Parabolic
JF-Expert Member
- Dec 3, 2013
- 2,922
- 3,252
Baada ya kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano, Dk Mwigulu Nchemba ana kibarua kigumu kuisafisha Serikali na uvunjifu wa haki za binadamu uliofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama kwenye maandamano yaliyofanyika siku ya uchaguzi Oktoba 29, 2025.
Novemba 24 Dk Mwigulu alifanya ziara kwenye miundombinu ya mabasi yaendayo haraka (BRT), ambapo alifanya mkutano Mbezi Luis, ambapo alitangaza maamuzi mbalimbali, likiwemo la kufungulia kanisa la Glory of Christ (Ufufuo na Uzima).
Katika hotuba yake, Dk Mwigulu alizungumzia maandamano ya Oktoba 29, akitoa kauli zinazozidisha maswali mengi Zaidi. Kwa mfano alidai kuwa baadhi ya waandamanaji walikuwa na silaha za moto, mara walikuwa hawajui Kiswahili na pia alihoji kama wananchi wanajua kwamba polisi nao walipata madhara.
Kwa kauli hizi, maswali yanaibuka kwamba, hao wageni walioandamana waliangiaje nchini? Kwamba mipaka yetu haina ulinzi, mtu yoyote anaweza kuingia na kushambulia majeshi yetu?
Haya, wameingia na silaha wamekamatwa? Wako wapi? Mbona hati ya mashitaka ya vijana waliokamatwa hakuna mgeni aliyekamatwa?
Kauli kama hizo amezirudia tena alipozungumza na wahariri na waaandishi wa habari Novemba 25, akisisitiza kuwa yale hayakuwa maandamano bali vurugu.
Kitu kikubwa kilichoibuka kwenye mkutano wake na wahariri ni swali kuhusu idadi ya watu waliokufa katika vurugu hizo, ni wangapi? Maana Dk Mwigulu alitaja pikipiki 2,268 ziliharibiwa, magari binafsi 1,642, magari ya Serikali 976, ofisi za Serikali 756, vituo vya mafuta 672, nyumba 273, vitui vya polisi 159, vituo vya mwendokasi 27 na mabasi sita.
Lakini hakuthubutu kutaja watu wangapi waliuawa au waliojeruhiwa, maiti nyingine ziko wapi mpaka watu wanazika nguo badala ya maiti?
Badala yake Dk Mwigulu akawa anapiga porojo tu za kisiasa, mara itakuwa ni kuwapa sifa walioanzisha hayo maandamano, mara hilo ni jambo kubwa, mara maiti zingekuwepo mji mzima ungetoa harufu.
Lakini hayo yote ni kuficha ukweli kuhusu uvunjifu wa haki za binadamu uliofaywa na vyombo vya Serikali.
Tungetarajia kumwina Dk Mwigulu akifanya ziara kwa watu waliofiwa akawafariji, akatoa suluhisho kwa watu waliofiwa wakakosa maiti zao, huo ndio utu. Lakini tunaona viongozi wa Serikali wanalilia vitu vilivyoharibika tu.
Novemba 23, Msemaji mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa habari ya watu waliokufa waipleke kwenye Tume Huru ya Kuchunguza uvunjifu wa Amani iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan. Kama ni hivyo, kwa nini vitu vilivyoharibika navyo kwa nini visisubiri hiyo tume ichunguze?
Hizi zote ni juhudi za kuficha uvunjifu wa haki za binadamu uliotokea Oktoba 29, achilia mbali tu uchaguzi ulivyoendeshwa. Tayari ripoti za awali za Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na ile ya Afrika Mashariki zimebainisha kuwa uchaguzi haukuwa huru wala wa haki. Yaani kwa kifupi, Tanzania imechafuka kimataifa.
Waswahili wanasema la kuvunda halina ubani. Kuficha uovu mkubwa namna hii ni sawa na kuficha moto, moshi unatokea nje.