China itaendelea kuwa fursa muhimu ya diplomasia ya uchumi kwa Tanzania

China itaendelea kuwa fursa muhimu ya diplomasia ya uchumi kwa Tanzania

ldleo

JF-Expert Member
Joined
Jan 9, 2010
Posts
1,116
Reaction score
1,121
Fadhili Mpunji

VCG111360573969.jpg


Hivi karibuni balozi wa Tanzania nchini China Balozi Mbelwa Kairuki alipohojiwa kwenye kipindi cha Dakika 45 cha kituo cha televisheni cha ITV, alifafanua vizuri kuhusu fursa inazotoa China kwa Tanzania, iwe ni katika sekta ya viwanda, kilimo, biashara na hata uwekezaji. Baadhi ya mifano aliyotoa Balozi Kairuki ni fursa ya soko la maharage ya soya, msaada unaotolewa na ubalozi wa Tanzania nchini China kwa watu wanaopenda kuuza na kununua bidhaa nchini China, na hata kuhusu uagizaji wa bidhaa ndogo ndogo za mtaji zenye teknolojia ya juu kiasi zinazoweza kusaidia kuongeza tija kwenye shughuli za kujiajiri na hata uzalishaji.

Kimsingi Balozi Kairuki alikuwa anazungumzia umuhimu wa diplomasia ya uchumi na manufaa kwa nchi yetu, na jinsi ubalozi wa Tanzania nchini China unavyotekeleza kivitendo diplomasia hiyo. Ukweli ni kwamba mahusiano mazuri kwenye diplomasia ya kisiasa ndio msingi wa diplomasia ya uchumi. Kutokana na msingi mzuri wa mahusiano ya kidiplomasia uliowekwa na baba wa taifa mwalimu Julius Nyerere, na juhudi kubwa zinazofanywa na Balozi Kairuki na maofisa wa ubalozi, sera ya diplomasia ya kiuchumi ya Tanzania kwa China inaweza kutekelezeka kwa ufanisi zaidi hata kuliko ilivyo sasa.

Inawezekana kuwa baadhi ya watu hawaelewi vya kutosha ukubwa wa fursa za kiuchumi zilizopo nchini China. Ukweli nchi yetu ikiwa na uhusiano wa kina na mkoa mmoja tu wa China au mji mmoja tu wa China inawezekana changamoto za soko kwa mazao yetu mengi ya kilimo itakuwa imetatuliwa. Mkoa wa Guangdong peke yake una GDP ya dola za kimarekani Trilioni 1.7 na kuziacha nyuma nchi nyingi za Ulaya zilizoendelea (mbali na nchi nne tu za Ulaya ambazo ni Ujerumani dola trilioni 4.3, Ufaransa 3.1, Uingereza dola trilioni 3.1 na Italia dola trilioni 2.7). Miji mikubwa ya China Shanghai wenye GDP ya zaidi bilioni 608 dola za kimarekani, au Beijing wenye GDP ya zaidi ya bilioni 458, na idadi kubwa ya watu wa tabaka la kati ambao uwezo wao wa matumizi kila mwaka unaongezeka.

Kwenye sekta ya kilimo, kwa sasa Tanzania ni moja ya nchi za Afrika zinazoruhusiwa kuuza karibu aina zote za mazao ya kilimo kwenye soko la China, kinachotakiwa ni kuangalia uwezo wa uzalishaji wa ndani ili kukidhi vigezo na kuweka makubaliano ya karantini, kama ilivyo kwenye maharage ya soya na muhogo mkavu. Kutokana na uhusiano mzuri wa kidiplomasia kati ya China na Tanzania, uwezekano wa ushirikiano kwenye sekta nyingine za uchumi kama utalii, madini, ufugaji, uvuvi nk ni mkubwa.

Jambo muhimu linalotakiwa kukumbukwa ni kuwa, kwa sasa ladha za wachina kuhusu vyakula zinabadilika kuendana na uwezo wao wa kifedha. Pamoja na kuwa China inajulikana kama nchi ya chai, idadi ya vijana wanaokunywa kahawa mijini nchini China inaongezeka kila mwaka, na idadi ya watu wanaopenda matunda ya kitropiki pia inaongezeka kila siku. Tukichukulia mji wa Beijing peke yake wenye GDP ya karibu dola za Marekani bilioni 460 na wakazi zaidi ya milioni 20, tunaweza kuuza kahawa yetu yote na matunda yetu yote kwa mji huo peke yake.

Kwa baadhi ya watu kumekuwa na kitu kama dosari fulani kwenye mitazamo yao kuhusu China, hasa kutokana upotoshaji kwenye vyombo vya habari vya nchi za magharibi. Lakini kinachosikitisha ni kwamba ukiangalia ushirikiano wa kiuchumi kati ya China na nchi zinazoikosoa China mara kwa mara, utaona kuwa ni mkubwa na nchi hizo zinanufaika zaidi kiuchumi na China kwa kuuza ndege, magari, mitambo, matunda na karibu kila bidhaa wanayoweza kuiuza. Kimsingi wao wananufaika zaidi kuliko hata nchi yetu yenye urafiki mkubwa na inayoiunga mkono China.

Serikali yetu imekuwa inasisitiza mara kwa mara mabalozi wetu watafute fursa na kutekeleza kwa makini maagizo kuhusu diplomasia ya uchumi. Tusisahau kuwa kazi za balozi zetu ni kufungua milango ya fursa, jukumu la watanzania ni kuhakikisha kuwa tunatumia fursa hizo. Inasikitisha pale tunapoambiwa tuna zabuni ya kuuza maharage ya soya, lakini tunashindwa kutumia fursa kwa sababu uzalishaji wetu ni mdogo wakati asilimia 70 ya ardhi ya Tanzania inaweza kuzalisha zao hilo. Tusipotumia fursa kama hizo ipasavyo, juhudi za serikali kututafutia fursa zitapotea bure, na sera ya diplomasia ya uchumi itabaki kuwa kauli tu.
 
Back
Top Bottom