Hivi karibuni mkutano wa uratibu wa utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya China na Afrika kwenye mkutano wa 8 wa mawaziri wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika, ulifanyika kwa njia ya video chini ya uenyekiti wa waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Wang Yi. Mkutano huo ulijadili kwa kina na kufikia makubaliano kuhusu mambo kadhaa yanayohusu uratibu wa ushirikiano kati ya China na nchi moja moja ya Afrika na nchi za Afrika kwa ujumla wake.
Kwenye mkutano uliofanyika mwezi Novemba mjini Dakar,Senegal, baadhi ya ahadi zilizotolewa na China ni kutoa dola bilioni 10 za kimarekani kwa taasisi mbalimbali za fedha za nchi za Afrika. Kwenye mapitio yaliyofanyika kwenye mkutano huo imeonekana kuwa tayari dola bilioni 3 zimetolewa, na kati ya hizo dola bilioni 2.5 zimewekezwa kwenye miradi ya kipaumbele inayogusa moja kwa moja maisha ya watu wa kawaida wa Afrika.
Ahadi nyingine iliyotolewa na China ni kuwa itahimiza uagizaji wa mazao ya kilimo kutoka nchi za Afrika. Kwenye mapitio hayo Waziri Wang alitoa takwimu zinazoonesha kuwa katika kipindi cha miezi saba iliyopita thamani ya uagizaji wa bidhaa za kilimo kutoka China imefikia dola za kimarekani bilioni 70, na makampuni ya China yamewekeza zaidi ya dola za kimarekani bilioni 2.17 sehemu ya hizo zikiwa ni kuhimiza uzalishaji na usafirishaji wa bidhaa za kilimo kwenye soko la China.
Mbali na hayo Waziri Wang alitangaza kuwa China itafuta madeni 23 yasiyo na riba kwa nchi 17 za Afrika, na haya ni madeni ambayo muda wake wa kuanza kulipa ulianza 2021. Suala la madeni limekuwa moja ya maeneo yanayotumiwa na vyombo vya habari vya nchi za magharibi kuupaka matope uhusiano kati ya China na nchi za Afrika, kwa kupotosha na hata kutia chumvi kuhusu baadhi ya takwimu zinahusu mikopo ya maendeleo inayotolewa na taasisi za fedha za China kwa nchi za Afrika.
Ukweli ni kwamba nchi za Afrika zinapochagua kukopa kutoka kwa China kwa masharti nafuu, wakopeshaji wa magharibi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakitoa za riba kubwa kwa nchi za Afrika wanakosa fursa. Hiki ndio kinawafanya waikosoe China. Ajabu nyingine ni kuwa kila China inapotangaza kuzifutia madeni nchi za Afrika, habari hii haionekani kwenye vyombo vya habari vya nchi za magharibi. Sababu kubwa ni kwamba kwao ni kama aibu, kwa sababu wao pia wanajua kuwa wanatakiwa kufanya hivyo, lakini hawafanyi hivyo kwa sababu mikopo yao kimsingi ni biashara inayotakiwa kuwaletea faida kubwa na sio nyenzo ya kuhimiza maendeleo au kuondoa umaskini barani Afrika.
Pamoja na kujadili mambo yanayohusu uhusiano kati ya China na Afrika, mkutano huo wa uratibu pia ulijadili hali ya kimataifa kwa sasa. Ni wazi kubwa mgogoro wa Ukraine umekuwa na athari hasi kwenye uchumi wa dunia na siasa za kimataifa. Lakini pia ziara ambazo zinafanywa na wanasiasa wa Marekani kisiwani Taiwan pia zimekuwa na athari hasi kwenye diplomasia ya kimataifa.
Taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya mkutano huo imesema bila kujali hali ya sasa ya kimataifa, China na Afrika zitaendelea kuhimiza mshikamano na ushirikiano kati yao, na kuweka mkazo kwenye maendeleo. Pande zote zimesema uhusiano kati ya China na Afrika utaendelea kuwa uti wa mgongo wa uhusiano wa Kusini-Kusini, na mfano wa kuingwa kwenye ushirikiano wa kimataifa.
Upande wa Afrika umesisitiza kwa mara nyingine tena kuwa utaendelea kufuata sera ya kuwepo kwa China moja, na kuunga mkono muungano wa taifa la China, na juhudi zake za kulinda mamlaka yake na ukamilifu wa ardhi yake.