Yoyo Zhou
Senior Member
- Jun 16, 2020
- 199
- 322
Afrika ni bara linaloathiriwa zaidi na UKIMWI. Hivi karibuni, UNAIDS ilitoa ripoti ikisema kupungua kwa misaada ya kimataifa ni tishio kwa juhudi za kuzuia na kudhibiti UKIMWI duniani. Kinyume na hali hii, China inaendelea na msaada wake kwa Afrika katika suala hilo.
Katika bara la Afrika, UKIMWI bado ni moja ya changamoto kubwa zaidi zinazotishia afya ya umma. Kulingana na takwimu za UNAIDS, nchi za Afrika zilizoko Kusini mwa Jangwa la Sahara zinachangia zaidi ya theluthi mbili katika idadi ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI duniani.
Ili kusaidia Afrika kukabiliana na changamoto hiyo sugu, China imebeba jukumu muhimu kwa miaka mingi katika kuzisaidia nchi za Afrika kukabiliana na UKIMWI kupitia mfumo wake wa kipekee wa ushirikiano.
Mwezi uliopita, Ubalozi wa China nchini Afrika Kusini ulizinduzi mradi wa kuunga mkono kinga na udhibiti wa UKIMWI nchini Afrika Kusini, ambayo ni moja ya nchi zenye idadi kubwa zaidi ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI duniani.
Takwimu zinaonesha kwamba takriban watu milioni 8 ambao ni asilimia 13.9 ya idadi ya watu nchini humo wanaishi na virusi vya UKIMWI, huku vijana wenye umri wa miaka kati ya 15 hadi 24 wakichukua theluthi moja ya maambukizi mapya.
Kwa miaka mingi, juhudi za kuzuia na kudhibiti UKIMWI nchini Afrika Kusini zimetegemea msaada wa Marekani. Lakini mapema mwaka huu, Marekani ilipunguza ghafla na kwa kiasi kikubwa msaada huo, na kuleta athari kubwa kwa Afrika Kusini.
Mradi huo wa msaada wa China utaendelea kwa miaka miwili, na unalenga kuimarisha huduma za kuzuia virusi vya UKIMWI na kupunguza madhara, hasa kutoa huduma za kuzuia UKIMWI kwa vijana katika shule, na huduma za kupunguza madhara kwa watu wanaojidunga dawa za kulevya.
Kwa kawaida, msaada wa kimataifa kwa Afrika katika kukabiliana na UKIMWI haswa ni utoaji wa dawa, na miradi ya matibabu ya muda mfupi. Lakini China imechukua mbinu ya ushirikiano inayosisitiza ufanisi wa muda mrefu na ujenzi wa uwezo wa ndani.
Tangu kuanzishwa kwa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika mwaka 2000, China si kama tu imetoa idadi kubwa ya dawa za kupunguza makali ya VVU na vifaa vya uchunguzi, bali pia imetuma timu za matibabu na wataalamu wa afya barani Afrika ili kusaidia kuanzisha mifumo ya kinga na udhibiti wa UKIMWI.
Ushirikiano kati ya China na Tanzania ni mfano bora. China sio tu inatoa dawa na vifaa, lakini pia inasaidia Tanzania katika kuanzisha maabara ya kitaifa ya kupima virusi vya UKIMWI, kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa afya, na kusaidia programu za kinga na uingiliaji kati kwa vikundi vilivyo hatarini zaidi.
Wakati huo huo, watafiti wa China wanashirikiana na wenzao wa Afrika kuunda mikakati ya kinga inayolingana na mazingira maalumu ya nchi za Afrika. Kwa mfano, nchini Malawi, wanasayansi wa China na nchi hiyo kwa pamoja wamefanya utafiti ili kuchunguza jinsi ya kuboresha programu za kuzuia maambukizi ya virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama hadi mtoto.