Ushirikiano kati ya China na Afrika katika elimu na mafunzo ya ufundi stadi ni muhimu sana na kwa sasa unaonekana kudumisha kasi nzuri, vilevile umeendelea kustawi kwa pande zote. Kupitia ushirikiano huu vijana wengi wa Afrika wananufaika katika masuala ya ufadhili wa masomo na kuja kusoma nchini China katika vyuo vikuu na vyuo vya ufundi, ambapo jambo hili linawezesha maendeleo ya mtaji wa binadamu barani Afrika.
China ikiwa mshirika mkubwa wa Afrika ambaye anategemeka, mbali na kuhakikisha kwamba katika ushirikiano huu Afrika inakuwa na maendeleo makubwa ya viwanda, pia inajitahidi kuboresha ujuzi wa vijana wa Afrika katika matumizi ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati, kwani hakuna asiyejua kwamba uwepo wa viwanda bila ya wataalamu, ni sawa na kununua gari bila dereva ama teknolojia ya kuiendesha na itaendelea kuwa pambo tu bandani kwake. Elimu na mafunzo ya ufundi stadi ni muhimu kwa bara la Afrika kuingia katika enzi ya nne ya viwanda.
Ili kuchochea kasi ya ujenzi wa uchumi wa viwanda, Tanzania imedhamiria kuimarisha zaidi ushirikiano wake na China katika kuendeleza elimu na mafunzo ya ufundi stadi (TVET) na kuweza kukidhi viwango vya ndani na kimataifa kwa wahitimu wake. Hatua hii itainufaisha zaidi Tanzania hasa katika kuboresha mafunzo, wakati huohuo ikitiliwa maanani kwamba ili nchi iweze kuendeleza uwekezaji wake basi itahitaji nguvu kazi wenye ujuzi, pamoja na miradi ya kimkakati.
Ikiwa sasa Tanzania ina taasisi 475 za ufundi, vyuo vya ufundi stadi 835 na shule za sekondari za ufundi stadi 96, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, James Mdoe, alitilia mkazo kwa kusema China ni nchi ya kupigiwa mfano yenye mifumo imara ya TVET ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya haraka ya uchumi wa Tanzania. Kwa maana hiyo anaona Tanzania itanufaika pakubwa kwa kuimarisha ushirikiano na vyuo vya TVET vya China.
Wakati inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2030, karibu kijana mmoja kati ya wawili duniani atakuwa Muafrika, mabadiliko ya idadi ya watu yanatia wasiwasi kwasababu hayalingani na ujuzi muhimu kwa Waafrika kuweza kushiriki kikamilifu katika mchakato wa mabadiliko ya nguvu kazi.
Wasiwasi huu umeipelekea China kufanya maamuzi ya busara ambapo katika Mazungumzo ya Viongozi wa China na Afrika yaliyofanyika Agosti mwaka jana mjini Johannesburg, Afrika Kusini, China ilitangaza kwamba itazindua Mpango wa Ushirikiano kati ya China na Afrika unaohusu Kukuza Vipaji vya Waafrika kila mwaka, ukilenga kutoa mafunzo kwa walimu 500 wa ngazi ya juu wa vyuo vya ufundi stadi, na wafanyakazi 10,000 wa ufundi. Mpango huu utaziba pengo la ujuzi wa kiufundi kupitia elimu, utafiti, na mafunzo na kuwezesha nchi za Afrika kujenga viwanda vya siku zijazo.
Mbali na China kutoa mafunzo ya ufundi stadi, pia inajenga na kufungua vituo vya kisasa vya ufundi katika nchi za Afrika. Mwaka jana Angola ilikuwa miongoni mwa nchi zilizobahatika kwenye ushirikiano huu, ambapo ilizindua Kituo Jumuishi cha Mafunzo ya Kiteknolojia katika mji wa Huambo, kilichofadhiliwa na China. Kituo hicho chenye ukubwa wa mita za mraba 20,000 kina maabara 30 na karakana sita zenye roboti, pia kinatumia sayansi ya kompyuta na kinafanya ukarabati wa magari. Katika awamu ya kwanza, China inatoa mafunzo kwa watu 2,400 kila mwaka ambapo walimu wote wamepatiwa mafunzo nchini China.
Ikizingatiwa kuwa sasa mafunzo ya ufundi stadi na ukuzaji vipaji yamekuwa maeneo muhimu zaidi ya ushirikiano kati ya China na Afrika, ni matarajio ya kila mtu kuona Afrika ikinufaika sana na utandawazi na kuharakisha ukuaji wa viwanda vyake ambavyo hatimaye vitaleta mageuzi ya kijamii na kiuchumi barani Afrika.