Kwa watu wenye upeo mpana, kuna mengi ya kujiuliza kuhusu kifo cha Ally Kibao:
1) Ally Kibao, alichukuliwa ndani ya basi la abiria, mbele ya abiria wote. Na waliomchukua wala hawakujificha nyuso zao, na waliingia ndani ya basi, kama watu wenye mamlaka. Jambo la kujiuliza, hivi mnadhani kama hawa watekaji dhamira yao ilikuwa ni kumpoteza tu Ally? Kama lengo lilikuwa tu kumwua, mnadhani walishindwa nini kumteka akiwa kwenye eneo ambalo hakuna watu wengi, na hivyo wasiwepo mashuhuda wa tukio?
2) Ally Kibao alichukuliwa akiwa kwenye basi muda wa jioni, basi ambalo lingefika Tanga usiku. Mnadhani kama walitaka tu kumpoteza, kwa nini wasingemvizia hata huko Tanga ambako angefika usiku, na angeshuka kutoka kwenye basi, na kutekwa kwake kungetengeneza maswali mengi, juu ya nani kamteka?
3) Kwa kuzingatia majibu ya swali la 1 na la 2, ni dhahiri, watu waliomteka walidhamiria tendo lile lifanyike mbele ya watu wengi, ili hao watu walioshuhudia walisimlie tukio lile kwa watu wengi, na habari ziwafikie watu wengi. Je, nia hii ya kutaka taarifa ile iwafikie watu wengi ililenga nini?
4) Baada ya kumwua, maiti yake ilienda kutupwa Ununio, eneo la walima mbogamboga. Hivi mnadhani kuwa wauaji walishindwa kuutupa mwili wa Ally kwenye eneo ambalo usingeonekana kiurahisi? Ni dhahiri, waliutupa eneo hilo ili mwili ule uonekane.
Ni dhahiri watekaji wa Ally waliamua kumteka mbele ya watu wengi ili watu wajue kuwa wao wana uwezo wa kumchukua mtu yeyote wakati wowote akiwa kwenye eneo lolote, na hakuna anayeweza kulizuia hilo, wakiamua. Pili baada ya kumwua, waliurejesha mwili wake kwenye eneo la watu ili watu wajue kuwa wao wana uwezo wa kukuchukua muda wowote, wanaweza kukua hata mbele ya watu, na watu wakajua kuwa umeuawa, lakini hakuna anayeweza kuzuia au kufanya kitu kingine chochote.
DHAMIRA YA TUKIO:
Marehemu Ally Kibao, anatajwa kuwa alikuwa mkufunzi wa CHADEMA, hasa vijana, katika mbinu za kufanya siasa zinazolenga ushindi wakati wa uchaguzi, na namna ya kupambana na mbinu zote chafu za CCM. Vijana walimtegemea sana kwa kuzingatia kuwa aliwahi kuwa senior officer wa jeshi, na aliwahi kuwa katibu mwenezi wa CCM mkoa. Vijana walimwona Ally ni mlinzi na mwalimu wao. Kuuelewa ukweli huu, kunatupatia mwanga wa kwa nini watekaji waliamua kumteka mbele ya watu wengi, kisha kumwua na kuirejesha maiti yake. Walitaka wale vijana waliokuwa wakimtegemea wajue kuwa wanayemtegemea si chochote na si lolote mbele yao watekaji, wao wakiamua wanaweza kumfanya chochote, mtu yeyote, wakati wowote, na katika mazingira yoyote, hata uwe katikati ya kundi la watu. Baada ya kumwua walitaka hawa vijana wajue kuwa mkufunzi na mtu wao waliyemtegemea, wao wamemwua, hayupo tena, halafu hawa vijana wajiulize, kama mkufunzi wetu, na mtu tuliyemtegemea anaweza kufanyiwa hivi, je, sisi???
MAUAJI YA ALLY KIBAO NI TERRORISM, iliyolenga kuwatisha wote waliomwona Ally kuwa ni kiongozi na kinga yao.