Wapendwa wanaJF wenzangu:
Nimekuwa mchangiaji wa nadra sana wa JF kutokana na sababu ambazo nilishawahi kueleza hapa siku za nyuma, mojawapo ukiwa ni ushauri wa baadhi yenu ambao niliuheshimu.
Nimekuwa msomaji wa majadiliano yanayoendelea kuhusu mustakabali wa taifa letu, na katika baadhi ya mijadala imetajwa CHADEMA na jina langu limekuwa likijitokeza tokeza. Aidha baadhi yenu mniandikia ujumbe nije hapa kufafanua baadhi ya mambo yanayohusu CHADEMA hususani yale yanayonihusisha kwa namna moja au nyingine.
Niliwahi kuandika hapa kwa kirefu naichukuliaje JF, lakini moja ya mtazamo wangu kuhusu JFni kuwa hivi ni chombo cha habari, pia ni kama kijiwe cha kijamii cha mijadala, lakini pia ni kama mkutano wa majadiliano katika mji(town hall meeting), naitazama pia JF kama mkutano wa hadhara ambao kila mmoja yuko huru kuhutubia!.
Katika muktadha huo, kama ambavyo nashiriki mijadala katika matukio yenye sura ya hayo hapo juu, najihisi nina wajibu kwangu binafsi na kwenu kuja kushiriki mijadala mara kadhaa.
Kwa kuanzia nawaletea taarifa hii rasmi, ambayo nimeitoa leo kwa niaba ya ya CHADEMA. Taarifa hii inajibu baadhi ya maswali ambayo yamekuwa yakiulizwa hasa kuhusu yanayoendelea ndani ya chama katika siku za karibuni.
Tamko hilo mnaweza kulipata kwa kubonyeza hapa:
http://www.chadema.or.tz/habari/habari.php?id=103
Kesho tutakuwa na Kongamano la Vijana, halafu kuanzia tarehe 30 Novemba, 2009 mpaka tarehe 3 Disemba 2009 tutakuwa kwenye mfululizo wa vikao vya juu vya chama tukiutathmini mwaka 2009 na kupanga mwelekeo wa chama kwenda mwaka 2010.
Hivyo, naomba muendelee na mjadala na kama kuna maswali yatakayoulizwa nitakuja kuyajibu moja baada ya jingine baada ya tarehe hizo.
Salamu zangu za baraka ya Iddi kwa waislamu, ni siku nzuri ya kutafakari aya kwenye kurani tukufu mathalani Al Heed 57:25, Al-Nisa 4:35, Al-Maidah 5:8