Zitto ageuka mada
na Irene Mark
UAMUZI wa Rais Jakaya Kikwete kumteua Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto, kuwa mjumbe wa kamati ya kuhakiki madini, umezidi kuchukua sura mpya, zinazotofautiana kila kukicha.
Hali hiyo imejidhihirisha tangu baadhi ya makundi ya watu wenye ushawishi, kuanza kuhoji kile kilichosababisha kuwamo kwa mwanasiasa huyo wa upinzani ndani ya kamati hiyo, Tanzania Daima imebaini.
Taarifa zilizokusanywa na gazeti hili kutoka vyanzo mbalimbali vya habari huru na vile vyenye masilahi tofauti katika suala hili, zinaonyesha kwamba, hoja hiyo sasa ndiyo inayogusa hisia za makundi yenye ushawishi katika jamii.
Aidha, mwenendo huo wa mambo, ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) anakotoka Zitto, umesababisha kuibuka na kuendelea kuimarika kwa makundi yenye mtazamo na mwelekeo unaopingana.
Hali hiyo ya mambo ambayo imepewa tafsiri tofauti na watu na vyombo mbalimbali vya habari, sasa imesababisha CHADEMA ilazimike kuchukua hatua za haraka kudhibiti mwelekeo wa mambo ambao kwa hakika unakiweka chama hicho katika hatari ya kuyumba, na kama hali isipodhibitiwa, kwenda kule ilikokwenda NCCR-Mageuzi miaka takriban 10 iliyopita.
Msimamo wa wanasiasa kadhaa ndani ya chama hicho unaoonyesha hali ya kutoaminiana na kupingana waziwazi, sasa umesababisha uongozi wa juu wa chama hicho, ukiongozwa na Mwenyekiti wake wa taifa, Freeman Mbowe, kuamua kuingilia kati ili kurejesha utulivu na mshikamano.
Habari kutoka ndani ya chama hicho ambazo zimethibitishwa na Mbowe na Katibu Mkuu wake, Willbrod Slaa, zinaeleza kuwa kwa siku nzima jana viongozi wote wakuu wa CHADEMA walitumia siku nzima kuwasiliana na kuwekana sawa kuhusu kimbunga cha kisiasa kinachoonekana kukikumba chama chao.
Wakati viongozi hao wakitafakari hatima ya chama hicho, wanahabari wa ndani na wale wa mashirika ya kimataifa ya habari kama lile la Uingereza (BBC) na la Ujerumani (DW) walikuwa wakihaha kuwasaka viongozi wakuu wa chama hicho ambao wamesambaa katika maeneo mbalimbali.
Miongoni mwa viongozi ambao walikuwa wakisakwa kwa udi na uvumba, ni Mbowe ambaye sasa yuko masomoni Uingereza akisomea siasa, uchumi na filosofia katika Chuo Kikuu cha Hull.
Kutokana na hali hiyo tete, Mbowe jana aliihakikishia Tanzania Daima kuwa, alikuwa amelazimika kurejea nyumbani na kuitisha kikao cha Kamati Kuu ya dharura ya chama hicho, lengo likiwa ni kufikia uamuzi wa pamoja utakaomaliza mzozo wa maneno kuhusu uteuzi huo wa Zitto.
Kikubwa kilichosababisha kurejea kwa Mbowe, ni kuibuka kwa mvutano wa mawazo ndani ya chama hicho yakihusisha makada wenye majina makubwa ndani ya CHADEMA ambao ama wanamuunga mkono Zitto au wanamtaka ajitoe katika kamati hiyo.
Akizungumza katika mahojiano kwa njia ya simu jana, Mbowe hakuwa tayari kutoa maoni yake kuhusu suala hilo zaidi ya kusema kwamba, chama hicho kilikuwa kikitarajia kutoa tamko lake rasmi Jumamosi wiki hii.
Mjumbe mmoja wa Kamati Kuu ya CHADEMA aliieleza Tanzania Daima kwamba, uamuzi wa kuitisha kikao hicho umekuja baada ya kubaini kuwapo kwa mpango mahususi kutoka kwa mahasimu wao wa kisiasa unaolenga kukisambaratisha chama chao, ambacho katika siku za hivi karibuni kimejijengea umaarufu mkubwa machoni mwa wananchi.
"Tunafahamu kwamba, hawa mahasimu wetu wanataka kutugombanisha kwa kutumia uteuzi huu wa Zitto. Ni jambo la bahati mbaya kwamba na sisi tumeingia katika mtego wao na tunacheza ngoma ya kujimaliza wenyewe," alisema kada huyo wa CHADEMA.
Akizungumzia mwenendo na misimamo ya baadhi ya wana CHADEMA, muasisi wa chama hicho, Edwin Mtei, alisema hakuna sababu ya Zitto kujiondoa ndani ya kamati hiyo, na akasisitiza kuwa chama hicho kinapaswa kutumia nafasi hiyo kuwasilisha maoni yake serikalini.
Alisema, CHADEMA ni mkusanyiko wa watu wengi, hivyo mawazo ya watu yanapokewa na kujadiliwa kwa mtazamo mpana zaidi, ili kuifikisha nchi kwenye maendeleo yanayotakiwa.
Alionya kuwa ni vigumu kuendesha nchi kwa kususia, badala yake aliwataka walio kwenye makundi kutoa mawazo ndani ya kamati husika za chama kwa ujasiri na uwazi.
"Tangu tulipounda chama tunaamini katika uwazi na ukweli lakini ‘view' zetu zinakuwa ‘recorded' huwezi kurekodi kama tunasusa, ni vizuri kwamba Zitto amekubali kushiriki na kushawishi.
"Endapo mawazo yake yatakubalika, atakuwa ame-influence policy ya nchi yetu na kama atapuuzwa, anaweza akatoa minority report. Mchango wetu uwe ni wa kuchangia na si wa kususia," alisema Mtei.
Alisema: "Wanaosema kuna ‘vested interest' ni lazima wajue kuwa masilahi ya kwanza ni nchi yetu…kama kuna mtu anaogopa ‘views' zake zitakuwa influenced, hana msimamo."
Hata hivyo aliweka wazi kwamba amempelekea Zitto mawazo yake na hadidu rejea na akamtaka aendelee kupigania masilahi ya taifa ndani ya kamati.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willbrod Slaa alikiri kuwa uongozi wa chama utakutana mwishoni mwa wiki kutoa msimamo kuhusu kamati ya madini iliyoteuliwa na Rais Kikwete.
"Kamati Kuu ya CHADEMA itakutana mwishoni mwa wiki kujadili suala la Zitto, lakini kubwa zaidi ni muundo mzima wa kazi za kamati ya madini iliyoteuliwa na Rais," alisisitiza Dk. Slaa ambaye msimamo wake kuhusu kamati hiyo umeacha maswali mengi.
Aidha, Mwenyekiti wa CHADEMA wa Mkoa wa Kigoma, Jaffari Kasisiko, aliupongeza uamuzi wa Rais Kikwete na kuongeza kuwa matokeo ya kamati hiyo yatawaongezea imani wananchi kutokana na mchanganyiko wa wajumbe wake.
"CHADEMA Kigoma, inapongeza uamuzi wa Rais Kikwete kwa sababu unaleta heshima kwa wapinzani…tumemshauri Zitto kutoa ushirikiano wa kutosha kwenye kamati hiyo bila kujiengua kama anavyoshauriwa na baadhi ya watu," alisema mwenyekiti huyo.
Naye, Jussa Ismail, kutoka Chama cha Wananchi, amewataka wanaomshauri Zitto kujitoa kwenye kamati hiyo waache, badala yake wajenge siasa za kistaarabu.
Alisema, iwapo wataendelea kumshinikiza kujiondoa kwenye kamati watamwathiri kisaikolojia na kumfanya ashindwe kutekeleza majukumu yake ndani ya kamati hiyo.
"Umefika wakati wa kujenga siasa za kistaarabu, haya yanayotokea yanawachanganya wananchi, kwani lengo letu tangu mwanzo ni kuundwa kwa kamati ya kuchunguza mikataba ya madini na kurekebisha sheria zinazohusu madini.
"Leo hii tukimwambia Zitto asiingie kwenye kamati ile ni kumchanganya. Kufanya hivyo ni kujishushia hadhi wapinzani na jamii itashindwa kutuelewa, tutaonekana tunayumba," alisema Ismail.
Aidha, amemtaka Zitto kuendelea na shughuli mbalimbali ndani ya kamati hiyo na si kuufanya uteuzi wake kuwa wa kisiasa, badala ya masilahi ya taifa.
source:freemedia