Leo China inaadhimisha miaka 50 tangu irejeshewe kiti chake halali kwenye Umoja wa Mataifa. China inaadhimisha siku hii wakati ikikumbuka safari yake hadi kurudishiwa kiti chake, na mchango iliotoa kwa Umoja huo na uwajibikaji iliounesha.
Ikumbukukwe kuwa Umoja wa Mataifa ulianzishwa kwa lengo la kudumisha amani duniani, na kuhimiza lengo la usalama wa pamoja. Lakini malengo yake yaliendelea kupanuliwa kadiri siku zilivyokuwa zikisonga mbele, na kuhusisha afya, kilimo, utamaduni, mazingira na maeneo mengine. Nguvu ya Umoja wa Mataifa katika kushughulikia mambo hayo, inatokana na ushirikiano mzuri wa nchi wanachama, hasa nchi kubwa na zenye nguvu ambazo ni wajumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
China iliporudishiwa kiti chake halali kwenye Umoja wa Mataifa, na hasa mjumbe wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ilitambua kuwa ukubwa unaendana na wajibu, na katika kipindi chote imekuwa ikijitahidi kuonyesha uwajibikaji. Tukiangalia mchango wa China kwenye shughuli za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa, tunaona kuwa China iko kwenye nafasi za mbele kwenye kutoa msaada wa fedha na vifaa, tukiangalia kwenye upande wa maendeleo tunaweza kuona China imetimiza ajenda ya maendeleo kuelekea mwaka 2030 mapema kwa miaka 10 kuliko nchi nyingine, na kufanikiwa kupunguza umaskini kwa asilimia 70.
China pia imekuwa inajitahidi kuhimiza maendeleo kwa nchi nyingine duniani kwa kuongeza bajeti za msaada wa fedha na vifaa, kuhamisha teknolojia na ujuzi, na kutoa misaada mbalimbali kwa zaidi ya nchi 160 zinazoendelea duniani.
Hata kwenye changamoto za dunia kama vile mabadiliko ya tabia nchi, China imekuwa mstari wa mbele kuchukua hatua ndani ya nchi kwa kupunguza utoaji wa hewa ya ukaa na hata kupanda miti, na pia kuzisaidia nchi nyingine kufikia malengo ya kupunguza utoaji wa hewa ya ukaa. Na hivi karibuni pia dunia imeshuhudia udhati wa China, ilipoamua kuongoza ushirikiano wa kupambana na COVID-19, na kutangaza kuwa chanjo ya COVID-19 iliyotengenezwa na China ni bidhaa ya umma ya dunia, na imeshiriki kikamilifu kwenye mpango wa COVAX.
Wakati China imekuwa ikijitahidi kuimarisha Umoja wa Mataifa na hata kulinda utaratibu wa pande nyingi, Marekani imekuwa ikifanya vitendo ambavyo vinayumbisha Umoja huo na hata kutishia umuhimu wake duniani. Kuna mifano mingi inayoonyesha kuwa Marekani imekuwa ikiuhujumu, kuudhoofisha au hata kuuburuta Umoja wa Mataifa kwa maslahi yake binafsi.
Mwanzo wakati Umoja wa Mataifa unaanzishwa, Marekani ilionekana kuwa na athari nzuri duniani, na kweli ilijitahidi kufuata sheria na kusimamia kanuni za Umoja wa Mataifa. Hatuwezi kupuuza mchango uliotolewa na Marekani kwa maendeleo ya dunia, lakini baadaye hasa katika kipindi cha vita baridi ya Marekani ilianza kubadilika na kutia shaka, hasa kutokana na vitendo vyake vya uingiliaji wa mambo ya ndani ya nchi nyingine, iwe ni kwa kuzivamia nchi hizo au kuchochea na kuunga mkono.
Ikumbukwe kuwa baada ya Umoja wa Mataifa kukataa kutoa idhini kwa serikali ya Rais George W. Bush wa Marekani kuishambulia Iraq baada ya kukosekana kwa ushahidi kuwa nchi hiyo ina silaha za kemikali, Marekani ilizishawishi baadhi ya nchi kuivamia nchi hiyo na kuiondoa serikali yake. Ilianzisha ilichokiita “ushirika wa waliokuwa tayari” (Coalition of the willing), na kutumia ujanja huo kuonekana kama sio uamuzi wa peke yake (unilateral action) bali ni wa “pande nyingi”. Lakini hata alipoingia madarakani Rais Donald Trump, yeye binafsi aliamua kuiondoa Marekani kwenye Shirika la Afya Duniani (WHO) na kuzuia kutoa ada ya Marekani kwa shirika hilo, na zaidi ya hapo pia alihujumu juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi zinazoongozwa na Umoja wa Mataifa kupitia Makubaliano ya Paris.
Tangu China irudishiwe kiti chake halali kwenye Umoja wa Mataifa imekuwa muungaji mkono na mfuataji mkubwa wa sheria na kanuni za Umoja wa Mataifa, licha ya kuwa kanuni hizo zilitungwa wakati bado China haijarudishiwa kiti chake halali. Lakini Marekani ambayo ndio ilikuwa kinara kwenye utungaji wa sheria na kanuni hizo, imekuwa na desturi ya kuchukua hatua za upande mmoja (unilateral actions) na kukiuka pale inapoona kuwa sheria hizo zinaondoa urahisi kufanya mambo yake, kitendo ambacho kinatafsiriwa na baadhi ya wachambuzi kama ni kuhamisha goli (moving goal post).
Hali halisi ya dunia ya sasa imebadilika sana ikilinganishwa na kipindi baada ya vita ya pili ya dunia ulipoanzishwa Umoja wa Mataifa, na hasa kipindi baada ya kwisha kwa vita baridi. Pamoja na ukweli kwamba Marekani ndio nchi pekee yenye nguvu zaidi duniani (Superpower), kimsingi dunia ya sasa imekuwa ni dunia ya ncha nyingi na imekuwa ya utatanishi zaidi. Marekani peke yake haiwezi kutatua changamoto zote bila kushirikiana na wengine.