SoC02 Changamoto za Jamii, Sera, Teknolojia - ajira

SoC02 Changamoto za Jamii, Sera, Teknolojia - ajira

Stories of Change - 2022 Competition

Mt09

Member
Joined
Sep 24, 2021
Posts
26
Reaction score
68
Binadamu hupitia nyakati tofauti katika maisha yake. Kuna nyakati za mafanikio na Kuna nyakati za mkwamo. Tofauti hizi za nyakati zinaonesha jinsi maisha ya mwanadamu yanavyopata mabadiliko ya hali kiuchumi na kijamii. Mabadiliko haya ni matunda ya fikra kukabili Changamoto za maisha.

Kwa mujibu wa kamusi ya kiswahili, neno changamoto ni hali kinzani na matarajio ya mtu au jamii.

Changamoto za jamii zina wigo mpana wa utatuzi kutoka kwa wadau mbalimbali wanaounda jamii. Changamoto ni fursa ya kutumia rasilimali.

Hata hivyo, ongezeko la ukosefu wa ajira kwa vijana ni matokeo ya kufikiri vibaya kuhusu maisha. Vijana wengi wamekua na maono na matarajio binafsi zaidi kuliko maslahi na matarajio ya jamii wanazoishi. Hali hii husababisha ufinyu wa fikra na kukosekana kwa ubunifu katika maisha.

Ukweli ni kwamba tunaishi ndani ya jamii kwa kutegemeana hivyo mabadiliko ya mtu mmoja yanafungamana na mabadiliko ya wengine.

Makala hii inakusudia kuchambua hatua muhimu za kuandaa na kutekeleza shughuli ya kiuchumi kwa ufanisi.

Jambo la kwanza mpango wowote wa kujikwamua utakaoupanga lazima uende sambamba na sera ya nchi. Mipango mingi hushindwa kufikia malengo kwa sababu haiendi sambamba na sera za nchi. Hali hii huleta ugumu katika kukusanya rasilimali za utekelezaji kwa sababu ya kukosa uungwaji mkono ama idhini ya serikali. Hivyo mipango kwenda sambamba na sera ni mkakati mzuri wa utekelezaji.

Kwa mfano, kufuatia ongezeko kubwa la bajeti ya wizara ya kilimo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ambapo serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 900 kwa ajili ya kuimarisha matumizi ya sayansi na teknolojia katika shughuli za uzalishaji, kutasababisha ongezeko kubwa la mavuno. Ongezeko la mavuno maana yake ni ongezeko la mapato na matumizi ya kaya.

Hali hii itakuwa fursa ya kuanzisha miradi ya ujenzi wa miundombinu ya uhifadhi mazao pamoja na mahitaji ya vifungashio kama vile magunia.

Vilevile kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi kutokana na kuongezeka kwa mapato ya kaya kutastawisha shughuli za kibiashara na hivyo kuongeza fursa za ajira.

Jambo la pili ni kufanya utafiti wa kina kwa kukusanya taarifa toka vyanzo mbalimbali kuhusu mahitaji na hali halisi ya changamoto na fursa zilizopo kulingana na mipango ya serikali.

Fanya mahojiano ya mmoja mmoja au vikundi vichache ama tengeneza dodoso la kupata taarifa na takwimu kwa watu wachache utakavyochagua kuwakilisha jamii nzima. Baada ya kupata mahitaji yao na uhalisia shirikisha katika kutafuta ufumbuzi unaoendana na mahitaji yao kwa teknolojia watakayoimudu lakini itakayoleta tija na ufanisi. Hii pia ni fursa ya ubunifu wa teknolojia mpya itakayochochea ajira.

Lakini mradi hautoweza kufanikiwa pasipo jamii kuwa na ufahamu nao. Hivyo, jambo la tatu utakalolifanya ni kutoa matokeo ya utafiti kwa jamii nzima Ili kuhamasisha wanajamii juu ya umuhimu wa mabadiliko. Hii itaweza kuwapa ufahamu wa haki na wajibu wao katika kutatua changamoto zinazowakabili lakini pia kuweza kutengeneza mahusiano ya karibu na jamii ambayo ni mtaji jamii.

Jambo la nne weka ramani ya utekelezaji kimaandishi kwa kuweka taarifa za fursa na mgawanyo wa rasilimali, jinsi zitakavyopatikana na zitakavyotumika. Hii ni muhimu ili kujenga ushawishi kutoka kwa wadau mbalimbali kuweza kushiriki utekelezaji. Tumia wataalamu kutengeneza andiko lako, lakini vilevile pitia katika mitandao kuona namna ya uandaaji andiko linalokidhi mahitaji ya kitaalamu. Zipo makala nyingi mitandaoni zikielezea namna ya kutengeneza maandiko ya miradi, tumia fursa hii TEHAMA (Teknolojia ya Habari na Mawasiliano) Ili kujipatia utaalamu Ili Kupunguza gharama za ushauri.

Jambo la tano andaa mpango kazi kuonesha mtiririko wa majukumu kulingana na muda. Ainisha aina gani ya shughuli itaanza na itachukua muda gani kwa rasilimali zipi ikiwemo wanaohusika kuzifanya. Hii itakusaidia katika usimamizi, ufuatiliaji wa maendeleo ya mradi pamoja na tathmini ya utekelezaji.

Jambo la sita baada ya kuhamasisha jamii ni kuhalalisha mpango kisheria. Hapa inahusu utengenezaji wa muundo wa usimamizi wa shughuli za mradi. Muundo huu utaundwa na taasisi itakayosajiliwa kwa mujibu wa sheria. Hapa sasa ndipo faida ya kuhamasisha inapoonekana. Kwa mujibu wa sheria usajili wa taasisi unahitaji uwepo wa baadhi ya rasilimali kama watu, vifaa na miundombinu ya kiofisi. Jamii yenye ufahamu wa kutosha ni rahisi kutoa ushirikiano katika kukamilisha zoezi hilo wanapofahamu ni hatima ya wao kuwa sehemu ya huo mchakato. Hii itakuwezesha kupata ulinzi wa kisheria utakaokuwezesha kufanya mikataba mbalimbali kisheria na kuweza kufikia mitaji, teknolojia na masoko.

Jambo la saba ni utafutaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya teknolojia mbalimbali kama zilivyoainishwa. Upatikanaji wa fedha unaotegemea na umuhimu wa mradi kwa jamii, uhalisia, uhalali wa kiserikali na kisheria lakini pia mwamko wa jamii katika kutekeleza ama kushiriki kwa ajili ya kuhakikisha usalama wa rasilimali zitakazoelekezwa kwenye mradi ili kupata matokeo tarajiwa.

Jambo la nane ni utekelezaji. Hapa inahusisha uwekaji katika vitendo pamoja na ufuatiliaji wa yale yote yaliyoanishwa katika andiko kwa kufanya mikataba ya ajira na manunuzi ya rasilimali mbalimbali za utekelezaji pamoja na usimamizi na ufuatiliaji wa mpango kazi.

Jambo la mwisho ni tathmini ya utekelezaji. Hii ni muhimu ili kuona mafanikio na mapungufu ya mradi/mpango kwa nia ya kufanya maboresho kuendelea na mradi ama kuachana na mradi.
Hapa Kuna mengi ya kuangaliwa, kama vile kupungua kwa changamoto, mabidliko katika sera, sheria na uongozi ni moja ya mambo yanayoweza kuathiri shughuli za mradi kutokana na kuwa na nguvu za ushawishi na maamuzi yenye mamlaka.

Hivyo basi ni muhimu sana kufahamu muelekeo wa serikali Ili kutambua mtiririko wa athari zitakazotokea kwa jamii kutokana na kutekeleza mpango wowote wa kitaifa. Hii itakusaidia kubaini fursa mbalimbali zilizopo kwenye mnyororo wa thamani. Lengo ni kukabiliana na changamoto ya upatikanaji masoko kunakosababishwa na kufanana kwa shughuli za kiuchumi.



 
Upvote 1
Karibuni kwenye mjadala kuhusu mada hii kwa maoni, ushauri Ili kujenga uelewa wa pamoja kama jamii.

Asanteni.
 
Back
Top Bottom