Dar es Salaam. CHADEMA imeanza kutumia nguvu ya mahakama kupinga mchakato wa uteuzi wa wabunge 19 wa viti maalumu na mtu aliyesaini fomu zao kwa nafasi ya katibu mkuu.
Chama hicho kilistahili kupata wabunge wa viti maalum kutokana na kupata idadi ya kura za wabunge inayozidi asilimia tano, lakini kinadai hakukuwa na kikao kilichopitisha majina ya wanachama na kupeleka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa ajili ya uteuzi.
Lakini Noveemba 24, makada 19 walijitokeza viwanja vya Bunge na kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalumu katika utaratibu mpya unaomruhusu Spika kufanya kazi hiyo bila ya kuwepo na mkutano wa chombo hicho cha kutunga sheria, kitendo kilichosababisha Kamati Kuu ya CHADEMA iliyokutana Novemba 27 kuamua kuwavua uanachama.
Pamoja na kustahili viti hivyo, CHADEMA ilishatangaza kutotambua matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, ikidai kwamba uchaguzi huo ulitawaliwa na ukiukwaji wa sheria na taratibu.
Mkurugenzi wa itikadi, uenezi, mawasiliano na mambo ya nje wa CHADEMA, John Mrema alisema mchakato huo unaendelea na tayari katibu mkuu wa chama hicho, John Mnyika ameiandikia barua NEC.
Katika barua hiyo kwa NEC, alisema CHADEMA inataka kupatiwa nakala ya barua iliyowasilisha majina pamoja na fomu namba 8D ambazo katibu mkuu anatakiwa kujaza ili ijulikane aliyeijaza na hivyo aunganishwe kwenye kesi hiyo.
Mwananchi