Elias Msuya
Platinum Member
- Dec 23, 2011
- 267
- 1,014
Wafanyabiashara katika soko la Kilombero Arusha.
Arusha. Wakati Itifaki ya Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ikiweka msingi wa uhuru wa kusafirisha bidhaa na huduma kati ya nchi wanachama, bado kumekuwa na changamoto zinazokwaza itifaki hiyo kutekelezeka.
Lengo la itifaki hiyo ni kuongeza kiwango cha biashara ndani ya kanda kutoka asilimia 15 ya sasa hadi kufikia asilimia 40 ifikapo mwaka 2030.
Changamoto hizo ni pamoja na vizuizi visivyo vya ushuru (NTBs), ushuru wa muda, kodi mbalimbali, migogoro ya kibiashara kati ya nchi wanachama, ushindani kutoka kwa vyakula na mbegu za viwandani zenye bei nafuu, pamoja na miundombinu duni ya kurahisisha biashara, hasa usafirishaji na hifadhi ya mazao kwa wafanyabiashara wa agroekolojia (Agroecological Produce – AEPs).
Hayo yanajiri wakati Bara la Afrika likiwa tegemezi wa bidhaa za nje katika sekta ya chakula na kilimo, ikiwa pamoja na kutumia Dola bilioni 50 (Sh123.9 trilioni) kuagiza wa chakula kwa mwaka, Dola bilioni 9.2 (Sh22.81 trilioni) kuagiza wa mbolea kwa mwaka (rekodi ya mwaka 2024) na Dola bilioni 3.4 Sh8.43 trilioni) kuagiza viuatilifu kwa mwaka (rekodi ya mwaka 2023).
Biashara ya mazao ya agroekolojia barani Afrika inatajwa kuweza kupunguza kwa kiasi kikubwa utegemezi huu na hivyo kupunguza mzigo mkubwa wa uagizaji wa bidhaa za kilimo kutoka nje.
Wafanyabiashara Arusha
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mkoani Arusha, baadhi ya wakulima na wafanyabiashara wameeleza changamoto wanazopitia katika biashara za mazao yaliyolimwa ki agroikolojia.
Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni jijini Arusha, mfanyabiashara wa soko la Kilombero, Latifa Laswai amesema wamekuwa wakitegemea mazao kutoka ndani na nje ya nchi lakini wanakabiliwa na changamoto hasa za ushuru mipakani.
“Tunaishi kwa kutegemea bidhaa kutoka mikoani na nje ya nchi. Kwa mfano kwa sasa malimao tunategemea kutoka nchini Uganda na wakati huu, matajiri wamebadilika, unakuta anakwambia ili ukodi gari lazima utoe Sh4 milioni, hataki kujua malimao hayo yatachukua muda gani kufika na kama yatafika yakiwa na mazima au yana kasoro.
“Kwa hiyo tungeomba Serikali ituangalie wanawake kwa jicho la huruma ili watupunguzie ushuru wa mipakani, ushuru wa mazao,” amesema.
Amegusi pia changamoto ya mitaji, akisema kutokana na changamoto za ushuru na gharama za usafirishaji, wanashindwa kulinda mitaji hiyo.
“Tunategemea mikopo ya halmashauri, hivyo watukopeshe ili kutuwezesha, kwa sababu tunarejesha kila mwezi. Sasa ikitokea umeagiza mzigo halafu kukawa na kasoro, maana yake unakata mtaji, matokeo yake mwisho wa mwezi huna rejesho,” amesema.
Ameendelea kueleza kuwa changamoto wanazokumbana nazo wanalazimika kutoa hata rushwa ili kufanikisha biashara zao.
“Kwa mfano nimetoka Uganda nimenunua malimao, nataka nivushe pale Namanga (Mpaka wa Kenya na Tanzania), nimeishiwa hela yote, utakuta trafiki anakwambia dada nipe hata Sh20,000, mwisho wake unalazimika kutoa hata rushwa ya ngono kwa sababu unaona ndio kitakachokusaidia, ili uweze kuvuka hiyo hatua kwenda nyingine,” amesema.
Mfanyabiashara wa mbogamboga wa soko la Kilombero Arusha, Cecilia Magembe anasema kutokana na vikwazo vingi mpakani kumekuwa na uhaba wa bidhaa hasa zilizolimwa kiikolojia.
“Biadhaa za viazi zinatoka Njombe an Nairobi tunachukua kwenye soko la Elerai, lakini kumekuwa na changamoto ongezeko la bei kwakuwa wafanyabiashara wanasema wanalipa kodi kubwa. Kwa vizazi vinavyotoka Arusha na Moshi vinakuwa na bei nafuu kwa sababu havina tozo nyingi,” amesema.
Amesema walipewa mafunzo na Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Arusha (MviwaArusha) ya kubaini mazao ya kiikolojia.
Meneja wa sokola Klmbero Arusha, Jeremiah Katemi anasema soko hilo hupokea mazao ya nafaka, samaki, nyama kutoka ndani na nje ya nchi hasa Kenya na Uganda na Rwanda.
“Kenya tunachukua sana mahindi, maembe na viazi mviringo, parachichi, limao. Rwanda tunachukua vitunguu na Uganda tunachukua malimao,” amesema.
Pia amesema Tanzania imekuwa ikisafirisha mazao ya nafaka kama mahindi na mchele na mboga na matunda kama nyanya, karoti, vitunguu kwenda nchi hizo za Afrika Mashariki.
Kwa kushirikiana na wadau wengine, Katemi anasema wameanza kuhamasisha uingizaji wa mazao ya kilimo ikolojia na tayari wameshajenga soko la bidhaa hizo eneo hilo la Kilombero.
Soko hilo lina wafanyabiashara wa maduka 330, wengine wenye meza 1,642, wafanyabiashara wa mazao ya jumla wapo zaidi ya 2,000.
Jimmy Mongi ofisa Masoko SHIWAKUTA (Shirikisho la vyama vya wakulima wadogo Tanzania) anasema wameshawafundisha wakulima na wafanyabiashara mbinu za kubaini mazao yaliyolimwa kwa njia za asili ikiwa pamoja na kutumia mbolea za asili na miti dawa iili kulinda afya za walaji.
“Kuna mbinu za kifizikia kutambua mazao yenye dawa, kama kunusa, au kimwonekano, mfano kama mboga haijatobolewa popote, basi itakuwa imetumia dawa kali. Tunaendelea kuihamasisha serikali kwenye masoko haya kuwe na vipimo vya kemikali sumu,” amesema.
Utafiti
Akitoa matokeo ya utafiti uliofanywa na Mtandao wa Uhuru wa Chakula Afrika (AFSA), mtafiti wa biashara wa Africa Kiiza, anasema utafiti unaonyesha kuwa kodi na tozo kubwa kupita kiasi kwa bidhaa za kilimo ni kikwazo cha upatikanaji wa mazao ya agroikilojia.
Ametaja kodi na tozo kuwa pamoja na ada za ukaguzi wa mazao, ushuru wa kuingiza bidhaa kutoka nje, na tozo za serikali za mitaa, zinawakatisha tamaa wafanyabiashara, kwani zinapunguza faida na mitaji waliyonayo.
“Mahojiano na wadau wa masoko ya mipakani katika maeneo ya Rusumo, Namanga, Busia na Mpondwe yalibaini kuwa kusafirisha tani 2 hadi 5 za nafaka kuvuka mipaka kunahitaji wafanyabiashara kushughulika na taasisi mbalimbali za urahisishaji biashara mipakani.
Aametoa mfano wa ada za ukaguzi na vipimo vya ubora ambazo hufikia takribani Dola 200 za Marekani (Sh495,993), sawa na karibu asilimia 10 ya thamani ya mzigo husika.
Katika mpaka wa Busia, wafanyabiashara wanawake na vijana kutoka Uganda walieleza wasiwasi wao kuhusu ushuru wa bidhaa (excise duty) unaotozwa na Kenya kwenye mayai, akisema umesababisha kusitishwa kwa usafirishaji wa mayai nje ya nchi ya Kenya.
“Mahojiano na wafanyabiashara wa masoko ya mipakani nchini Kenya pamoja na maofisa wa Wizara ya Biashara ya Kenya yalifichua kuwa, mamlaka za Tanzania zinatoza ushuru wa Sh1,000 kwa kila lita ya maziwa zinazotengenezwa Kenya (sawa na takribani Sh50 za Kenya).
“Kiwango hicho ni mara 19 ya ushuru unaotozwa kwa maziwa yanazozalishwa ndani ya Tanzania. Kodi hii imefanya maziwa kutoka Kenya kuwa ghali zaidi nchini Tanzania, na hivyo kupunguza ushindani wake katika soko la Tanzania,” amesema Kiiza.
Wakulima wajielekeza soko la ndani
Baadhi ya wakulima wanaozalisha mazao kwa mbinu za agroikolojia mkoani humo, sasa wamejikita kwenye soko la ndani kuuza mazao yao.
George Ndege ni mkulima anayeishi na kufanya kazi zake Ayalabe wilayani Karatu Mkoa wa Arusha.
Anaema ameshanufaika kwa kuzalisha kilimo cha mbogamboga kwa kutumia mbinu za agroikolojia.
Anasema mazao ya agroikolojia yana soko kubwa kwa nchi za Afrika Mashariki na kwa sasa anapata soko kutoka kwenye hoteli za kitalii zilizopo wilayani humo.
“Nimeanza kilimo tangu nikiwa kijana na sasa tumebadilisha kilimo kimekuwa cha kibiashara, ambapo hizi mboga na matunda tunauza kwenye hoteli za kitalii ambazo kwa hapa Karatu ni nyingi,” anasema.
Kwenye shamba lake, Ndege amepanda aina 13 za mboga yakiwamo maharage machanga (green beans), matango, butternuts, cornflower, garbage na nyinginezo.
“Nimejifunza kilimo hiki Mviwa Arusha ambapo mimi ni mwanacghama na ni kiongozi. Ni kilimo rahisi mno, kwa sababu hapa tunazalisha mbolea wenyewe kutokana na mabaki ya chakula cha mifugo na baada ya kuzalisha tunapeleka mabaki ya mazao kwenda kwenye mifugo.
“Nimewasaidia pia wakulima wenzangu kutumia mbinu za asili. Hapo awali ukifika kwa wafugaji unakuta mbolea inakaa kwa muda mrefu, lakini sasa mbolea ile inatumika kwa wingi,” anasema.
Kuhusu masoko, Ndege anasema alishafanya utafiti na kujihakikishia kila anacholima kinauzika.
“Kabla ya kuanza kuzalisha unakwenda kufanya utafiti wa soko, linahitaji nini? Vilevile kuna misimu ya wageni, hapa tunalenga msimu wa sikukuu kuanzia Desemba 20 hadi 25 ndio kunakuwa na wageni wengi.
“Tunafanya mpaka Machi, wageni wanaanza kupungua, tunakwenda mpaka Mei na Julai wageni wanaongezeka tena hadi Agosti. Kwa hiyo ukipanda mboga hizi lazima ulenge hii tarehe, kwani kwenye masoko ya kawaida hazinunuliki.
“Biashara hii imenisaidia sana, kwani nimejenga nyumba ya kuishi, nina usafiri na hata kule mjini nimejenga nyumba ya biashara,” anasema.
Tomothy Kimoka na mkewe wa Celestine wanalima mboga mboga na kufuga ng’ombe, mbuzi na kondoo.
Wanatumia kinyesi na mkojo wa mifugo kutengeneza bayogesi wanayoitumia kupikia.
Baadaya kutengeneza gesi hiyo kinyesi kilichochujwa gesi kinawekwa kwenye mimea kama mbolea na dawa ya kuua wadudu.