Hivi punde
JF-Expert Member
- Apr 1, 2017
- 2,554
- 8,587
Bandari ya Dar es Salaam imeendelea kuzivutia kampuni kubwa za usafirishaji duniani, baada ya meli kubwa ya kisasa ikiwa na shehena kubwa zaidi ya magari kuwahi kutia nanga bandarini hapo.
Meli hiyo ya TRANQUAIL ACE (IMO: 9561253) inayomilikiwa na Kampuni ya Mitsui ikitokea moja kwa moja nchini Japan, imetia nanga ikiwa na magari 3,743 ambayo ni mengi zaidi kuwahi kusafirishwa kuja nchini kwa mara moja.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Eric Hamissi amesema kuwa meli hiyo imeandika historia mpya kutokana na kubeba shehena kubwa ya magari.
Meli hiyo iliyotengenezwa mwaka 2009 ina urefu wa mita 199.9 na upana mita 32.2 kwenda chini, ambapo imetia nanga chini ya nahodha, Diardado Garate.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 10, 2021 katika Bandari ya Dar es Salaam, Hamissi amesema kuwa meli hiyo imetia nanga Agosti 9, 2021 na kuanza shughuli ya ushushaji ambao unatarajiwa kumalizika kesho jioni.
Meli kubwa kuwahi kutia nanga nchini na ailiyokuwa imebeba shehena kubwa ya magari ilitia nanga bandarini hapo mwaka 2018 ikiwa na magari 2600.
"Leo ni siku nzuri sana katika historia ya TPA kwa kuweka rekodi mpya kwa kupokea meli kubwa na iliyobeba shehena kubwa zaidi kuja nchini. Hii haijawahi kutokea katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na kubwa zaidi meli hii imetoka moja kwa moja Japan kuja nchini bila kupitia bandari nyingine.
"Kwa hiyo ni jambo jema dunia inakafahamu kwamba, Tanzania tuna bandari bora na ya kisasa yenye uwezo wa kupokea meli zote na ikazihudumia kwa wakati,” amesema Hamissi na kuongeza: “Katika inayoendelea kushushwa, magari yatasafirishwa kwa njia ya barabara kwenda nchi jirani na mengine 798 yanabaki hapa nchini.
"Mtaona ni jinsi gani sasa nchi zetu za jirani zinazotuzunguuka zimeenza kutuamini, kati ya magari yaliyoingia asilimia 65 yanakwenda kwenye nchi hizo."
Meneja Kampuni ya Inchcape Shipping Services, John Massawe amesema meli hiyo ina uwezo wa kubeba magari 5,200 na kwamba imetumia siku 20 ikiwa safari hadi kuwasili.
"Tumekuwa tukihudumia kampuni ya magari kwa miaka zaidi ya 20, na hii ni meli ya kwanza hivyo tunatarajia huu ni mwanzo wa kuleta meli nyingine kubwa zaidi," amesema Massawe.