Kongamano la pili la Amani na Usalama kati ya China na Afrika limefanyika hivi karibuni kwa njia ya mtandao. Katika barua yake ya pongezi kwa kongamano hilo, Rais Xi Jinping wa China ameeleza kwamba anatilia maanani sana ushirikiano wa amani na usalama kati ya China na Afrika, na kupendekeza kufuata wazo endelevu la pamoja, linalozingatia ushirikiano kuhusu suala la amani na usalama, na kujenga jumuiya ya China na Afrika yenye hatma ya pamoja katika enzi mpya.
Kongamano hilo lenye kaulimbiu ya “Kuimarisha Mshikamano na Ushirikiano ili kufikia Usalama wa Pamoja”, limeshirikisha viongozi 50 wa ngazi ya mawaziri wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika na nchi nyingine za Afrika. Washiriki hao wamesema barua ya pongezi ya Rais Xi Jinping inaonyesha kuwa China inatilia maanani sana uhusiano na Afrika katika suala la usalama, na China ni rafiki, ndugu na mwezi mzuri wa kutegemewa. Wameongeza kuwa nchi za Afrika zinapenda kuimarisha ushirikiano na China, na kutoa mchango kwa ajili ya ujenzi wa jumuiya yenye hatma ya pamoja.
China na Afrika ni marafiki wakubwa na wenzi wazuri wanaosaidiana, na kutimiza amani na usalama wa kudumu ni matarajio ya pamoja ya watu wa China na Afrika. Katika suala hilo, China daima inaungana mkono na ndugu wa Afrika. Takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya walinda amani wa China wametumwa barani Afrika, na hadi sasa zaidi ya askari 30,000 wa China wametekeleza majukumu katika maeneo 17 barani Afrika. China inaunga mkono nchi za Afrika kuimarisha utulivu na kuongeza uwezo wa kulinda amani, na kuunga mkono Afrika kutatua matatizo yake kwa njia za Kiafrika. China inatekeleza mapendekezo ya maendeleo ya kimataifa kwa hatua madhubuti, kuunganisha mipango yake ya maendeleo na mikakati ya maendeleo ya Afrika, ili kuharakisha utekelezaji wa Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa ya 2030, na kuhimiza usalama endelevu kupitia maendeleo endelevu.
Katika Mkutano wa Nane wa Mawaziri wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika mwaka jana, China na Afrika zilitangaza utekelezaji wa pamoja wa “Miradi Tisa”, ukiwemo mradi wa amani na usalama. Kwa mujibu wa mpango wa mradi huo, China itatekeleza miradi 10 ya ushirikiano katika nyanja ya amani na usalama, kuendelea kutekeleza usaidizi wa kijeshi kwa Umoja wa Afrika, kuunga mkono juhudi za nchi za Afrika za kudumisha usalama wa kikanda na kukabiliana na ugaidi, kutoa mafunzo, na kufanya ushirikiano wa udhibiti wa silaha nyepesi na vikosi vya kulinda amani vya China na Afrika.
Mafanikio ya kudumisha amani na usalama ndio msingi wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii barani Afrika na ustawi wa watu wa bara hilo, na yana umuhimu mkubwa kwa amani na maendeleo ya dunia nzima, ikiwemo China. China itashirikiana na Afrika kuzidisha ushirikiano katika nyanja ya amani na usalama, na kujenga jumuiya ya China na Afrika yenye hatma ya pamoja katika enzi mpya.