari) kwa ajili ya mradi wa kuimarisha chama, lakini zitasaidia pia uchaguzi wa 2010. Tunalenga kuwafikia wananchi wote hata vijijini, tunafanya siasa ambayo bila usafiri haiwezekani, lakini kwa kuwa uchaguzi ni mwakani, tunafanya mazoezi kwani mechi bila mazoezi huwezi kushinda. Sasa tunapiga jalamba," alisema Makalla.
Tangu Dk Slaa amwage hadharani mpango huo, viongozi tofauti wa CCM wamejaribu kutoa ufafanuzi, akiwemo Chiligati ambaye alisema kwa kifupi tu kuwa chama hicho ni kikubwa hivyo suala la kununua magari hayo si la ajabu.
Makamba alifafanua makombora ya Dk Slaa kwa kueleza kuwa alikosea katika idadi ya magari yaliyoagizwa na CCM na kutaja kuwa ni 150 na ndipo Makalla alipoanza kutoa ufafanuzi kwa kuonyesha waandishi nakala za nyaraka za kuagizia magari hayo na risiti za benki za kulipia ushuru. Kuhusu mkakati wa wanaCCM kukichangia chama hicho fedha ili kijitegemee, Makalla alisema wanachama wameitikia wito huo na wengi wameonyesha nia ya kuchangia, lakini akasema baada ya vikao vikuu vya CCM Januari na Februari mwaka 2010 watazindua kampeni hizo za kuchangisha fedha.