DogoWaNjombe
JF-Expert Member
- Feb 7, 2022
- 3,284
- 7,708
Cheyo, maarufu Mzee Mapesa, amewasili ukumbini hapo saa sita mchana akiwa amevalia suti ya buluu, anatembelea mkongojo, huku akisaidiwa na watu wawili.
Akihutubia wajumbe, Cheyo amesema kama si umuhimu wa mkutano huo asingetoka kitandani.
“Kama isingekuwa kikao hiki, nisingeondoka kitandani. Lakini kwa sababu UDP ni chama cha upendo, pamoja daima imebidi hata kwa mkongojo nije,” amesema Cheo.
Amesema amefurahishwa na wingi wa wajumbe licha ya changamoto za kifedha zinazokikabili chama hicho, akibainisha kuwa baadhi ya wanachama wamejitolea kugharamia nauli zao ili kushiriki mkutano mkuu huo muhimu.
Kuhusu malengo ya mkutano huo, Cheyo amesema agenda kuu ni kutimiza takwa la kisheria la kumuidhinisha mgombea urais wa chama na mgombea mwenza, ambapo kamati kuu itathibitisha jina, kabla ya kuwasilishwa kwa mkutano mkuu maalumu kwa ajili ya kuridhiwa.
Aidha, amewashukuru wawakilishi wa vyama vingine vya siasa walioitikia mwaliko, akisema kuwa hali hiyo ni ishara ya mshikamano.
“Msituchoke tukiimba wimbo huu wa ‘upendo, daima, pamoja,’ kwa sababu nchi hii ni yetu. Hatuna mahali pengine pa kukimbilia. Tanzania tuendelee kuiweka salama na yenye amani,” amesema kiongozi huyo.
Mbali na wajumbe wa UDP, mkutano huo unahudhuriwa pia na wawakilishi kutoka vyama vya UPDP, Ada-Tadea, Demokrasia Makini, SAU na NCCR-Mageuzi.
Baada ya ufunguzi wa mkutano, wajumbe wametolewa nje ili kuruhusu kikao cha kamati kuu kuendelea.
Baadaye, mkutano mkuu utaendelea kwa ajili ya kutajiwa rasmi jina la mgombea urais na mgombea mwenza wa chama hicho.
Stori: Mwananchi