Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinauarifu umma na wadau wote wa demokrasia nchini kuwa, jana Jumamosi, Agosti 16, 2025, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam lilivamia kikao cha ndani cha wanachama na viongozi wetu kilichokuwa kikifanyika Kibaha, Mkoa wa Pwani.
Katika uvamizi huo, Polisi waliwakamata wanachama wetu sita pamoja na raia wasio na hatia, ambao ni wakazi wa nyumba jirani na eneo la kikao. Waliokamatwa ni:
1. Pendo Msechu
2. Pendo Kyosi
3. Mary Mushi
4. Samson Mzambia
5. Focus Laurent
6. Alfred Bundala
Aidha, Polisi walifanya upekuzi ndani ya ukumbi, kwenye nyumba na kwenye magari yaliyokuwa eneo hilo, na wakaondoka na nyaraka muhimu za chama pamoja na fedha taslimu za Kitanzania.
Waliokamatwa walichukuliwa na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi (Central), jijini Dar es Salaam. Cha kushangaza ni kwamba Polisi wa Central walikana kuendelea kuwashikilia.
Tunaona kitendo hiki kama muendelezo wa Serikali kutumia vyombo vya dola kuishambulia Chadema na kukandamiza haki za raia.
Chadema inalitaka Jeshi la Polisi kutoka hadharani na kueleza:
1. Kwa nini lilivamia kikao cha ndani cha wanachama wa Chadema?
2. Kwa nini limewakamata wanachama wetu bila sababu za msingi?
Tunawakumbusha Jeshi la Polisi kuwa wajibu wao kwa mujibu wa sheria za nchi ni kulinda raia na mali zao, na siyo chombo cha kukandamiza vyama vya upinzani.
Chadema itaendelea kusimama kidete kupigania haki, uhuru wa wananchi na ustawi wa demokrasia nchini.
Imetolewa leo Jumapili, Agosti 17, 2025 na:
Brenda Rupia
Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi
Soma > Polisi: Tumewakamata Watu 10 Kibaha wakiwa wanaandaa njama za Uhalifu