Ikilinganishwa na mabara mengine hasa yale zilizoendelea, Afrika imetoa kiwango kidogo zaidi cha hewa inayoongeza joto duniani, lakini imekuwa moja ya maeneo yaliyoathiriwa zaidi na majanga yaliyoletwa na mabadiliko ya tabianchi katika miaka ya hivi karibuni. Tangu mwaka 2019, Afrika imekumbwa na majanga mengi makubwa ya asili, ikiwemo kimbunga “Idai”, nzige wa jangwani, ukame mkali katika kanda ya Sahel, mafuriko makubwa kaskazini mwa Bonde la Ufa, na ukame mkali katika Pembe ya Afrika. Kushughulikia mabadiliko ya tabianchi kumekuwa kipaumbele cha juu zaidi kwa Afrika kuhakikisha usalama na maendeleo.
China na nchi za Afrika zote ni nchi zinazoendelea, na ni jumuiya yenye hatma ya pamoja. Mkutano wa 8 wa Mawaziri wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika Novemba mwaka 2021 ulipitisha “Azimio la Ushirikiano kati ya China na Afrika katika Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi”, na kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya pande hizo mbili katika kushughulikia changamoto hiyo. Katika miaka ya hivi karibuni, ushirikiano huo umeimarika na unaendelea kuimarishwa siku hadi siku.
Kwanza, kupunguza matishio ya majanga kutokana na mabadiliko ya tabianchi ni sehemu ya kimsingi ya ushirikiano kati ya China na Afrika. Tangu mwaka 2013, China imeimarisha kiwango cha ushirikiano na Afrika katika suala la hali ya hewa, na kusaidia kujenga vituo vya utabiri wa hali ya hewa nchini Comoro, Kenya, Zimbabwe, Namibia na nchi nyingine nyingi. Wakati huo huo China pia imetoa data za uchunguzi wa satelaiti ya hali ya hewa ya “Fengyun-3” kwa nchi za Afrika. Katika mchakato wa kushiriki katika mradi wa “Ukuta Mkubwa wa Kijani”, unaojulikana kama mradi mkubwa zaidi wa kiikolojia barani Afrika, China ilitoa uzoefu wake wa kupanda miti, hasa katika maeneo ya jangwa huko kaskazini-magharibi mwa China kwa ajili ya kuzuia upepo na mchanga, na kuchangia kupanda misitu ya kuzuia upepo nchini Burkina Faso, Mauritania, na Niger.
Pili, kushughulikia na kudhibiti majanga ya pili kutokana na mabadiliko ya tabianchi ni suala muhimu lingine la ushirikiano kati ya China na Afrika. Kuimarisha usambazaji wa chakula na nishati ni lengo muhimu la Afrika katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. China imedumisha ushirikiano wa karibu na Afrika katika sekta za kilimo ikiwemo mbegu, ufugaji, udhibiti wa wadudu, upandikizaji na usindikaji wa mazao, na imejenga vituo kadhaa vya vielelezo vya kilimo barani Afrika, na kupata matokeo mazuri. Katika miaka ya hivi karibuni, China imeeneza teknolojia yake ya mpunga chotara nchini Madagaska, Nigeria, Guinea ya Ikweta, Uganda na nchi nyingine, na kuongeza mavuno ya nafaka kwa mara 1 hadi 3.
Ugavi wa nishati safi na ya bei nafuu ni nyenzo muhimu kwa nchi za Afrika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Ushirikiano kati ya China na Afrika umesaidia nchi za Afrika kugeuza maliasili kuwa nishati halisi. Kituo cha umeme wa nishati ya maji katika Mto Blue Nile kitaifanya Ethiopia kujitosheleza kwa umeme. Kituo cha Umeme wa nishati ya jua cha Garissa nchini Kenya na kituo cha umeme wa nishati ya upepo cha De'a nchini Afrika Kusini vinetoa nishati ya kutosha kwa mahitaji ya uzalishaji na maisha ya maelfu ya wakazi wa maeneo hayo.
Kushughulikia mabadiliko ya tabianchi ni changamoto inayokabili binadamu wote, na hakuna eneo au nchi yoyote inayoweza kushinda changamoto hiyo peke yake. Ushirikiano kati ya China na Afrika umesaidia Afrika katika kukabiliana na changamoto hiyo, na pia umeweka mfano mzuri kwa ushirikiano wa kimataifa.