Twataka magari ya uchaguzi au magari ya maendeleo?
Hidaya
Disemba 30, 2009
Kwa Waziri wa Mikiki na Makeke,
Uzitoni Street,
Bongo.
Mheshimiwa mpenzi wangu Frank,
VIPI Krisimasi yako? Ulifurahi pamoja na mama yako? Nadhani karibu ndugu zako wote walikusanyika kule. Raha iliyoje! Nilisikitika sana hatukuwa wote.
Lakini pia, baada ya kumeza uchungu wote wa kukukosa wakati wa Krisimasi, nafurahi sana angalau kuwasiliana na wewe kwa njia hii. Yaani mpenzi nilivyokuwazia wakati wa Krisimasi! Nikiwahudumia wageni wote wa bosi, nakuwazia hadi nafikiria na wewe utaingia pamoja na kundi jingine, nikikosha vyombo naona uso wako ndani ya kila kikombe, nikifagia nyumba baada ya wageni wote kuondoka, naona vumbi zinajikusanya kuunda uso wako. Hadi nalala nakuota wewe tu. Ndiyo maana nakuita mheshimiwa wangu maana unawakilisha kila kitu kwangu. Waniridhisha, wanifurahisha, una matendo (si maneno) yanayonifanya nijikabidhi kwako moja kwa moja.
Laiti waheshimiwa wetu wa mji wa kudidimia wangekuwa kama wewe. Yaani hapa kwa bosi ilikuwa kufuru. Watu wamemiminika wakitegemea Krisimasi imwagike kwao. Na kwa kuwa ule uchaguzi unanukia, basi bosi akageuka Baba Krisimasi. Ilibaki kidogo avae ile suti nyekundu na ndevu feki kama wengine. Yaani sisi wabongo, Bwana. Suti ya nchi za baridi, labda wavae Makete, lakini hapa Bongo, unaona kabisa dimbwi la jasho likijitengeneza kwapani. Kwani lazima tuige hayo? Kuna mtu kaniambia hata theluji haikuwapo Israel enzi zile, mambo yote hayo ya theluji na nini, ni mambo ya Wazungu tu! Ama kweli iga ufe, maana mababa krisimasi wanaonekana kama presha kuka!
Lakini tuache hayo maana sisi kwa kuiga kila kitu hatujambo. Kilichonichekesha mimi ni kwamba baadhi ya wapiga kura wa bosi (maana mwaka huu unaokuja hatuwi binadamu tena, tunakuwa wapiga kura tu) walimiminika wakitarajia kufaidi magari mapya ya chama cha bosi. Yaani watu Bwana. Bosi aliposema kwamba magari hayo yanangoja uchaguzi, bado walisononeeeeka, utadhani maafa makubwa. Eti walitaka kuwa wa kwanza kufaidi.
Ndipo hapo nashindwa kuelewa mpenzi. Kwa mfano, ungeamua kugombea na wewe (na hapo mimi kweli mpiga kura wako), ungeona jambo gani ni muhimu zaidi? Ungefanya nini ili upendwe na wapiga kura wako? Ungenunua magari makubwa na vipaza sauti kibao? Njia nzuri ya kuonyesha kwamba kweli wewe unawajali kama mwakilishi mtarajiwa ni kujitangaza kwa njia ya magari? Au ni kuhakikisha mambo yote ndani ya jimbo lako yanaenda vizuri?
Kwa kweli inanitia uchungu mpenzi. Nikifikiria hali ya kituo cha afya kule kwa mama yangu. Kituo gofu tu. Hakuna dawa, hakuna gari la kupeleka wagonjwa. Mama kaniambia jirani yetu, Mama Saidi alifariki juzi wakati anajifungua kwa sababu walishindwa kumwahisha hospitali kubwa. Sasa baada ya hapo aje mtu na kipaza sauti chake ndani ya gari linalomeremeta kama gari la harusi, aniambie kwamba ananipenda sana ndiyo maana anataka kwenda kudidimia huko kwa ajili yangu nitamwelewa kweli?
Ndiyo maana naanza kuogopa sana hili dudu uchaguzi. Najua upande mmoja wengine watafaidi pilao kama ile ya Krisimasi (pilao mara moja kwa miaka mitano?). Najua na barabara zetu zitapigwa greda kidogo (ili ziharibike tena mara baada ya uchaguzi). Najua na tutawaona watu kutoka Dar es Salaam, na hata kutoka makao makuu ya mkoa ambao tulikuwa tunawasikia tu. Najua na wengine watapata angalau fulana ya kwenda kulima nayo. Lakini hayo ndiyo ya maana kweli? Nadhani ndiyo maana wengine wanatuita Wadanganyika maana kwa hayo madogo tu tumeshamchagua mtu asiyetujali hata chembe.
Mimi nilidhani kwamba lengo la kuchaguliwa ni kuleta maisha bora kwa wananchi. Lakini sasa naona lengo la kuchaguliwa ni kuchaguliwa tu. Hakuna lengo la zaidi. Kuchaguliwa basi! Na kama ni hivyo, kuna faida gani kuwa na uchaguzi?
Au unaonaje mpenzi? Kwa kweli mimi nilikuwa naona uchungu sana bila kutafakari kwa undani. Lakini mgeni mmoja wa bosi aliweza kueleza kwa maneno nilichokuwa nasikia ndani ya moyo wangu. Hadi bosi alikasirika kama kawaida yake. Kwanza huyu mgeni alianza kwa kumsalimia.
‘Habari za maandalizi ya uchaguzi?'
‘Na wewe Bwana mambo zako! Hatujaanza hata mwaka mpya wewe unaongelea hayo?'
‘Kwani uongo? Badala ya kumiminika kwenye mahoteli makubwa ya wenyewe, watu wamekumbuka hata njia ya kwenda kijijini kwao. Pesa zimeshaanza kumwagwa kama kokoto za kujengea nyumba. Na wewe hujamwaga kidogo?'
Bosi alicheka.
‘Sasa ukitaka kujenga, si uanze mapema. Watu watajuaje kwamba ninawafaa kama simwagi hizo.'
‘Angalia hizo lakini usije ukamwaga radhi badala ya neema.'
‘We Bwana, hubadiliki? Yaani tangu tukiwa shuleni, kazi yako kukosoa tu. Ndiyo maana huwezi kupata maendeleo hata kidogo'
‘Nani kakuambia sipati maendeleo? Kwani maendeleo ni kufanya kufuru na pesa zako wakati wenzetu hawana kitu? Hebu angalia na haya magari yote uliyoyaagiza. Ndiyo njia ya kuleta maendeleo?'
‘Ndiyo njia ya kuchaguliwa ili tuweze kuzidi kuleta maendeleo.'
Lo! Yule mgeni akacheka hadi alipaliwa. Hadi machozi yalimtoka au labda yalikuwa ni machozi ya uchungu.
‘Usinichekeshe Bwana. Kama kweli nia yenu ni kuleta maendeleo, msingenunua magari ya uchaguzi. Angalia jina lenyewe ... magari ya uchaguzi. Si magari ya maendeleo hapana. Si magari ya hospitali au magari ya shule, hata kidogo. Ni magari ya uchaguzi!! Mabilioni mangapi kwa ajili ya uchaguzi tu?'
‘Lakini katika mfumo wa demokrasia lazima kwanza ushinde ili uweze kuwahudumia watu. Uchaguzi ni maendeleo.'
Mgeni alinyanyua mkono.
‘Usinichekeshe tena Bwana. Nikipaliwa tena, itabidi unipeleke hospitali na magari yenu ya uchaguzi. Mimi kwanza sioni hata faida ya uchaguzi siku hizi maana nyie wakubwa mmekwisha kujua jinsi ya kuvuruga uchaguzi wenyewe.'
‘Una maana gani?'
‘Sikiliza hoja za watu! Wanatumia pesa, ukabila, udini vyote kichinichini hadi watu wanafikiri hii ndiyo maana ya uchaguzi. Watu wanaanza kuamini kwamba uchaguzi maana yake ni kundi fulani katika kabila au dini, au eneo lifaidi kutokana na mwenzao kuchaguliwa. Si uchaguzi ili watu wote wafaidi kutokana na kulengesha maendeleo kwa wote. Uchaguzi unatugawa badala ya kutuunganisha.'
‘Kwa hiyo wewe unapendekeza nini?'
‘Sioni hata faida ya kuwa na wabunge. Kila mwaka kila halmashauri ingeteua diwani mmoja kwenda kuwawakilisha tu. Hapo tungeokoa pesa nyingi sana, na pia kuondoa hili tabaka la walaji.'
Bosi alianza kukasirika.
‘Nimekuambia rafiki yangu wewe kazi yako kukosoa tu, kukosoa tu. Huoni hata kitu kimoja kizuri tunachokifanya.'
‘Naona! Lakini upande wa uchaguzi naona mmeshapotoka. Vipaumbele vyenu si sawa kwa sababu lengo lenu ni kuchaguliwa tu, si yatokanayo na uchaguzi. Ndiyo maana tunafisadiwa tu.'
‘Ohoo, umeanza na wimbo huohuo. Huna kitu kingine. Nimechoka na hayo. Kama unaona mambo ni rahisi kiasi hicho.'
‘Thubutu! Nijihusishe na watu wanaonuka ....'
‘Imetosha Bwana. Kama umekuja kuniletea nuksi badala ya furaha ya sikukuu, hebu ondoka.'
Hadi bosi alienda kufungua mlango kabisa. Hasira mtindo mmoja.
Kwa hiyo ndiyo hivyo mpenzi. Magari ya uchaguzi wakati maisha ni uchafuzi. Tutabadilika lini.
Akupendaye akupendaye, akupendaye mheshimiwa wa maisha yangu,
Hidaya.